Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Kiza Hussein Mayeye

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nianze na kumshukuru Mungu kwa kunipa kibali kilichoniwezesha kusimama siku ya leo katika kuchangia bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninatambua kazi ambayo Mheshimiwa Waziri, baba yangu Mheshimiwa Kakurwa anaifanya, hongera kwa kazi ambayo anafanya kwa ajili ya Watanzania. Sitakuwa na mengi kwa sababu wenzangu wa Ziwa Tanganyika wamezungumza mengi, lakini ninataka kukazia katika suala la kufunga Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezaliwa Kigoma, nimekulia Kigoma; asilimia kubwa ya watu wa Kigoma wanategemea Ziwa Tanganyika hasa katika Jimbo la Kigoma Kaskazini, kwangu, lakini na Jimbo la Kigoma Mjini kwa kaka yangu Revocatus.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la samaki kuongezeka na kupungua katika Ziwa Tanganyika liko automatic toka tunakua, enzi za mababu na mabibi. Kuna wakati samaki wenyewe ziwa linajifunga, linajifungua, samaki wanakuwa wengi, samaki wanakuwa wachache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, mkakati wa kufunga ziwa kwa Wanakigoma ama Ziwa Tanganyika kwa ujumla, sisi kama wananchi hatukubaliani nalo. Kiukweli tunaona kabisa ni kama hawataki kutusikiliza wananchi. Nimwombe Mheshimiwa Waziri atenge muda akazungumze na wananchi, yawezekana akaletewa ripoti kutoka kwa watu wake wa chini, wakamwambia tumefunga ziwa, tulivyofungua samaki walikuwa wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nimhakikishie Mheshimiwa Waziri, kama kuna kipindi watu wa Kigoma walikula sana dagaa wa Mwanza, ni wakati tumefunga Ziwa Tanganyika na likafunguliwa, lakini watu walikosa mboga zilikuwa hazipatikani. Wananchi wa Kigoma hali zetu tunazijua, tukifunga ziwa kuna watu nyama hawaioni ndani ya mwezi au Eid mpaka Eid ndiyo wanakula nyama. Maana yake, tunapowafungia ziwa watu wanakosa mboga, lakini siyo kukosa mboga tu; kwa mfano, Kigoma Kaskazini, wengi wanategemea uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lile ndiyo duka lao, waingie ziwani wakavue, wapate pesa, wasomeshe watoto. Unapomfungia mtu ziwa miezi mitatu tafsiri yake ni kwamba, unamrudisha mtaani akakae bila kazi. Kipindi tumefungiwa ziwa ni kipindi ambacho hata wizi uliongezeka. Watu walikuwa wananyang’anywa mizigo pale Kigoma, wizi ulikuwa mkubwa kwa sababu watu walikosa kazi za kufanya. Kwa hiyo, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri busara iwaongoze watu wa Wizara ya Uvuvi. Wawasikilize wananchi, tukae tutafute namna gani ya kuweza kusaidia samaki zisipotee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamesema Waheshimiwa na iko wazi samaki wanapotea kwa sababu ya uvuvi haramu. Watu wanatumia nyavu haramu, lakini hizi nyavu zinaingizwa kutoka nje, zinauzwa. Wavuvi wanakwenda wanazinunua madukani, maana yake wanalipa kodi pia kwa Serikali. Sasa kama Serikali inachukua pesa, watu wananunua nyavu, lakini nyavu hizohizo zikifika kwa mvuvi Ziwa Tanganyika zinaitwa nyavu haramu, hatuwatendei haki wavuvi. Kama ni nyavu haramu, Serikali izuie kuingiza nyavu hizi, ili hawa wananchi wanyonge wasiweze kuzipata hizo nyavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ninataka nizungumze, ni suala zima la leseni kwa wavuvi. Leo ukikata leseni ya gari kama umekata tarehe 14 ya mwezi Mei, maana yake itakwenda kwisha ndani ya mwaka mmoja, tarehe 14 ya mwezi Mei, 2027, lakini wavuvi leo akikata leseni tarehe 14 mwezi Mei, 2026, ikifika Disemba leseni yake ime-expire. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ninaomba u-take note hii, wasaidieni wavuvi, wakate leseni kwa mwaka. Akikata mwezi Mei, mwaka huu, arudie mwezi Mei mwakani na siyo ikifika Disemba akate tena. Hali ya maisha kwa Watanzania ni ngumu, watu hawana pesa kwenye mifuko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nizungumzie suala la vizimba. Wenzangu wamesema, ni kweli ukitazama vizimba vilivyopo katika Ziwa Tanganyika, huwezi kulinganisha na idadi ya vizimba katika Ziwa Victoria. Tunataka Ziwa Tanganyika na sisi tuongezewe vizimba, viwe vya kutosha na visiwe kwa watu wachache ama watu specific. Tuwachukue hata wale wavuvi wadogo wadogo na wao waweze kupewa vizimba, waweze kumiliki vizimba na tuweze kupata samaki kwa wingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, ninataka kuzungumza, ndani ya Ziwa Tanganyika kumekuwa na matukio ya wavuvi kuibiwa mashine, wavuvi kupigwa na majambazi kuwateka. Tunaomba tuwe na ulinzi wa kutosha katika Ziwa Tanganyika, kuwasaidia wavuvi wasiweze kuibiwa mali zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mikopo kwa wavuvi. Ni kweli tunashukuru Serikali, inatoa mikopo kwa wavuvi, lakini bado si wavuvi wote. Tunaomba Mheshimiwa Waziri, wavuvi hawa hata wale wadogo kabisa waweze kuaminiwa, waweze kupata mikopo, waweze kufanya kazi zao vizuri bila changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua unataka kuniambia muda…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ndiyo muda wako umekwisha.

MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba dakika moja. Ninataka nigusie suala zima la migogoro ya ardhi, kwa maana ya wafugaji na wakulima. Hili tulichukulie very serious. Ukifika huko kwenye majimbo yetu vijijini, wakulima na wafugaji wanakatana mapanga, wanauana, hali ya kuwa sote ni Watanzania. Tutafute namna ya kuondoa hii changamoto. Ahsante. (Makofi)