Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Kangi Alphaxard Lugola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwibara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze na mtu anaitwa ratiba. Huyu ratiba huyu, hivi kweli Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kupangiwa siku moja, Mbunge kuongea dakika sita, wakati ng'ombe duniani, Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 ambazo zinahusika na ng'ombe. Katika Afrika, Tanzania ni ya pili nyuma ya Ethiopia, tuna ng'ombe milioni 39. Ratiba huyu basi tu. Ninampongeza Mheshimiwa Waziri anafanya kazi sana, Wizara imechangamka. Kwenye hotuba yake amezungumzia suala la BBT, lakini akaja na ile kauli mbiu ile ya kujenga kesho iliyo bora na hasa kwa kupitia ufugaji wa samaki kwa vizimba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nijikite kwenye vizimba kwa sababu ya muda. Tulilenga kwamba tukifuga kwa vizimba, kwanza tutaongeza ajira, lakini pia tutaongeza pato la Taifa kupitia uvuvi. Pia, tutapambana na umaskini ambao umekithiri miongoni mwa watu wa chini, hasa kwenye Ziwa Victoria ambako mimi ninatoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nichangie kwa kumuuliza Mheshimiwa Waziri, sijui kama anazijua changamoto au matishio dhidi ya ufugaji wa samaki kwa vizimba katika Ziwa Victoria? Ninaomba Mheshimiwa Waziri anisikilize kwa makini. Sasa hivi kuna matishio makubwa yameanza kule Ziwa Victoria, hususan kwenye ufugaji wa samaki kwa vizimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji wazawa sasa hivi hawako kwenye ushindani ulio sawa, kwa sababu wawekezaji wa kigeni wamekwishatamalaki kwenye Ziwa Victoria. Wengine wamepewa mialo kilometa zaidi ya tano, wakiwemo Wachina na Wazambia. Sasa Waziri akumbuke kule kwao China, kwa mfano wakichukua mikopo, wanachukua kwenye benki kwa asilimia mbili lakini wazawa sisi hapa wakienda kwenye benki ili wawekeze kwenye vizimba, watapigwa mikopo kuanzia asilimia nane mpaka 24%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hawa wawekezaji wa kigeni watakuwa ma-giant, watakuwa na uwezo wa kuzalisha samaki kwa wingi, watatawala masoko na teknolojia. Kwa hiyo, kwa vyovyote vile, wafugaji wazawa watatelekeza vizimba, kwa sababu hata uwezo wa kushindana hawatakuwa nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri, ajaribu kuhakikisha kwenye mazingira kama haya hawa wafugaji wa vizimba wa kigeni waweze kupata leseni ambazo zina mazingira tofauti. Kwa sababu nimejaribu kufuatilia, mazingira ambayo yanaondoa kabisa ushindani ulio sawa, leseni zao na za wazawa hazina utofauti. Sasa tishio hili Waziri asipolifanyia kazi wafugaji wazawa watatoweka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kumeanza pia, kuwa na wawekezaji wa mitaji ya briefcase. Wanatoka kule hawana hela, wanakuja humu wanazungukazunguka, wanapata mikopo kwenye benki halafu wanaenda kuwekeza kwenye vizimba. Ninamwomba Waziri ajaribu kuhakikisha kwenye eneo la samaki ahakikishe kwamba, zile inputs zote ambazo ni sehemu ya mtaji waweze kuwalinda wazawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inakuwaje tunakuwa na sera za kulinda viwanda vyetu vya ndani, halafu tushindwe kuwalinda wafugaji wa vizimba ambao ni wazawa, ili kweli waweze kujenga kesho iliyo bora! Hivi kweli, Tyson unaweza ukampambanisha na Kiduku au Mwakinyo? Si ni kumuua tu yule!

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakwenda kwenye suala la uvuvi haramu pale Ziwa Victoria, maeneo ya Jimbo la Mwibara. Mheshimiwa Waziri hii sasa hapana, kuna wavuvi hao wamekuja na teknolojia, ninadhani unaifahamu au umeisikia, inaitwa manyamu au machoteni. Wanatoka Wilaya ya Busega wanasogea pale Sozia mpaka Kisoria, wana marungu, wana mapanga, wana mawe, wanakatakata nyavu za wavuvi wengine, halafu wanavua kiharamu kwa kutumia hayo manyamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maafisa Uvuvi wapo wanawaona na hata wakienda kufanya doria wanawafanya kama mtaji sasa wa kujipatia fedha. Pambana na uvuvi haramu. Nimesikia hapa kwamba, kuna utaratibu wa kufunga Ziwa Tanganyika. Sisi ambao tuko kwenye Ziwa Victoria ni kweli kwenye dagaa tumejaribu, kuna kitu kinaitwa mtegeruko, watu wanategeruka wanaacha ziwa linapumua halafu wanapata dagaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo wakifunga Ziwa Tanganyika kwa sababu ya huu uvuvi mwingine na wakaona kwamba, kufunga Ziwa Tanganyika hakutoshi! Sisi Ziwa Victoria tuna wasiwasi kwa sababu, tunajua sasa sisi ndiyo tunafuata. Ninaomba Serikali isije ikajaribu kufanya kitu kama hicho, waimarishe doria. Doria ndizo zitanusuru haya maziwa. Wakifunga maziwa haya na watu wengine wana mikopo, Wasifikiri tu hawa vijana tuliowakopesha ndiyo wana mikopo, kuna wafanyabiashara ambao pia wana mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)