Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi jioni ya leo. Kwanza kabisa ninaomba nirekebishe kidogo jina langu, Mwantumu Mzamilu Zodo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya dhati ya kutaka kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na sisi tumekuwa tukishuhudia, lakini ninaomba niwapongeze Wizara pamoja na Waziri na watendaji wote kwa Wizara hii. Nimeipitia bajeti yote na nimeisoma kwa umakini sana, nimeona mikakati yao, mikakati ni mizuri kama itatekelezwa ipasavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwasi wangu, kabla sijaenda kwenye mchango ni bajeti. Mimi kama alivyoongea msemaji wa mwisho kabla yangu, ninaomba Serikali ijaribu kuiangalia Wizara hii kwa jicho lingine tena kwa sababu bado hatujapitisha ile bajeti kuu. Nimeshtuka sana kuona zile fedha kwa ajili ya maendeleo, badala ya kuongezeka zinapungua na hapa kila Mbunge akisimama anaomba majosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kuna Mbunge mmoja tu hapa alisimama peke yake tu akaomba majosho 20. Bado wengine na wengine hawajasimama. Sasa kwa bajeti hii, ninapata wasiwasi kidogo, kwa hiyo niiombe sana Serikali yangu sikivu ijaribu kuiangalia tena kwa mara ya pili, Wizara hii muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tunayo changamoto kubwa ya ajira. Tukitoa watu walioajiriwa Serikalini na sekta binafsi, sekta ambazo zinatoa ajira ni sekta ya kilimo, uvuvi pamoja na mifugo, kwa hiyo hii ni moja ya sekta ambazo zinatoa ajira, kwa wananchi wetu, kwa vijana, wazee, akina mama. Kwa hiyo ni Sekta muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizipongeze jitihada za Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mfano, kama sisi Tanga mwaka jana alileta zile boti za uvuvi, tulipata boti 38, Sisi tuna wilaya nane, lakini Wilaya nane kati ya Wilaya nane, Wilaya nne zote zimepitiwa na bahari na wananchi wetu shughuli zao kubwa kule ni uvuvi, lakini changamoto kubwa walikuwa wanavua kwa kutumia zile kokoro ambazo sasa hivi hazitakiwi kabisa na zinapigwa vita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wakishaachana na zile nyavu ambazo hazitakiwi, wanakuwa hawawezi kwenda kwenye shughuli zao za uvuvi, kwa sababu hawana hivi vifaa vya kisasa ni gharama kubwa na Wizara peke yao hawawezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru sana hawa wadau wa taasisi za kifedha kama CRDB, NMB na Benki yetu ya Kilimo, hawa wamekuwa ni msaada mkubwa sana. Sasa kwa mfano kama mwaka jana, zile boti 38, katika Wilaya ile moja tu ya Tanga, maana yake tuna Wilaya nne pale za Uvuvi. Wilaya ya Tanga tulipata boti 15 tu na kati ya hizo boti 15, walioomba, ilikuwa ni vikundi 47. Kwa hiyo sasa hapo unaweza ukaona, vikundi 32 vyote bado havikupata boti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vikundi vina watu kumi kumi na wale hawawezi kwenda kuvua kwa sababu wana zile nyavu za bei rahisi. Ile boti ikija inakuja na package yote na zile nyavu za kisasa ambazo zinatakiwa. Hii boti moja ni 135,000,000 mpaka 160,000,000. Mwananchi wa kawaida, wa kipato cha kawaida, hawezi kumudu kununua hii boti bila ya aidha kupata msaada wa Serikali au kupata mkopo kupitia kwenye hizo taasisi za kifedha ambazo nimezitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sasa unaweza ukaona kama vikundi 32 vilibaki, vyenye watu kumi kumi, ina maana kuna watu zaidi ya 300, ambao wana familia, hawawezi kwenda kutafuta kile kipato chao cha kila siku. Mwaka huu tuna maombi ya vikundi 35, mwaka jana vimebaki 32, lakini bado tuna maombi ya vikundi 35. Kwa hiyo unaweza ukapata hiyo picha na hawa watu ni wale wanaotegemea uvuvi, ili walipe ada wanategemea Uvuvi, ili walipe kodi wanategemea uvuvi na sasa hivi hawawezi kwenda kuvua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niwaombe sana Wizara, wajaribu kukaa chini, lakini washirikiane na hizi taasisi za kifedha ili kuokoa maisha ya hawa wananchi, sasa hivi hali zao ni duni kimapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama muda wangu umekwisha, ninaunga mkono hoja, mengine nitaandika kwa maandishi. (Makofi)