Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Monduli
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ISACK J. COPRIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua nafasi hii kushukuru sana kwa kupata nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Mifugo. Nina-declare interest, mimi ni mfugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Waziri, tunaona ni jinsi gani kila anapotua kuna jambo linaonekana kwamba, Mheshimiwa Bashiru amefika hapo. Kwa kuwa, dakika sita ni chache, ninaomba nijielekeze moja kwa moja kwenye mambo yafuatayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaiomba Wizara hii, kumekuwa kukizungumzwa sana mambo ya migongano kati ya wakulima na wafugaji, halafu tunapata muda mchache wa kujadili jambo hili. Ninasema tu kwamba, jambo hili la wakulima na wafugaji ni jambo ambalo limejadiliwa Bungeni kwa muda mrefu, sasa solution ni kutafuta nafasi ya Waheshimiwa Wabunge kuzungumza namna bora ya kutatua changamoto hii kati ya wakulima na wafugaji, ili isiendelee kuwa ni jambo ambalo linajadiliwa Bungeni kila mara. Hilo litakuwa ni jambo zuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais ya Tarehe 14/11/2025, alisema maneno mazuri ambayo ninatamani sana Mheshimiwa Waziri atembee kwenye eneo hilo. Alisema ataongeza maeneo ya malisho kutoka 3,000,000 mpaka 6,000,000. Sasa ikoje? Iko hivi, lazima tuyaainishe haya maeneo ambayo tunafikiri tunatamani sana yawe ni maeneo ya malisho. Je, ni kwenye vijiji tunakwenda kutathmini maeneo tuliyonayo? Je, ni kuongeza kwenye maeneo ya ranchi? Je, ni kupunguza kwenye maeneo hata ya hifadhi zetu? Je, tunakwenda wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatamani sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up Wizara yake atuambie mikakati gani wanayo ya kwenda kutafsiri Hotuba ya Mheshimiwa Rais ya kuleta matumaini makubwa au tabasamu kwa Watanzania, hususani wafugaji. Ninaomba sana kwa sababu, hivi tunavyozungumza ranchi zetu nazo sasa hivi zimekuwa kama ni taasisi, hata wakikamata ng'ombe, wanapiga faini kubwa. Hivi kuna maeneo sasa hivi tunavyozungumza, na ninaomba Mheshimiwa Waziri aliangalie hilo jambo; kuna wananchi huko Morogoro ng'ombe wameshikwa zaidi ya siku mbili, wamefungiwa ndani mpaka sasa hivi. Ni vyema wakaona jinsi ya kuwasaidia wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajielekeza zaidi jinsi ya kufanya kupata malisho. Mfano, tutengeneze taasisi na taasisi, tuna maeneo mengi ambayo tunaweza kuvuna majani, hata kwenye hifadhi zetu kuliko kuchoma tuvune majani, tuweke kwa kanda, tuwauzie wafugaji. Punde wanapopata matatizo haya wanakwenda kununua kwenye Taasisi kama NFRA, sasa hivi ina chakula kwenye kanda zote. Lazima watengeneze nafasi ya kuvuna majani kwa kipindi hiki tumepata mvua za kutosha, wangetengeneza maeneo ya kuvuna majani, ili kuwauzia wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ni lazima tuhakikishe tunajenga mabwawa. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, kaka yangu, tunalo bwawa kule Monduli Juu lililojengwa na Hayati Edward Moringe Sokoine miaka ya 1980, limedumu mpaka mwaka 2005. Sasa limekufa lile bwawa na ndiyo lililokuwa linabeba zaidi ya vijiji 30 kwenye Wilaya ya Munduli. Ninamwomba na ninatamani kusikia kama bwawa hilo na lenyewe lipo kwenye mikakati ya kulifufua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima Wizara sasa ije na mpango kazi na tafiti juu ya kuwapa wafugaji elimu ya kufuga mifugo yenye faida kwa sababu, tukiwa na mifugo mingi ambayo haina faida, haina maana. Kwa hiyo, ninaiomba Wizara ijipambanue vizuri kutengeneza nafasi na kutoa wataalam wazuri wa kwenda kutoa elimu juu ya ufugaji bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti; ili waeleweke kabisa, siyo kila mahali mifugo inaweza ikastawi. Kuna mifugo kwenye Kanda ya Kaskazini inaweza ikakubali, kama bohemia, kuna mahali pengine hawakubali. Lazima tafiti zifanyike kuhakikisha kwamba, wananchi wanapewa elimu, ili wawe na elimu nzuri ya kufuga mifugo michache yenye tija tuondokane na kufuga mifugo mingi isiyokuwa na tija. Lazima Mheshimiwa Waziri ajipange vizuri kutengeneza wataalam ambao watakwenda kuhakikisha wanatufanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, chanjo. Wanajua fika na Mheshimiwa Waziri nilipata muda wa kuzungumza naye, lazima tuwe tunawa-promote wawekezaji wanaotengeneza chanjo nchini, ili waweze kuzisambaza na kuhakikisha kwamba, wanazuia za nje zisiingie, ili za nchini zifanye vizuri na wananchi wetu waendelee kupata kipato. Ni lazima wasimame kwenye hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo ni lazima wajenge majosho. Wanajua kabisa kwamba, majosho nchini ni uhitaji mkubwa wa wafugaji, watengeneze majosho ya kutosha. Sijui kama kwenye hotuba yake ameyataja, lakini ninatamani sana Mheshimiwa Waziri majosho mengi yajengwe. Ranchi hizi za Taifa ni vyema, kama wenzangu walivyosema, kama tunataka kubinafsisha na kuwapa wawekezaji tuangalie percentage, lakini tusimpe mtu li-ranch lote akalihodhi mwenyewe pale, ndipo Watanzania wa kawaida wanawakamata wanawatesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima wafanye research kwenye ranch zetu tulizonazo. Je, zote zinafanya vizuri? Au zimekaa tu zime-hang? Nyingine zimekuwa mapori, zimekuwa misitu; je, tuna mikakati gani, kama Wizara, kwenda kusimama na kutengeneza ranch zile na kuzifufua, ili kuhakikisha tunakwenda vizuri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Mheshimiwa Waziri, ni lazima huu mgongano uliopo na ninashukuru kwa sababu Mheshimiwa Waziri Mkuu anapopita anasema sisi wafugaji ni ndugu…
MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wako umekwisha.
MHE. ISACK J. COPRIANO: ... na wakulima kwa hiyo, ninaomba sana tuweke mikakati mizuri ya kutatua hizi changamoto, ili wananchi wetu waweze kuwa na ufugaji bora na sio ufugaji wa kuhamahama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana na ninaunga hoja mkono. (Makofi)