Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Mhe. Dickson Nathan Lutevele

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. DICKSON N. LUTEVELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii pamoja na Naibu wake. Kimsingi tumeona kazi kubwa ambayo wanaifanya na sisi kama Waheshimiwa Wabunge tunaendelea kumpa moyo Mheshimiwa Waziri. Yako maeneo mawili ninaomba kutoa mchango wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tumesikiliza na kuangalia michango mingi sana kwenye Ufugaji na Uvuvi, unaona watu wanaoinuka ni wale walioko kwenye Kanda za Maziwa au kule ambako kuna wafugaji wengi. Sasa ninaomba nitoe ushauri. Ushauri wangu ni kwamba, sasa hivi kufuga siyo tena issue ya kanda, sasa hivi kufuga ni biashara, kufuga ni fursa. Tumeona soko kubwa la maziwa sasa hivi hapa nchini kwetu. Wafanyabiashara wanajenga viwanda vya maziwa. Tumeona, ili uweze kula samaki, kwa mfano sisi tunaotoka Nyanda za Juu Kusini, ama awe ametoka Mwanza au awe ametoka Mtera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo unaona kwamba, soko kubwa la samaki lipo, lakini kama Wizara haijaja na mikakati mahususi ya kuhakikisha kwamba kila sehemu kunakuwa na fursa za mtindo huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaenda kwa mfano kwenye Uvuvi. Ninaomba kuishauri Wizara, iweke mpango yakinifu. Hapa tumekuwa tukizungumza sana kuhusu ajira za vijana, lakini ajira kubwa sana ya vijana tungeweza kuiweka pia kwenye uanzishwaji na uendelezaji wa mabwawa ya samaki; iwe ni ajenda ya Wizara. Leo hii tunasimama hapa watu wa maziwa walioko kandokando ya ziwa, wanavuta vizimba. Wako watu wanalalamika ufungwaji wa Ziwa Tanganyika; lakini kumbe tungekuwa na mbadala hata hawa wasingekuwa wanalalamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba kuishauri Wizara, ianze kuangalia namna bora; wakati tunafunga ziwa, kuwe kuna vijana au kuna wafugaji wa samaki ambao hawategemei ziwa. Tuanze kujifunza kutazama namna gani tunaachana na yale mazoea, kwamba samaki lazima atoke ziwani, kumbe samaki anaweza kutoka kwenye bwawa. Huo ni mfumo ambao mataifa mengi wanafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe mawazo yangu pia kwenye mifugo. Sasa hivi soko la nyama limekuwa kubwa sana, soko la maziwa limekuwa kubwa sana. Tunaomba tuuone mpango wa wizara. Wizara iache kutembea kwenye mipango ya zamani ije na mpango mpya wa namna gani watu wa Nyanda za Juu Kusini wanashiriki kwenye kufuga ng'ombe wa nyama na kushiriki kwenye kuzalisha maziwa ili viwanda vilivyopo Tanzania vianze kupata maziwa kutoka humu humu ndani. Ni fedheha sana kwa Taifa letu kuagiza maziwa kutoka nje wakati ndani wapo watu wanalalamika hawana ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi tunategemea ubunifu na umahiri wa Mheshimiwa Waziri tuuone kwenye kuendeleza maeneo haya ambayo hayana historia ya ufugaji wa samaki, wala hayana historia ya ufugaji wa ng'ombe wa nyama na wa maziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huo, ninaomba kushukuru na ninaunga mkono hoja. Hata hivyo, sisi tunasubiri tuone mapinduzi katika maeneo hayo. (Makofi)