Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. BONIFACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Ninamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumteua Ndugu yetu Bashiru kuwa Waziri katika Wizara hii, ni mtu muhimu sana katika maisha yetu, ninamshukuru sana Naibu wake, ninamshukuru sana Katibu Mkuu na viongozi wote na watendaji wote wa Wizara ya Mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Waziri, ndugu yangu Mheshimiwa Kakurwa ujamaa tuliokuwa tunauona enzi hizo siyo ujamaa uliopo sasa hivi. Ujamaa wa zamani viongozi walikuwa wanakaa wanajadiliana wanatenda, saa hizi mnaweza mkajadiliana halafu ukigeuza kisogo hakuna kinachotendeka. Sasa ninamwomba achanganye ujamaa na ubepari kidogo ili mambo yaende saa hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri. Pale Bunda tuliahidiwa na Naibu Waziri aliyekuwepo na bahati nzuri sasa amekuja mwingine...

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa, kwa kifupi.

TAARIFA

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu kwa mujibu wa Katiba ni nchi ya ujamaa na kujitegemea, ninataka nimpe taarifa mzungumzaji, sijui kama anaongea kwa utani au serious, neno ubepari kwamba uchanganywe na ujamaa anafanya makosa makubwa. Ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Boniface Getere unaipokea taarifa hiyo?

MHE. BONIFACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea ni mtazamo wake, mimi nimemwambia Mheshimiwa Waziri kwamba awe mkali, sijasema akatae ujamaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Waziri tafadhali, alikuja Naibu Waziri pale Bunda tulikuwa na kaya 200 ambazo ziliomba ng'ombe wa maziwa na bahati nzuri sasa tuna kiwanda, tuna industrial park ya maziwa kutoka Jambo lakini ng'ombe tuliowapata madume ni 20 tu kati ya 200. Waziri alikuwa ametuahidi kwamba atatupatia ng'ombe 40 tena ili watu wetu sasa wabadilike kwenda kuchunga kule porini, wakawe na maziwa kwa sababu tayari tuna viwanda sasa hivi ninamwomba sana, kwa sababu tunayo mashamba ya Serikali na tuna mashamba ya NARCO na sera ya Serikali huko nyuma mashamba ya Serikali yalikuwa ni kupatia watu mitamba, sheria sasa hivi ninaona kama haipo sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii tuombe mashamba ya Serikali yatusaidie kupata mitamba, yatusaidie kupata madume na NARCO, Mheshimiwa Waziri ndiyo maana ninasema kwamba sasa aone, tusipoangalia haya mashamba ya NARCO yatakuwa ya wafanyabiashara wakubwa tu. Wanakaa, wamepanga mikataba! Mikataba! Mikataba! Akija Waziri mwingine mpya anamwambiwa bwana tayari mashamba yote yana mikataba. Wanasubiri uchaguzi unakaribia tukishaenda kwenye uchaguzi wanaanza mikataba, akija Waziri mpya kuna mikataba! Tusipoangalia hakuna madaraka yoyote atakayofanya kwa NARCO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, NARCO nenda pale Missenyi, maeneo yote yaliyopakana na Uganda wanachunga watu upande wa kule tu. Mashamba makubwa makubwa yapo, mtu anapewa shamba zima ana ng'ombe 100, ana ng'ombe 300, halafu anakodisha. Ninaomba mashamba ya NARCO yaangaliwe mara mbili mbili.

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa, Taarifa. Niko hapa.

MWENYEKITI: Ndiyo Mheshimiwa, itakuwa Taarifa ya mwisho hiyo.

TAARIFA

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kumpa Taarifa Mheshimiwa Getere kwa mchango wake mzuri. Katika Wilaya ya Misenye tuna vitalu vingi vya mifugo, lakini vitalu hivyo hakuna hata kimoja ambacho kina mwananchi kutoka nje ya Tanzania. Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia imeweka Depo ya Jeshi wanalinda mipaka yetu vizuri na wananchi wa Wilaya ya Misenyi wanaendelea kufaidi matunda ya Tanzania. Ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Boniphace Getere, unapokea Taarifa hiyo?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea. Sasa nisipokee ninafanyaje wakati tunawatetea watu wetu na watu wa kule, ni jamaa zetu sana. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tafadhali, tulikuwa na mnada wa ng'ombe pale Mikomaliro. Mnada ule mnada wakautoa. Hivi kuna vigezo gani vya kuondoa watu wanataka study yao? Sisi vijijini minada ni study tour, sasa watu wameanzisha mnada wao umekaa pale miezi 12 halafu unauondoa, wala hakuna mapato, watu wanalia kila siku. Nitakwenda ofisini kwa Waziri tuangalie namna gani ya kurudisha ule mnada ili watu wa kule waweze ku-enjoy.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Bashiru, hivi kweli; unajua katika Bunge hili ndiyo maana kuna Waheshimiwa Wabunge fulani tunaungana pamoja, kisha tunakuwa ma-group. Hivi ni nani alipanga ratiba ya siku moja kwa hii Wizara? Ni nani na ni kwa namna gani? Hivi kweli wizara hii ambayo inalisha watu nchi nzima? Ukitaka maziwa ni ng'ombe, ukitaka ngozi ni ng'ombe, ukitaka nini ng'ombe, leo wanakula balenge humu ndani, kwato, balenge, ng'ombe, kila kitu ng'ombe, inapangwa siku moja! Haiwezekani…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Getere, hoja ya ratiba siyo sehemu ya mjadala, kwa hiyo jielekeze kwenye mjadala ulioko Mezani…

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mjadala wangu ni kwamba, nimwombe Mheshimiwa Waziri, baada ya bajeti hii kupita, tunaomba tukae sisi wafugaji na wakulima pamoja tutoe matatizo yetu. Tupate nafasi ya kukaa na Mheshimiwa Waziri. Matatizo ya ng'ombe ni mengi. Kwa hiyo akimaliza hii hoja ya bajeti yake, tukae pamoja. Suala la kuhusu utaratibu asizingatie, atuite tu twende, hatutamhoji chochote, tunampelekea hoja tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafadhali sana, ninaomba kwa kweli siku nyingine wanaopanga ratiba wasiweke hivyo, wanatuumiza. Ninakushukuru. (Makofi)