Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia Bajeti ya Wizara ya Mifugo. Kwanza ninampongeza sana mtendaji wa Wizara hii, kwa kasi aliyoanza nayo, sisi tunaendelea kumwombea. Aendelee kupambana, mtu mzalendo, mjamaa, anayefikika na ambaye amekubali kuwasogelea wavuvi na wafugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa kwanza ni juu ya Bajeti ya Wizara hii. Fedha zinazotengwa na zinazotolewa. Hii ni Wizara nyeti kabisa kwa Watanzania, ni nyeti kwa sababu ni Wizara inayohusu usalama wa chakula katika nchi yetu, lakini ni Wizara tunayoitegemea kwa lishe. Tunajua tuna changamoto nyingi sana za lishe katika nchi yetu. Kuna utapiamlo, kuna udumavu, zaidi ya 30% ya watoto wetu wana udumavu na wao ndiyo Taifa la kesho, kwamba tuseme Watanzania watakuwa na udumavu. Sehemu pekee ambayo viini lishe muhimu kwa binadamu, kwa ajili ya lishe, tunavipata katika vyanzo vya mifugo kuliko ukilinganisha hata kwenye vyanzo vya mimea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana utaona takwimu za kitaifa za FAO au WHO, sisi ulaji wetu wa vyakula hivi huko chini, kama ni nyama wenyewe recommended ni kama kilo 25 kwa mwaka, sisi bado tuko 15; tunatakiwa tule mayai 300 kwa mwaka kwa mtu, lakini sisi bado tunakula 106. Maziwa tunatakiwa tunywe zaidi ya lita 200, sisi bado tuko kwenye lita 62, ni kwa sababu upatikanaji ni mdogo. Upatikanaji ni mdogo kama tusipoendelea kuwekeza katika sekta hii, ina maana matokeo yake ni mabaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii iliyopita, fedha za maendeleo ilitengwa shilingi bilioni 375.138, lakini hadi Februari fedha zilizotolewa ilikuwa ni shilingi bilioni 110.942. Ina maana bajeti ilitekelezwa kwa 29% au 30%, hebu ona sasa ilivyo hatari. Niiombe Serikali iko hapa, hata kama fedha hizi zimevuka mwaka, hawa watu wapewe fedha wakatekeleze miradi muhimu kwa ajili ya maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia fedha ambayo Waziri ameomba mwaka huu, ukienda kwenye bajeti ya maendeleo, bado fedha zimepungua. Bajeti inayoendelea kutekelezwa ndiyo hii ya shilingi bilioni 375.138, sasa hivi ameomba shilingi bilioni 335.099, imepungua kwa karibu 10% na pointi. Tunaomba hata kwenye majumuisho ya mwisho, itakavyosomwa bajeti ya nchi hii, hii Wizara nyeti iweze kuongezewa fedha ikiwezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine ni kwenye nyanda za mifugo. Sisi tumebarikiwa, tuna rasilimali ya ardhi zaidi ya hekta 94,000,000, ambapo 50,000,000 zingefaa kwa nyanda za mifugo, hiyo 44,000,000 ndiyo ingekuwa ya kilimo. Ijapokuwa kinachotumika ni shilingi milioni 9.3 kwenye malisho ya mifugo, sisi tumeweza kupima kiasi cha hekta milioni 3,489,701, lakini bado ni maeneo ambayo kila mtu anaona ni maeneo wazi, yasiyomilikiwa na mtu, yasiyo na sheria, kwa hiyo, kila mtu anavamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatari yake ndiyo hii kuhangaika na mifugo, wanazunguka Tanzania nzima hata nje ya Tanzania wakitafuta malisho. Tufike mahali sasa, nyanda za malisho zipimwe, zipewe sheria ili kusaidia mifugo hii isihangaike ikawa na afya bora, lakini ikawa inasambaza magonjwa na mambo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, ni suala la maji kwa mifugo, ndiyo inayofanya mifugo izurure kote nchini. Kwenye mifugo tunataka malambo madogo madogo, yanaitwa charco dams. Hizi charco dams zinawezekana kwenye kila kitongoji cha wafugaji. Kama Wizara ya Maji imeweza kununua mitambo yao wenyewe ya kuchimba maji na visima. Tunaomba basi, hata Wizara ya Mifugo iwe na mitambo yake iwe na ma-excavator, ili katika maeneo madogo madogo, hata wafugaji watakuwa tayari kuchangia mafuta, iweze kuwachimbia malambo haya madogo madogo kwenye maeneo yote ya wafugaji, kusaidia mifugo hii isizurure na ikawa na afya njema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine ni kwenye suala la chanjo na utambuzi wa mifugo. Ninaipongeza Serikali, imezindua hii chanjo, mifugo imechanjwa na bado utambuzi wa hereni unaendelea kuwepo. Hii imetusaidia sana, angalau mifugo sasa hivi masoko yanafunguka, kama hivi sasa hivi tumeshaanza kupata soko la Uarabuni. Ninaomba mpango huu, ni kweli tumeanza kuchanja magonjwa kama CCPP (Homa ya Mapafu), lakini bado tuna magonjwa mengi. Tuna foot and mouth disease, tuna anthrax, tuna magonjwa mengine. Tunaomba tuwe na kalenda ipelekwe kule halmashauri, watumishi wa halmashauri ndiyo waendelee kuchanja mifugo, kila siku sehemu ya uchanjaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona umeniwashia, kwa hiyo ninashukuru na ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)