Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Asha Salum Motto

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ASHA S. MOTTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Mifugo na Uvuvi ina mchango mkubwa sana katika uchumi wa nchi yetu imechangia takribani asilimia sita ya pato la Taifa (GDP), lakini pia ni chanzo kikuu cha kipato, usalama wa chakula na lishe bora. Kupitia uzalishaji wa mazao kama nyama, maziwa,ngozi na samaki sekta hii imeendelea kuimarisha viwanda vya ndani na kuongeza mauzo ya nje na kuweza kuongeza fedha za kigeni zinazo chochea ukuaji thabiti wa uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Uvuvi na Usindikaji wa Mazao; ninapenda kuipongeza sana Serikali kwa dhamira yake ya dhati kwa wananchi na kuthibitisha kwa vitendo kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta hii kwa lengo la kumkomboa mwananchi kiuchumi na kuliletea Taifa maendeleo endelevu. Serikali imewekeza kwa kutoa mikopo ya boti za kisasa kwa wakazi wa mikoa ya pwani hususani Mkoa wa Mtwara. Mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali pia ilitenga shilingi bilioni 9.5 kwa ajili ya kutoa boti 100 za kisasa na boti saidizi 76 kwa wananchi wa mwambao ili kuwezesha wavuvi wadogo wadogo ikiwemo Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uwezeshaji wa Vijana na Wanawake BBT - Uvuvi: kupitia programu ya jenga kesho iliyo bora (BBT-UVUVI) Serikali imetoa hundi ya shilingi 7,000,000,000 kwa ajili ya kuwapatia mitaji vijana waliohitimu mafunzo ya ukuzaji viumbe maji na uvuvi kibiashara. Wananchi wa Mkoa wa Mtwara tayari wanatumia rasilimali zinazotokana na bahari ingawa uvuvi wa kwenda maji marefu unafanywa zaidi na wanaume na zaidi ya 70% ya shughuli za uchakataji na uuzaji wa mazao ya baharini zinasimamiwa na wanawake ikiwemo kufuga majongoo, zao la mwani, usindikaji unahusisha uongezaji thamani wa samaki, dagaa, ngisi na pweza, prawns ili kuwafanya wadumu kwa muda mrefu kabla ya kufika sokoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi za Serikali, bado kuna changamoto katika sekta hii ya uvuvi kama ifuatavyo:-

(1) Uhaba wa mitambo ya kisasa ya kuchakata mazao hayo;

(2) Changamoto ya masoko na Dijitali;

(3) Mila potofu zinazo kandamiza wanawake kuhusu kumiliki mali;

(4) Uhaba wa vinu vya barafu;
(5) Teknolojia duni ya kukausha;

(6) Hakuna viwanda vikubwa vya kukausha na kusindika bidhaa;

(7) Gharama kubwa za Nishati ya umeme;

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuishauri Serikali mambo yafuatayo kuboresha zana, miundombinu na teknolojia juu ya ukaushaji wa bidhaa na kutoa mafunzo ya kuongeza thamani ya bidhaa hizo; Kuwezesha vifaranga vya samaki na kamba ili kuongeza uzalishaji; Kujenga na kuongeza vizimba vya kufugia samaki na kamba; Kudhibiti uvuvi haramu; na Uhifadhi wa mazingira

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Mifugo Mkoani Mtwara, kihistoria ni mkoa unaotegemea kilimo cha korosho na shughuli za uvuvi, hali inayofanya mwamko wa sekta ya mifugo hususani n'gombe, mbuzi na kondoo kuwa chini ikilinganishwa na Mikoa ya Kanda ya Kaskazini au Kanda ya Ziwa.