Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kiteto
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi na kwa sababu ya muda nimpongeze Waziri, Mheshimiwa Balozi Dkt. Bashiru, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu nzima ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kazi ambayo wanajaribu kufanya. Mheshimiwa Balozi Dkt. Bashiru, sisi tuna imani kubwa sana na wewe. Unajua Katibu Mkuu wa CCM Mstaafu, Balozi, Profesa chuo kikuu huko, maana yake ni mtu ambaye anaifahamu hii nchi sana. Matamanio yetu ni utujengee misingi hiyo ya ujamaa; hii nchi ni ya ujamaa, Watanzania ni wajamaa, ni lazima tuendeshe Wizara hii kijamaa jamaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na bajeti kuongezeka, lakini sisi bado tunaona bado tungetamani sana Wizara hii ipate bajeti, kwa sababu mahitaji ya Watanzania ni mengi sana. Mabwawa, majosho na maeneo ya malisho, hiyo yote inataka pesa. Kwa hiyo, tungetamani na wito wetu kwa Serikali iendelee kuongeza pesa nyingi sana. Hata kwenye uvuvi huko, mahitaji ya Watanzania kwa masuala ya uvuvi ni mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kweli kwa nchi ya kijamaa, tungetamani sana kuona bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi iwe kubwa sana. Mheshimiwa Dkt. Bashiru, tuna imani kwamba, huko mbele utajenga hoja vizuri, ieleweke zaidi ili Wizara hii iendelee kupatiwa bajeti kubwa zaidi, kwa sababu mahitaji ya Watanzania ni mengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Kiteto lina ng'ombe zaidi ya 500,000 na mahitaji ya majosho leo, kwa sababu Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inasema kila kijiji chenye ng'ombe, inastahili kuwa na josho. Tunahitaji majosho zaidi ya 40, pamoja na kazi kubwa iliyofanyika, mabwawa zaidi ya 45, Mabwawa kama ya Dosidosi, Ndedo, Bwawani, Sunya na Kijungu. Kwa sababu, tunazungumza habari ya dira inayotaka kuwapeleka Watanzania miaka 25 ijayo, ya kuongeza kipato kwa Watanzania, hatutaweza kufika huko kama pesa hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji wasipopata maeneo ya kutosha ya malisho, tukapata maji ya kutosha kwenye mabwawa, lakini mifugo ikapata dawa kwa wepesi na kwa wakati, tukapata na majosho, huko hatutaweza kufika. Kwa hiyo ni lazima, formula pekee hapa ni kuwa na pesa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri kwa kweli tunatamani sana Serikali iibebe sekta hii vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti iliyopita kwa sababu Kiteto ina minada mikubwa sana na mapato yanayotokana na mifugo tunapata kupitia minada. Mnada wa Dosidosi, Kibaya na Sunya, sisi tulishaahidiwa hapa kwamba tungepata pesa kwa ajili ya kuboresha minada. Kwa hiyo, matamanio ya Wanakiteto ni kuendelea kuwaambia Serikali watuletee pesa hizi kwa ajili ya minada hii mikubwa, lakini watupatie pesa kwa ajili ya mabwawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bwawa la Ndido, Wizara ilishapeleka karibu 200,000,000, na ni bwawa la 500,000,000. Sasa kwa sababu nimemsikia mara kadhaa akisema, miradi ambayo tumeshaanza tumalize, hebu alichukue hili la Ndido sasa tumalize, halafu tupambane na haya mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitamani sana tujenge mazingira mazuri kwa ajili ya wafugaji. Ninadhani, maeneo haya ya Serikali, ya NARCO na Ranchi za Taifa, nchi ya kijamaa kama hii, ningetamani sera yetu iwe maeneo haya tuwape wafugaji wadogo kwa 60% na 40% watumie kwa ajili ya wafanyabiashara wakubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ya kijamaa lazima ionekane kwenye percent kwamba focus yake iko wapi. Kwa hiyo, tuangalie pamoja na kwamba wanapitia hizo, lakini 60% ya Ranchi za Taifa ziende kwa wafugaji wadogo, ziende kwa vijana, kwa sababu tunataka vijana wetu wapate ajira. Kwa hiyo, tungetamani sana kuwe na maelekezo maalum kwamba, ranchi zetu tuelekeze nguvu huko. Mheshimiwa Waziri, mambo ya jumla mengine, nimezungumza sana habari ya wakulima na wafugaji, vurugu hizi. Nchi ya kijamaa, kwa kweli lazima tujenge misingi na Mheshimiwa Rais tumpongeze hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, alizungumza Mbunge wa Morogoro hapa, ile Programu ya Tutunzane, ambayo Mheshimiwa Rais ameshaonesha nia. Sisi kazi yetu ni kuendelea kuboresha zaidi, ili tujenge mahusiano ya wakulima na wafugaji. Nchi hii hakuna kijiji hata kimoja, utakuta kina wakulima peke yake ama wafugaji peke yake. Dawa ya hii ni kutengeneza pesa, mipango bora ya ardhi tutenge; anayefuga ajue anafuga wapi, anayelima ajue analima wapi. Hili wazee na viongozi, tuzungumze lugha hapa bila kuonesha kugawa hawa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hii ndiyo kengele ya mwisho, basi ninaunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)