Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa hii nafasi. Awali ya yote, ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa afya na uhai kwa siku ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninapenda kuipongeza sana Wizara yetu hii, Mheshimiwa Waziri na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhakikisha wavuvi na wafugaji wetu wanafikia malengo na kupata maendeleo katika nchi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumpongeza kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutuwekea Waziri mahiri na makini wa Wizara hii ambaye ni mfuatiliaji wa kila siku wa moja kwa moja. Pia, ni Waziri ambaye hana urasimu katika kutekeleza majukumu yake, anapatikana wakati wote na anawahudumia wananchi kwa wakati wote. Haki yake mtu apewe akiwa bado yupo hai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango wangu ninaendelea kuishauri Serikali kwa tozo zile mbalimbali za sekta ya uvuvi na sekta ya ufugaji ziendelee kutazamwa ili zitoe unafuu kwa wafugaji wetu na wavuvi wetu, ikiwemo vile vifaa na zana za ufugaji na uvuvi zifikiriwe tena namna ya kodi na tozo mbalimbali ili wavuvi waweze kuzimudu na kutumia katika kazi zao za kila siku. Pia, zipitiwe upya sheria zilizopitwa na wakati ambazo hazimsaidii sasa hivi mvuvi na mfugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo ninaendelea kuishauri Serikali kuharakisha mchakato wa mamlaka zile za uvuvi na ufugaji kwa sababu tuna Shirika letu la TAFICO tumelifufua. Ninaipongeza Serikali kwa juhudi hiyo ya kufufua Shirika la TAFICO ambapo tunasubiri hiyo mamlaka, ili liweze kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea na mchango wangu ninaipongeza sana Serikali. Tumeanza kupata meli ya uvuvi ya kuvua katika bahari kuu. Kwa kweli ni jambo la mfano na ninaendelea kuishauri Serikali, mchakato ule wa kuongeza meli nyingine mbili za uvuvi uendelee ili sasa tuweze kuingia kwenye uvuvi wa bahari kuu rasmi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya uzinduzi rasmi wa bandari yetu ya uvuvi kule Kilwa; ninaipongeza sana Serikali kwa kuanzisha hii bandari ya uvuvi itakuwa ni mkombozi kwa wavuvi, lakini itaongeza uchumi wa nchi. Pia, itaongeza ajira kwa vijana na wanawake na wajasiriamali mbalimbali, hasa katika maeneo ya kule Kilwa ambako bandari hii ndipo ilipo. Ninaipongeza sana Serikali na hatua nyingine ambazo inafanya za kujenga bandari nyingine katika maeneo mengine ya Pwani yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza majukumu yake, Wizara hii inafanya kazi kubwa. Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwaona na kuwajali wafugaji na wavuvi wa nchi hii kwa kuwapelekea vitendea kazi na zana za kisasa ili waweze kuingia kwenye uvuvi wa faida, uvuvi wenye tija, uvuvi utakaoleta kipato katika nchi na juhudi hizo ziendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza pia Serikali kwa kuanzisha ile chanjo ya mifugo. Sasa wafugaji waendelee kuipokea ile chanjo wafuge mifugo yao ili waweze kuingia kwenye soko la kimataifa kwa sababu tunakosa soko la kimataifa kutokana na mifugo yetu kutopatiwa ithibati kutokana na chanjo zile. Tunakosa soko kubwa, wafugaji sasa walishike hili soko la kimataifa ili kuongeza kipato chao, kuongeza ajira, lakini na Serikali nayo itapata mapato makubwa sana tutakapouza mifugo yetu nje ya nchi kwa sababu tayari ina ithibati kubwa ya kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, ninapenda kuchukua fursa hii kuwatia nguvu na kuwatia moyo watendaji na viongozi wote wa Wizara hii, lakini pia kumtia moyo na kumtia nguvu Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi kubwa anayofanya kuhakikisha sekta hizi kwenye uvuvi na ufugaji zinapewa kipaumbele. Tumeona sasa ile kuongeza bajeti katika sekta za uzalishaji, tumeona mafanikio makubwa kwenye sekta hizi, ikiwemo hayo niliyoyasema, bandari ya uvuvi, meli za uvuvi, maboti na vitendea kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeanzisha vilevile kufufua au kuongeza ufanisi katika sekta zetu za utafiti ambazo sekta hizi zitasaidia kwenye chakula cha wanyama, chakula cha samaki na kuanzisha miradi mingine ya kutengeneza chakula na samaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia na ninaunga mkono hoja. (Makofi)