Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ludewa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia Bajeti hii ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Awali ya yote, ninapenda kuipongeza sana Serikali na kuishukuru kwa kutoa kiasi cha shilingi 800,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa Soko la Samaki Ludewa ambalo linajengwa pale Kata ya Manda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jumamosi nilikuwa huko, nimeona ujenzi unaendelea vizuri. Nimshukuru pia Waziri, Mheshimiwa Dkt. Bashiru, kwa sababu kuna muda kulikuwa na mkwamo. Tuliweza kuwasiliana naye aliweza kutatua tatizo na sasa ujenzi wa soko unaendelea. Mimi mwenyewe nimeshuhudia nikiwa na Mwenyekiti wa Chama, Mzee Stanley Kolimba na Katibu wa Chama. Kwa hiyo, ninaishukuru sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru pia Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Wizara ya Vijana imeweza kutoa kiasi cha shilingi milioni 520 kwa ajili ya mikopo ya vijana kupitia Benki ya CRDB waweze kufanya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba Ziwa Nyasa. Kwa hiyo, nishukuru sana kwa niaba ya wananchi wa Ludewa, Serikali sasa inakwenda kutengeneza ajira za moja kwa moja kwa vijana zaidi ya 100. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru pia Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya aliweza kufanya ziara. Baada ya mimi kuwasiliana naye aliweza kufanya ziara kata kwa kata kwenda kuunda vikundi hivyo na kusimamia kuhakikisha kwamba jambo hili la Serikali lenye nia njema kwa vijana wa nchi hii linakwenda kutimia. Kwa hiyo, wameshaunda vikundi kwenye kata nne, kwa hiyo sasa Ziwa Nyasa linaenda kuwa na uvuvi wa vizimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nishukuru pia watu wa TAFIRI kwa ushirikiano na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Ludewa ambaye alilipia gharama, Baraza la Madiwani liliidhinisha, Mkurugenzi akalipa, watu wa TAFIRI walikuja kwenda kufanya utafiti maeneo ambayo yanafaa kwa ajili ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba Ludewa. Hii ni kwa sababu kwa muda mrefu Ziwa Nyasa lilikuwa linaaminika kama haiwezekani kwa sababu ya upepo mkali na mawimbi na kina kirefu cha maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, watu hawa waliweza kupata eneo la Uhonjo ambalo lipo Kata ya Iwela na tayari tulishawahi kufanya jaribio la kufuga samaki na matokeo yalikuwa mazuri sana. Baada ya hapo sasa, Baraza la Madiwani wakaidhinisha fedha zile za vikundi ili ziweze kukopeshwa kwa vijana kwa ajili ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niipongeze halmashauri, Baraza la Madiwani kwa kuidhinisha fedha zile. Kwa hiyo, kuna vikundi vitano tayari ninavyozungumza vilipewa mkopo na waliweka tayari vizimba Ziwa Nyasa sehemu ya Uhonjo iliyopo Kata ya Lupingu. Kwa hiyo, haya ni mafanikio makubwa sana kupata kutokea kwenye Ziwa Nyasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unavyozungumzia shilingi milioni 520 maana yake hapo, vizimba zaidi ya 100 vitakwenda kuwekwa kwenye ziwa na vijana zaidi ya 100 pia watakwenda kunufaika na mapato kutokana na mauzo ya samaki. Sasa, hili litapelekea hitaji kubwa sana la vifaranga kwa ajili ya kwenda kuweka kwenye hivyo vizimba zaidi ya 20 ambavyo vinaenda kuanza, ukichanganya na vilivyopo vya halmashauri vitakuwa vingi sana. Kwa hiyo, utafiti tulioufanya kule tuliona watu wa Ruhila walituongoza kwa kushirikiana na Wizara kwamba, vifaranga wanapatikana upande wa wenzetu Malawi ambao wanakubalika kutokana na ikolojia ya Ziwa Nyasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo Kikuu cha Malawi kina kitengo hicho na wanazalisha vifaranga. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri alielekeza wale watu wa Ruhila waweze kuanzisha na hatchery yao. Sisi pia tumetafuta wadau mbalimbali, ambao watakwenda kwa Mheshimiwa Waziri kuomba vibali vya kwenda kuchukua samaki wazazi ili waje waanzishe hatchery Ziwa Nyasa kuzalisha vifaranga wengi zaidi. Hii itaweza kutatua tatizo la upande wa Kyela na upande wa Nyasa. Kwa hiyo, tutaomba hiyo hoja ya vibali kwa ajili ya kwenda kuchukua wazazi na vifaranga wa kuanzia tuweze kupewa ushirikiano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ambayo naiona tukiachana na hii ya vifaranga ambayo tayari angalau tumejua wapi wanapatikana na huwa nina kawaida ya kuwasiliana na watu wa Ruhila kuweza kupata vibali tukachukue kule, ili tusiharibu ikolojia ya Ziwa Nyasa. Kwa hiyo, changamoto inayokuja nyingine ni ya chakula cha samaki (fish feed) wanaita. Kwa hiyo, chakula cha samaki kwa sasa kwa kiwango kikubwa bado tunategemea kuagiza nje ya nchi. Kwa hiyo, kile chakula kinakuwa ni cha gharama sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kutengeneza chakula cha samaki siyo sawa na mtu anayesomea wanaita (rocket science). Ninafikiri tunaweza tukatengeneza wenyewe chakula cha samaki. Kwa hiyo, ninaomba tutatue hii changamoto ya chakula cha samaki ili Ziwa Nyasa tuweze kufuga samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, ninaona umeniwashia taa sijui dakika zimeisha?
MWENYEKITI: Ndiyo.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na nimwombe Mheshimiwa Waziri aje kututembelea, aone tunayofanya Ziwa Nyasa. Ahsante sana. (Makofi)