Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka 2026/2027. Ninaanza mwanzo kabisa kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa ambayo anaifanya, lakini pia, kwa msaidizi wake, Naibu Waziri, kwa kipindi chote toka ameteuliwa tunaona kazi kubwa, ambayo anaifanya ya kumsaidia Waziri na Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza pia Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu pamoja na watumishi wote walioko katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Baada ya kusema hayo, ninatoa salamu za kipekee kabisa za wananchi wa Hanang kwa moyo wao wa shukrani, hasa wafugaji, kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusababisha sasa angalau wameanza kupata mikopo katika Benki ya CRDB. Hili tunamshukuru sana na ninaomba salamu hizi zimfikie Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wafugaji wanampenda na wanamshukuru sana kwa hatua hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ni ambayo inaweza kuisaidia sana nchi yetu katika kupata fedha za kigeni na fedha za ndani. Wizara hii bila kuwa na miundombinu bado tutaendelea kuona kwamba, hii sio Wizara ya kimkakati ya kuleta fedha kwa kiasi kikubwa, fedha za kigeni pamoja na fedha za ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii lazima ijiwekeze katika majosho. Kama tunahitaji kuwa na mifugo ya kisasa, yenye tija, ninaamini tutatoka kuwa wa pili katika Afrika tutakuwa, kama kuna namba nyingine zaidi ya moja, basi tunaweza tukawa namba nyingine zaidi ya moja. Kwamba, tukawa tumefanya kwa ukubwa wake na tukazalisha siyo tu kuwa wa 10 kidunia, tukawa wa pili, watatu au wa kwanza huko kidunia na Afrika tukawa wa kwanza kwa sababu, ya miundombinu na uwekezaji mzuri katika kuhakikisha mifugo yetu inapata malisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nje ya majosho inaenda sambamba kabisa na mabwawa. Ni lazima tuhakikishe kwamba, tunapata mabwawa na mabwawa haya yanaweza kutoa fursa kubwa, siyo tu kwenye mifugo kama ng'ombe, mbuzi, kondoo na kadhalika, lakini pia, kwenye mabwawa tunaweza kupandikiza na kuwekeza samaki na vijana wengine wakaweza kupata ajira. Mbali zaidi tunaweza pia, kutumia mabwawa haya, yakiwa makubwa, basi yakaweza kusaidia kwa upande wa kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la watumishi katika Wizara hii, mimi ninatolea mfano wilaya yangu, wilaya yangu ina uhitaji wa watumishi 129, lakini waliopo ni watumishi 25. Nina upungufu wa watumishi 104, hii unaona kabisa ufanisi hauwezi kuwa na malengo ya Dira 2050 kwa sababu watumishi ni wachache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata ruzuku ya madawa, lakini madawa au elimu inayohusiana na masuala ya Mifugo, Wizara hii imejitahidi kwa sasa hivi mnaona mpaka wanauza mbegu za majani, lakini ni nani ambaye anapeleka taarifa kwa mwananchi kule Gidahababieg, kwa mwananchi kule Bassotu, kwa mwananchi kule wa Bassodesh ili waweze kupata taarifa sahihi? Ni lazima tujiwekeze katika kuajiri watumishi katika Wizara hii na hususani kwenye kata zetu na vijiji vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, bila kuwa na watumishi ni lazima wananchi wetu waendelee kuonewa. Wataonewa katika huduma za madawa zinazotolewa. Huduma za madawa nani anadhibiti? Nani anachoma sindano kule chini kabisa kwenye vijiji vyetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nina wataalam 25, nina upungufu wa wataalam 104, maana yake ni kwamba hatutakuwa na uwezo wa kuzalisha ng'ombe bora, tutakuwa na uwezo wa kuzalisha ng'ombe ambao tunakimbizana nao mnadani na wanatusaidia tu hapa ndani kwa kula kinyonge na kiubishi hivyo hivyo. Ni lazima tujiwekeze kabisa katika wataalam ili pia tuweze kudhibiti bei na wananchi wetu hususani wafugaji waweze kuendana na Dira ya 2050.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la minada. Ninatolea mfano na hapa ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, nina minada mikubwa minne ya ng'ombe. Mnada wa Endagaw, mnada wa Bassotu, mnada wa Bassodesh, mnada wa Katesh. Fedha hizi ambazo wanachukua mapato kupitia uuzaji wa ng'ombe, tunaomba sana Wizara ijitahidi kurejesha ili kuweza kuboresha miundombinu baada ya wao kuchukua zile fedha ambazo wanaziokota kule kwenye minada baada ya mauzo yetu ya ng'ombe, basi zirudi ili zitengeneze miundombinu mizuri na tuweze kuhakikisha kwamba tunaendelea kuboresha sekta ya mifugo na sekta ya uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kusema kwamba, Wizara hii lazima iwekeze kwa watu wake ambao ni wafugaji. Wafugaji hawaeleweki katika ardhi yao ya Tanzania. Mfugaji anakutana na TFS, mfugaji kwenye kijiji anakutana na mkulima, mfugaji amekuwa ni sehemu ya kuhamahama, hajui kesho asubuhi ataamkia wapi. Bahati mbaya sana, mfugaji akikamatiwa ng'ombe, amenusurika sana amepigwa faini, lakini wakati mwingine wafugaji ng'ombe zao zinataifishwa na hili halifanyiki huku juu, linafanyika na watendaji wa chini ambao siyo waaminifu lakini wanaumiza kwa kiwango kikubwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawa wana imani kubwa na Serikali yao ya Chama Cha Mapinduzi, wana imani kubwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa hiyo ni lazima Wizara hii ione namna ya kuwalinda wafugaji huko chini katika kuonewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, katika suala la Uvuvi, tuhakikishe kwamba tuna maziwa mengi makubwa, lakini hata yale maziwa madogo madogo tuweze kuleta samaki na nchi hii karibu kila Wilaya ina bwawa, ina ziwa, ambalo linaweza kuzalisha samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni lazima tuangalie, mifugo yetu, mbegu zetu zinastawi wapi ili ujue Kanda ya Kaskazini utapeleka mbegu gani na Kanda zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima na unyenyekevu mkubwa ninaunga mkono hoja, lakini Wizara hii ni lazima Wizara ya Fedha iongezee bajeti ili iweze kutufikisha katika Dira ya Mwaka 2050. Ahsante sana. (Makofi)