Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muleba Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ADONIS A. BITEGEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kupongeza jitihada za Serikali chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa namna ambavyo anatoa kipaumbele katika sekta hii ya mifugo na uvuvi. Tumeona, dhamira yake ya dhati kabisa kuleta mageuzi katika sekta ya mifugo na uvuvi. Niwapongeze pia Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipata bahati baada tu ya kuapa, kupata ziara ya Mheshimiwa Waziri pia Naibu Makatibu Wakuu nao walikuja, kipindi hicho wakiwa bado hawajakuwa kwenye nafasi hizo ninashukuru sana nimeona kwamba wana nia ya dhati kabisa kuleta mageuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia hotuba ya Waziri na nimefurahishwa sana na mikakati ya Serikali, hasa katika kufanya ufugaji wa kimkakati pamoja na uvuvi wa kimkakati. Nimeona dhamira ya dhati ya Serikali katika kuwekeza au kuvutia uwekezaji katika ufugaji wa mifugo hasa kwa kuongea mikataba na wale wafugaji wakubwa wanne, kuwekeza zaidi katika kile kituo chetu cha umahirishaji wa mifugo cha NAIC cha Arusha, lakini pia katika kuendeleza mashamba ya mitamba ya mifugo na kuweza kuvutia uwekezaji zaidi katika vitalu vya NARCO. Imani yangu ni kwamba kupitia vitalu vya NARCO tutapata wawekezaji zaidi wakubwa ambao watafuga kisasa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefurahishwa pia na nia ya dhati ya Serikali pamoja na Wizara kuona kwamba tunaimarisha ulinzi wa rasilimali za maji, yaani rasilimali za uvuvi, pamoja na kuziendeleza. Ninategemea kwamba katika upande huu basi wa Uvuvi, basi uvuvi utakuwa unazingatia sheria, lakini pamoja na kuendeleza yale mazao ya maziwa yetu pamoja na bahari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uchache wa muda nitaongea machache. Jambo la kwanza nitaanza katika sekta ya uvuvi na kwenye sekta ya uvuvi nitajikita zaidi katika Wilaya yetu ya Muleba, hasa katika Jimbo la Muleba Kaskazini ambalo mimi pia ni mwakilishi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa tuna changamoto kubwa ya raia wa kigeni kuingia katika ziwa letu la Victoria. Sisi tulitarajia kwamba, kwa vile Serikali imewekeza zaidi katika masoko ya mazao ya uvuvi, basi wale raia wa kigeni watakuwa wanaenda kule kununua aidha dagaa au samaki katika yale masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ambacho tunakiona ni kwamba, hawa raia wa kigeni wanaingia na kwenda kwenye visiwa na kununua samaki na dagaa. Ninaamini kabisa, nia ya dhati ya Serikali ilikuwa ni kwamba kuwawezesha wananchi waweze kwamba, wao ndiyo wavue, lakini pamoja na kuja kuleta kwenye masoko kwa ajili ya kuuza, lakini tunapoona raia wa kigeni wanafika na kuingia kwenye ziwa na kuvua, hasa kwenye Visiwa vyetu vya Kelebe na Goziba, hii inatayarisha kabisa ustawi wa jamii pamoja na uchumi wa wananchi wa Wilaya ya Muleba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na hivyo ni kwamba tuna changamoto nyingine ya uvamizi kwenye Ziwa Victoria, hasa upande wa Muleba kuna raia wa kigeni, wanakuja wanavamia wale wavuvi na kuwajeruhi pia kuwapora dagaa na samaki wao. Kwa hiyo, ninadhani ni kwamba Serikali inapaswa ijipange sasa katika eneo hili kuona kwamba tunakuwa na ulinzi au kufanya doria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, kimetoa ahadi kwamba kitanunua boti tatu za doria katika upande wa ziwa, upande wa Wilaya ya Muleba. Ninaamini kabisa tukinunua hizi tupate hizi boti tatu, pamoja tukiimarisha na ulinzi wa doria katika ziwa letu tutaweza kukabiliana na hawa raia wa kigeni ambao wanaingia na kuvamia wavuvi wetu pamoja na kuwapora dagaa au samaki wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ni la msingi ambalo ninaomba pia Serikali ione na nimeona hapo kwenye bajeti wamelisisitiza ni kwamba, Serikali imejipanga kuona kwamba inajenga na kuendeleza Soko la Mazao ya Uvuvi la Kyamkwikwi lililopo Kata ya Izigo. Ninaamini kabisa Mheshimiwa Waziri alishafika pale akaliona, lile soko limefikia 26%, ninaamini kwamba Serikali itawekeza zaidi ili kuona soko hili linakamilika ili wananchi waweze kupata thamani ya uvuvi wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la kumalizia ni kwamba kwenye Wilaya ya Muleba tuna changamoto ya uhaba wa chanjo ya ugonjwa wa miguu na midomo ya mifugo yetu, ninaomba sana Wizara iliangalie hili ili kuona kwamba tunapata chanjo hii kwa kupitia ruzuku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba pia tuna uhaba na changamoto ya wataalam wa mifugo. Tunao wachache, Wilaya ya Muleba ina Kata 43, lakini tunao wataalam 21, tunaomba sana Serikali iliangalie hili pamoja na kuwawezesha pia pikipiki. Kwa upande wa majosho pia tuna uhaba wa dawa za kuogeshea mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niishie hapo na ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)