Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tanganyika
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu. Kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na kumpongeza kwa kazi nzuri ambayo anaifanya hasa ile ya operation kwenye eneo la Ziwa Tanganyika. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri juhudi ambazo amezianzisha zisiwe za zimamoto. Twende moja kwa moja kudhibiti uvuvi haramu ambao unachangia sana kuua Sekta ya Uvuvi hasa kwenye eneo la Ziwa Tanganyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ni miongoni mwa watu ambao siafikiani na mpango wa Serikali wa kulifunga Ziwa Tanganyika. Ninafahamu chanzo cha Ziwa Tanganyika kufungwa ni sababu ya uvuvi haramu ambao upo kwenye eneo la Ziwa Tanganyika. Nyavu zinazoletwa kutoka nje ya nchi zimekuwa ni tishio kwa mazalia ya samaki na viumbe hai ndani ya Ziwa Tanganyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mchangiaji aliyepita alivyosema, zile nyavu ikikatika inaendelea kuua kizazi hadi kizazi kwa kipindi kirefu sana na matokeo yake asilimia kubwa ya uvuvi ndani ya Ziwa Tanganyika unaenda kutoweka. Ili kudhibiti suala hilo ni lazima sasa Serikali ijielekeze kufanya doria ambazo zitasaidia kuondoa kabisa tatizo la uvuvi haramu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaofanya uvuvi haramu ni jirani zetu, wavuvi kutoka Nchi za Burundi na DRC (Congo) ndiyo wanaokuja na hizo nyavu. Lakini bahati mbaya iliyopo hata wale maafisa wetu, Maafisa Samaki ambao wapo kwenye maeneo hayo wanadiriki kushirikiana na hao ambao wanafanya kadhia hiyo mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, lazima tuwe na mpango kazi ikiwa ni pamoja na hao watumishi. Mtumishi wa idara hiyo ya samaki anapokaa kwenye eneo kwa muda mrefu anajenga mazingira ambayo kiukweli yanakuwa na mnyororo mrefu ambao unashirikiana na wavuvi haramu. Kwa hiyo, ninashauri watumishi wawe wanahamishwa mara kwa mara ili kuweza kuondoa hili tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninashauri kwenye maeneo haya, Serikali itenge maeneo ya mazalia ya samaki. Tunao mfano kwenye maeneo yanayomilikiwa na Jeshi (JKT), kwenye maeneo ambayo yapo kwenye Ziwa Tanganyika, mazalia ya samaki yapo na samaki wanapatikana. Kwenye eneo la hifadhi, mfano kule Mahale samaki ni wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tungetenga kila eneo tukawa na mazalia ya samaki, tungetenga hayo kama hifadhi tungekuwa na maeneo makubwa ambayo kwa kuwa Ziwa Tanganyika ni refu, kila eneo tungetenga Mkoa wa Kigoma kuwepo na eneo la mazalia karibu hata vituo vitano, Katavi, Rukwa. Tungesaidia sana kutatua tatizo la uvuvi haramu na kusaidia mazalia ya samaki katika ziwa letu ili kuwe na uvuvi endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la vizimba. Mikoa yetu Mkoa wa Katavi, Rukwa tumepata idadi ndogo sana ya vizimba. Mheshimiwa Waziri niombe sana, tuache kuwa na mpango wa kupeleka vizimba kwenye maeneo ya ziwa moja tu. Ukichukua takwimu Ziwa Victoria ndilo ambalo limepata vizimba vingi. Ninajua Mheshimiwa Waziri hatakuja na mfumo kama ule uliokuwepo huko nyuma, aende akavisambaze vizimba. Kwangu Mkoa wa Katavi eneo pekee ambalo linapakana na ziwa ni jimbo langu. Tunahitaji tupate vizimba na maombi walishaleta, lakini kwa bahati mbaya mpaka sasa hatujakuwa na vizimba vya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mifugo. Kwenye eneo la mifugo Mkoa wa Katavi una idadi ya mifugo mingi sana. Kwa bahati mbaya sana hatuna maeneo ya malisho. Niombe Serikali kwa kushirikiana na halmashauri na halmashauri zishirikiane na Serikali za vijiji, kuhakikisha wanatenga maeneo ya malisho ili kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo ni tatizo kubwa sana katika maeneo hayo. Wakitusaidia hayo, tutakuwa tumeondoa kabisa tatizo la migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini wafugaji wamekuwa wanafanya shughuli ya kufuga mifugo kwa kutangatanga? Ni kwa sababu kwanza hawana malambo, majosho. Sasa ninaomba na kuishauri Serikali hayo maeneo wayasaidie kwa kuchimba majosho na malambo ili tuweze kusaidia jamii ya wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)