Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MORRIS J. MAKOI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi. Ninaomba nianze kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuhakikisha Wizara ya Mifugo na Uvuvi inafanya majukumu yake. Pia nimshukuru Mheshimiwa Waziri wetu, Naibu Waziri na wale wote ambao wanamsaidia katika kutimiza wajibu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma Bajeti ya Mifugo na Uvuvi, ninaona kama imezingatia mambo mengi mazuri. Hata hivyo, nina ushauri, nimeona hapa Wizara wamesema kwamba wataanzisha ng'ombe wa mtambo wa maziwa na ambao watapeleka katika familia 1,600. Sasa sijajua specific kwamba hawa ng'ombe wanapelekwa upande gani. Ninamwomba Waziri, kule Moshi Vijijini tunahitaji ng'ombe hawa sana kutokana na umuhimu wa kubadilisha mbegu ya ng'ombe wa maziwa kule. Kwa hiyo, kama ataweza kutuzingatia walau kwa uchache basi tunamwomba atuzingatie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia elimu hii ya ufugaji ingetolewa kwa vijana, lakini ilenge vijana ambao tunaanzia shuleni. Kwa mfano tukiweza kutoa elimu hii kwa vijana wetu ambao wako kwenye shule za kata na hata msingi kuanzia darasa la sita na la saba ingeweza ikasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa vijana wengi ambao tunawakuta mtaani sasa hivi wanapatikana au wanazalishwa kutoka kwenye shule za msingi na shule za kata. Kwa hiyo, wakiwa na elimu ile mapema inaweza ikasaidia kuwa na uzoefu na wakati wanaporudi baada ya kumaliza shule wanaweza wakaendelea kujiunga au kuendelea na mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri kwenye eneo hilo hilo kuanzishwa kwa ufugaji wa kuku wa kienyeji kwa wale vijana wa vijijini hasa Jimbo la Moshi Vijijini ambako inaonekana kwamba soko la mauzo kwa ajili ya kuku hao ni kubwa na hata mayai. Kwa hiyo, Wizara kama itakuwa na mpango ikileta Moshi Vijijini tuko tayari kupokea na mahitaji ni makubwa. Tunaamini kwamba hawatatumia gharama kubwa sana kwa sababu tumeshaanza elimu kule na utaratibu unaendelea vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia Wizara ya Mifugo kama wanaweza wakaunganisha nguvu na Wizara ya Maliasili kwa ajili ya kusaidia upatikanaji wa mbegu za vipando kwa ajili ya nyasi za kulishia mifugo. Kwa sababu wafugaji wetu ambao wanapatikana katika vijiji 40 vinavyozunguka Mlima wa Kilimanjaro wamekuwa na migogoro na watu wa KINAPA na TANAPA kwa sababu ya kutafuta malisho kwenye maeneo ya jirani na Mlima Kilimanjaro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, magomvi yamekuwa ni mengi kule kwa sababu ya kutafuta malisho. Kwa hiyo, kama Wizara ya Mifugo wakishirikiana na Maliasili wakasambaza mbegu za majani haya ya vipando ya ng'ombe, mbuzi na kadhalika, wananchi wale wanaweza wakazalisha majani na wakalisha mifugo yao na hiyo ikapunguza yale mambo ya kuingilia kwenye mamlaka zile na kupunguza migogoro ambayo haina lazima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utaratibu mwingine ninashauri Wizara ya Mifugo waanzishe Wakala wa Ugani wa Mifugo na Uvuvi. Kwa sababu Wizara ya Kilimo ninaona wameanzisha Wagani na inasemekana kwamba wanaweza wakafanya kazi kwa ukaribu na wananchi na watakuwa wameondokana na ule mnyororo wa Wakurugenzi kuwapa majukumu mengine ambayo yanawafanya wanashindwa kufanya wajibu wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kwa sasa hivi kwa mfano Wagani wa Mifugo na Uvuvi hawapatikani katika maeneo ya vijijini kufanya majukumu yao kikamilifu, kwa sababu muda mrefu wanakuwa wameelekezwa na Wakurugenzi kukusanya maduhuli na hata wakati mwingine kukaimu Utendaji Vijiji kwenye vijiji ambavyo havina watendaji. Matokeo yake ni kwamba wakati wafugaji wanawahitaji hawapati kwa muda. Kwa hiyo, wamekuwa ni bidhaa adimu kule vijijini, kama wakianzisha wakala huenda hawa wakafanya kazi kwa bidii, lakini vilevile watawekeza nguvu zao kwenye jukumu hilo na hivyo kuweza kuleta tija zaidi kuliko hali halisi ilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri pia kuhusiana na vizimba vya samaki. Wizara ya Mifugo na Uvuvi wanaleta miradi ya uvuvi kwenye maeneo, lakini hawashauriani wala kutoa taarifa kwa Wabunge. Kwa hiyo, matokeo yake fedha zinafika kule kwenye halmashauri ama zinafikia kwenye kata au vijiji na Wabunge hawana taarifa. Matokeo yake, ile miradi haipati uangalizi mzuri na hata ile hamasa ya vijana ili waweze kufuatilia na kuelekezwa namna ya kufanya inakuwa kidogo ina changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninamwomba Mheshimiwa Waziri wakati wanaleta miradi ya namna ile Wizara ya Mifugo ijitahidi kuhakikisha kwamba, Waheshimiwa Wabunge wanafahamu ili wahusishe Madiwani na wale watu wa ngazi ya chini ili kuwezesha hilo jambo liweze kuwa na tija ambayo inakusudiwa na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri vilevile, kwamba katika kuhakikisha kwamba mifugo inaimarika ni vizuri sana tukahakikisha kwamba, hawa vijana ambao tulikuwa tunawapa mikopo ya 10% tungeweza tukaelekeza kwenye mbuzi wa maziwa. Mbuzi wa maziwa katika maeneo yetu ya vijijini kama wangekuwa ni sehemu ya mikopo ya 10% ingeweza kuleta matokeo mazuri kuliko zile fedha taslimu wanazopokea. Kwa kuwa zile fedha kila mtu anachukua akitaka kufanya jambo analolifanya ambalo halina uhakika badala yake matatizo yanakuja kuanzia pale kwenye kurudisha ile mkopo, matokeo yake, yale ambayo yamekusudiwa hayaonekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninamshauri Waziri kama itampendeza, basi wajaribu kuelekeza nguvu ile ya mikopo ya 10% ambayo imepelekwa kwenye Wizara ya Mifugo katika ile 200,000,000,000 kwenye ukopeshaji wa mbuzi wa maziwa kwa vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)