Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nachingwea
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. FADHILI A. LIWAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Ninaungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Dkt. Balozi Kakurwa kwa kazi kubwa na namna ambavyo anahuisha shughuli za sekta hii ya uvuvi na mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba uniruhusu nijielekeze kwanza kwenye kupongeza namna ambavyo hotuba hii imechagiza na imetoa mwelekeo kwenye vipaumbele vya msingi ambavyo sisi kama Taifa tunatamani kupiga hatua kwenye eneo hili la mifugo na uvuvi. Mimi ninatoka Jimbo la Nachingwea na ninaanza kabisa kwa kuleta ombi kwa Mheshimiwa Waziri, kwamba, ninakuomba sana, moja ya maeneo ambayo ninatamani afike, aje kutembea, lakini pia kuona kazi kubwa ya kilimo na shughuli hizi za mifugo, basi ni Nachingwea na ninazo sababu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Watanzania ni wamoja na Waheshimiwa Wabunge wenzangu watakubaliana na mimi kwamba tumeshaweka msingi wa Kitaifa kwamba Mtanzania yeyote atafanya shughuli yoyote mahali popote. Mimi binafsi ni muumini kabisa wa kupokea shughuli zote zinazofanywa na Watanzania. Moja kati ya shughuli ambazo nazithamini na kuziheshimu ni shughuli ya ufugaji, lakini lazima niweke rekodi yangu sawasawa. Mimi ni mtoto wa mkulima na nilishawahi kuwaambia baadhi ya watu kwamba pia ni mwindaji; lakini kwa sababu jamii ya Wanachingwea ni wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu Nachingwea imezaliwa, tangu wakoloni wameondoka kwenye mashamba, kuanzia shamba namba moja hadi shamba namba 19, hakuna wakati ambao wamewahi kupigana vita ya kugombea ardhi wala kugombea chakula. Katika siku za hivi karibuni kumeibuka tatizo kidogo na hapa ninaomba nieleweke, kwamba ufugaji tunaupenda na mimi ni mdau namba moja wa wafugaji. Hata hivyo, kilimo pia ndiyo maisha ambayo yametukuza baadhi ya Waheshimiwa Wabunge humu ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba, baadhi ya maeneo ikiwemo Nachingwea, suala la mifugo limegeuka kuwa changamoto na ni changamoto ambayo kila kunapokucha inaibua matatizo na mnyukano baina ya jamii zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi wakati wa kampeni nikiwa ninaomba ridhaa ya wananchi, 75% ya jimbo langu nililoomba kura wananchi walilalamikia juu ya mgogoro wa mifugo kwenda kwenye mashamba ya wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wafugaji wamegawanyika; wako wafugaji ambao wanaijua taaluma ya ufugaji kwa kufuata misingi na taratibu zilizowekwa. Hawa tunawafahamu vizuri kabisa na wako hapa, lakini wako wafugaji wamejificha kwenye kivuli cha kutokujua sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti ninataka kuwaomba sana, kundi lolote la wafugaji ambalo linajificha kwenye kivuli cha kutokujua sheria ni makusudi ya kuvunja sheria. Wataalam wa sheria watanikubalia kwamba kutokujua sheria hakuwezi kukupa nafasi ya kufanya makosa. Kwa hiyo kule kwangu ninapata shida sana, na majimbo mengine ya Kanda za Kusini, kwa sababu kumekuwa na tabia ya makusudi kabisa ya wafugaji kuchukua mifugo kwa makusudi kutoka kwenye maeneo waliyopangiwa, kwenda kulisha kwenye mbaazi. Mbaazi Nachingwea ni biashara, tunasomesha, tunajenga na tunakuza uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki cha msimu wa mahindi, ninataka kumwambia Waziri, pale mahindi yatakapoanza kuvunwa, moja ya changamoto tutakayokutana nayo ni pamoja na wafugaji kupeleka mifugo yao mashambani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimewaambia ninawapenda sana wafugaji na kule Nachingwea nimewaruhusu. Sasa tufanye vikao na Mheshimiwa Waziri anisaidie, nimpate kiongozi wa wafugaji ili tuongozane. Kwenye jimbo langu sitaki wapigane, ninataka tufanye vizuri, tuwe na sherehe kabisa siku ya wafugaji na wakulima kuondoa haya matatizo. Wafugaji watoe ng'ombe, watoe mbuzi tuchinje na wakulima wenzetu watoe mahindi, watoe mpunga na mtama tupike wali tucheze ngoma. Watu waoane; wafugaji na wakulima wa Nachingwea, tuzaliane tujue ufugaji ni biashara, kilimo ni biashara na kuishi pamoja ni maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini ninayasema haya? Ninasema kwa uchungu mkubwa kwa sababu rekodi zangu hapa zinanionesha, katika kipindi cha miaka mitatu, moja ya athari tulizozipata, jumla ya ekari zilizoharibiwa za mazao ya chakula ni ekari 115, lakini mazao ya biashara ekari 165 zimeharibiwa. Nachingwea peke yake watu waliopoteza maisha ni watu saba kwa kupigwa mishale. Ninataka kukwambia, siyo kwa kuchekesha, mfugaji unayemsikia na analenga mshale hakuna mfano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, alishapigwa mwalimu wangu mshale jichoni umetokea upande wa pili; this is not just a story, kwamba ninachekesha, ni kitu ambacho kimetokea kabisa, watu saba. Watu 23 Nachingwea wamejeruhiwa na wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika matukio haya huwezi kukuta mkulima amempiga mfugaji. Unajua ni kwa nini? Sababu ni moja tu, mkulima wa Nachingwea, mkulima wa Ruvuma, mkulima wa Kilwa, mkulima wa Liwale, hajui kurusha mshale, hajui kurusha jembe, hajui kurusha shoka wala rungu. Anajua kutumia jembe kwa kulima shambani, anajua kutumia upanga kwa kukata mafukutu ili aweze kufanya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimwomba Mheshimiwa Waziri, anisaidie mtoto wake na kijana wake, aniangalie hapo kwenye screen kwa jicho la huruma. Moja ya jambo ambalo nimeji-commit kwa wananchi wa Nachingwea ni kwenda kuhakikisha kwamba tuna-harmonize situation ya mgogoro huu ili uwe salama. Baba yeye atanisaidia, ninamwomba sana twende Nachingwea tukakae na wakulima, tutafute viongozi wa kimila wanaohusiana na jamii hizi ili tuweze kuzungumza lugha moja tufanye maisha ya pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)