Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nichangie kwenye sekta hii muhimu ya uvuvi, ingawa mimi siyo mvuvi wala siyo mfugaji sana, lakini nimeshawishika sana kuchangia sekta hii kwa sababu ya mambo makubwa ambayo nimeona yamefanyika.


Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taarifa niliyokuwa ninaisoma ya kaka yangu, Mheshimiwa Dkt. Bashiru, nimeona mafanikio makubwa kwenye sekta hii ya uvuvi. Hivyo, tumpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kukuza sekta zote nchini bila kuchagua, ikiwa ni pamoja na hii ya uvuvi na mifugo. Tumeona, hapa inaonesha kazi kubwa zilizofanywa; kwa mfano, nilikuwa Mjumbe wa Kamati hii mwanzoni na tulikuwa tunazungumza habari ya kuwa na meli ya uvuvi. Hapa leo nimeona katika taarifa kaka yangu, Mheshimiwa Bashiru amesoma kwamba, sasa meli ya uvuvi imekwishanunuliwa kwa njia ya ubia. Sisi tunaendelea kupongeza mpango huo wa ubia kati ya Serikali na sekta binafsi uendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona hapo bandari ya uvuvi pia, tumeizungumza, Kilwa Masoko na imefikia 97%. Yote haya ni mafanikio, lakini tukiangalia kwenye upande wa uzalishaji wa mazao ya uvuvi karibu tani 659,000 zimepatikana, ambayo ni ongezeko kama la 10%, lakini pia jumla ya maboti 219 pamoja na vizimba 509 vimetolewa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo yote ni mafanikio katika sekta ya uvuvi. Programu ya mafunzo kwa vitendo, kupitia programu za BBT, ambapo zaidi ya shilingi 30,000,000,000 zinaendelea kutolewa kwa vijana kuhakikisha kwamba, tunaongeza ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mifugo wakati tumeanza ilikuwa ni kelele, lakini ninafahamu tu ma-curtail walioko humu, wanasiasa pamoja na watu wa Serikali walileta shida. Waligoma ile chanzo cha kuweka hereni, lakini nikachangia, mnakumbuka, nikasema jamani wanasiasa waiache Serikali ifanye kazi maana wakati mwingine mambo huwa yanakwama kwa sababu, sisi tunahusika, kwa hiyo, tuipe nafasi Serikali ifanye kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana ndugu yangu, Mheshimiwa Bashiru, ninamjua amekuwa mjumbe wangu, kama Mwenyekiti wa Kamati ya Maji na Mazingira. Mjumbe mwaminifu aliyenitumikia mimi, kama Mwenyekiti, kwa uaminifu sana. Nilivyosikia amepewa Uwaziri wa Uvuvi nilifurahi sana na ninamfahamu pia, Katibu Agnes Meena, ni watu wazalendo. Sasa ndugu yangu Bashiru umeingia mahali pana wahuni wengi na mahali pagumu, tukiwemo sisi wanasiasa na wafanyabiashara wengine walioko Serikalini. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua sasa mijadala mingi inaendelea hapa kufunga au kutokufunga mabwawa na maziwa. Ninamshauri Waziri kwa uaminifu kabisa, mimi kama mzalendo kwamba, kutakuwa na manung’uniko mengi, lakini aongozwe na sayansi, aongozwe na utafiti, huo ndiyo msingi wake. Maana kila mtu atalalamika, hata mimi ninaweza kuja kulalamika kwa lolote, wewe kwa sababu, huwezi kumdhulumu mtu, ninamjua uzalendo wake, hawezi kumwonea mtu, ahakikishe anaongozwa na sayansi…

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. JACKSON G. KISWAGA: ...na aongozwe na utafiti, hakuna lingine. Yaani hakuna lingine...

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jackson Kiswaga, kuna Taarifa.

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mchangiaji anachangiaje vizuri?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Getere kwanza sijakuruhusu.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: aah!

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kiswaga, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Boniphace Getere.

TAARIFA

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mchangaji anachangiaje vizuri, lakini ninaomba tu kwamba na yeye ana mamlaka makubwa sana hapa Bungeni, kusema hii Wizara ina wahuni wengi na wanaochangia ni wahuni! Ninaomba afute hiyo kauli, siyo nzuri sana kwa mamlaka yake.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Getere hiyo ni Taarifa au?

Kwa sababu, kwa mujibu wa kanuni na hicho ambacho unakisema, hiyo haiwezi kuwa Taarifa, unless ulete kwa utaratibu mwingine. Kama nimemsikia Mheshimiwa hakumaanisha hicho.

Tuendelee, Mheshimiwa Kiswaga.

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninaamini kaka yangu alikuwa amesinzia kidogo, ninajua huu ni mchana. (Makofi/Kicheko)

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Sasa mambo ambayo ninataka kushauri, kwanza tuhakikishe…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti.

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Wewe usinipotezee muda. Tuhakikishe mamlaka... (Kicheko)

MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, niliomba Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jackson Kiswaga, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kangi Lugola.

TAARIFA

MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Jackson Kiswaga anaanza kuchangia alijipambanua kwamba, yeye hatoki kwenye ziwa lolote hapa nchini. Ninaomba nimpe Taarifa kwamba, kuna msemo au methali inayosema, uchungu wa mwana aujuaye mzazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona nimpe hiyo Taarifa kwamba, sisi tulioko kwenye maziwa ndiyo tunajua matatizo tunayoyapata, kama maziwa yatafungwa. Nimeona nimpe Taarifa hiyo. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jackson Kiswaga.

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ngoja nipokee Taarifa tu. Ni kweli sitoki huko, lakini ninazo taarifa nyingi zinazohusu mambo ya uvuvi na mifugo, kwa hiyo, nimeipokea Taarifa kwa namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaloomba kushauri, nikiwa Mjumbe wa Kamati ya Uvuvi, Mifugo, Kilimo na Maji tulishauri mamlaka ianzishwe, ili kusaidia kuisimamia sekta ya uvuvi ambayo ina wadau wapatao kama 6,000,000 ambao wanahusika na hii sekta. Kwa hiyo, ni muhimu kuwa na chombo ambacho kinaweza kuwasaidia kudhibiti kwa sababu, tunataka tuwe na uvuvi endelevu, uvuvi utakaoishi. Hatutaki uvuvi utakaokwisha leo, tunataka vizazi vya sasa na vya baadaye viendelee. Ndiyo maana suala la udhibiti halina mbadala wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwenye mipango ya matumizi bora ya ardhi ni muhimu sana kuendelea kufanya hivyo kwa sababu, migogoro kati ya wafugaji na wakulima imeendelea kuwa mingi kwa hiyo, suala la matumizi bora ya ardhi, Serikali iendelee kujipanga polepole. Ni nchi yetu, wavuvi wanazidi kuongezeka, wafugaji wanazidi kuongezeka, kwa hiyo, tuendelee kuona namna gani tunagawanya maeneo vizuri, ili tuweze kuimaliza migogoro, lakini ninaona ndiyo namna bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninaomba washirikiane sana na sekta ya maji kwa sababu, sekta ya maji tulianza, ninamalizia tu hii kwa sababu, tulianza ule mpango kabambe wa matumizi ya maji, ambapo ndani yake tumesema kuwe na maji, kwa ajili ya wanyama, binadamu na kilimo. Washirikiane vizuri, ili watu wa mifugo wapate mabwawa kutoka kwenye sekta ya maji, wakishirikiana mambo yatakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia, yako mengi tutayaandika. Ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)