Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, ninamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetujalia afya. Pili ninawapongeza Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niende moja kwa moja kwenye hoja kulingana na muda tulionao. Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamezungumzia suala zima la migogoro ya ardhi. Suala la migogoro ya ardhi nchini limekuwa ni donda sugu. Suala la migogoro hii sielewi, nilisikia Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuwa kwenye ziara zake akasema hataki kuona wataalam ama watumishi wa Serikali wakizoea shida za Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninashangaa, shida za Watanzania ni pamoja na suala la migogoro baina ya wafugaji na watu wa hifadhi na vilevile baina ya wafugaji na wakulima wetu. Ni nini shida? Nini changamoto? Ni tatizo gani ambalo linasababisha Serikali kutokuitatua migogoro hii, ili kila mmoja wetu ndani ya nchi hii aweze kuishi kwa amani na utulivu na kwa haki anayostahili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Wizara ikija, ituambie, changamoto ni nini kwenye suala la kuwapatia wafugaji maeneo yao mahususi ambayo wanastahili kuweka mifugo yao kwa ustaarabu na kupewa huduma nyingine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo, kaka yangu Mheshimiwa Getere ametoka kusema hapa; suala la nyama humu ndani tukiulizana leo nani ambaye hajala nyama, nani ambaye hajanywa maziwa hayupo. Lakini ng'ombe hawa tumekuwa tukiwaona ni adhabu, ng'ombe hawa tumekuwa tukiona ni laana, kitu ambacho si sahihi; na sisi kama Taifa pia hatujitendei haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfugaji huyu leo ndiye anayesomesha watoto wake kwa kutumia fedha ya mifugo yake, bila Serikali kumpelekea josho, bila Serikali kumpelekea bwawa, bila Serikali kufanya chochote. Anahangaika mwenyewe kwa jitihada zake. Anasomesha watoto wake, analisha familia yake na mambo mengine. Wakati wengine tumekuwa tukiwatumia wafugaji hawa kwenye shughuli zetu mbalimbali; hata za Kiserikali. Tuna mwenge, tunawafuata wafugaji watupe ng'ombe ili tupate kitoweo. Kwa nini hatutaki kuwathamini wafugaji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe, suala la migogoro ya ardhi kwa wafugaji, twende tukatatue tatizo hili ili tuwaache hao wafugaji waweze kuishi maisha yenye amani na utulivu ndani ya Taifa lao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la pili ambalo ninatamani kulisema ni kuhusu mikopo kwa wafugaji. Mfugaji wetu kitu pekee anachoweza kuweka dhamana ni ng'ombe, kwa sababu ndiyo biashara anayofanya. Leseni yake kubwa ni mifugo yake; lakini leo wafugaji hawawakopeshi wanawaambia kwamba ng'ombe hawezi kuwa dhamana. Kwa nini, eti kwa sababu hana uhai, anaweza akafa, anaweza akaugua, anaweza akafanya nini. Hivi haya maduka yanayoungua Kariakoo na kwingine yanakochomwa moto huko? Kwa nini hawa wafanyabiashara wengine hatuwanyimi mikopo? Kwa nini mfugaji ananyimwa mkopo eti kwa sababu ng'ombe wake anaweza akapata madhara akafa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe pia, kwenye suala la mikopo twende tukatumie mifugo ya wafugaji kama dhamana na sehemu ya kupatiwa mikopo ili waweze kuboresha miundobinu yao pamoja na kuboresha mifugo yao ili tuweze kujikwamua kiuchumi katika maeneo yetu mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la majosho limesemwa; Wilaya ya Chemba ninaomba majosho; Wilaya ya Chemba ninaomba malambo; tuna hali mbaya, hali ni tete. Kwa hiyo suala la majosho na malambo Wilaya ya Chemba ninamwomba Mheshimiwa Waziri atusaidie kwa jicho la kipekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tuna mnada wetu mkubwa sana wa soya, ambapo mnada huu hata Mheshimiwa Rais alivyokuja kuwaomba kura alituahidi kwenda kujenga mnada huu. Lakini kwa kuwa tumekuwa tukisafirisha ng'ombe wetu kwa kuwaswaga lakini na kupakia kwenye magari; tunawaswaga ng'ombe, tunaharibu miundobinu ya barabara; tunawapakia ng'ombe kwenye malori, tunawatoa Kagera hadi Dar es Salaam, foleni ng'ombe wanakufa barabarani wanapata ajali, wakulima wetu wanaendelea kupata hasara. Mheshimiwa Rais alituahidi kutujengea pia kiwanda kwa ajili ya uchakataji wa mifugo yetu ambayo inatokana ndani ya Wilaya yetu ya Chemba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatamani kusikia neno na Wanachemba na wafugaji wa Chemba wanatamani kusikia neno juu ya suala la kiwanda cha kuchakata mifugo inayotoka Wilaya ya Chemba na kwenda kunusuru uharibifu mkubwa unaofanyika kwenye suala la uharibifu wa barabara. Pili, kuokoa maisha ya ng'ombe na hasara zinazomkuta mfugaji kwa kumsafirisha kwa muda mrefu na ng'ombe yule kufariki ama kupata ajali njiani. Tatu, walaji wetu wa nyama kwenda kupata nyama iliyo bora badala ya kwenda kupata manati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninakushukuru kwa muda wako na Mungu akubariki sana, uishi maisha marefu kwa hii nafasi. (Makofi)