Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Yannick Ikayo Ndoinyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. YANNICK I. NDOINYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi hii ili niweze kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Awali kabisa niwapongeze viongozi wote wa Wizara, (Waziri, Naibu na Makatibu Wakuu wa Wizara hiyo), lakini pia zaidi Mheshimiwa Rais kwa maono yake na usimamizi wake katika sekta hii ambayo kwa kweli inawaajiri Watanzania wengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi kama mnavyojua na kama walivyochangia wengine hii sekta ya ufugaji na nitachangia zaidi kuhusu ufugaji wa ng’ombe. Hii sekta ya ufugaji pamoja na kwamba ni mila za watu wengi sana za jamii nyingi sana hapa Tanzania, lakini ni sehemu kubwa ya uchumi na ajira yao na ambayo kwa kweli bado mikakati mikubwa inatakiwa ili kuiboresha sekta hii, ili iweze kuchangia kipato cha familia na kaya pamoja na pato la Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii wilaya ambayo ninatoka ya Ngorongoro ambayo 98% ya wakazi wa wilaya ile ni wafugaji, wangefurahi zaidi kupata matokeo makubwa sana ya ufugaji wao. Kama Waziri anavyofahamu wilaya ile iko mpakani, sisi tunastahili sasa hivi kupata viwanda vya kusindika mazao ya mifugo (nyama na maziwa) kwa sababu wanaonufaika zaidi sana sana na mazao yetu ni nchi jirani ambayo ndiyo inatoa hayo masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunayo changamoto moja kubwa sana kama hiyo ya upatikanaji wa masoko ya bidhaa za mifugo na mifugo yenyewe. Kwa kweli ningefurahi sana kama Wizara hii ingeshugulikia changamoto nyingine kubwa ya upatikanaji wa malisho ya mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, malisho ya mifugo pamoja na kwamba imebainishwa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya 2025 - 2030 kwamba itaongezeka kutoka hekta 3,000,000 hadi 6,000,000. Hilo jambo lingeharakishwa sana, upatikanaji wa malisho, kwa sababu kadri tunavyoendelea kutofikia lengo hilo la upatikanaji wa hekta 6,000,000 ndivyo wafugaji wataendelea kupoteza mifugo yao wakati wa ukame.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mifugo mingi inakufa kwa sababu inakosa majani, inakosa malisho wakati wa kiangazi na mingi sana pamoja na kwamba inakufa kwa kukosa malisho bado Serikali inatakiwa iweke msisitizo zaidi, iende mbio sana kuhakikisha kwamba malisho ya mifugo yanapatikana na kuhakikisha kwamba inazuia mifugo kufa wakati wa kiangazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mifugo mingi sana inakufa wakati wa kiangazi na mifugo inapokufa ndivyo umaskini unavyoongezeka kwa wafugaji. Tusipodhibiti vifo vya mifugo wakati wa kiangazi hatutadhibiti umaskini unaoongezeka kwa kaya na familia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru sana Serikali kwa kuweka ruzuku ya upatikanaji wa chanjo. Chanjo inapatikana kwa bei nafuu na kwa wingi, lakini inatakiwa kuhakikisha kwamba Maafisa Ugani wa Mifugo wanasambazwa karibu kila kata au kila kijiji, ili watoe elimu na hamasa ya ufugaji wa kisasa kwa wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyofahamu maeneo mengi sana ya wafugaji yanakaa karibu na mipaka ya maeneo yaliyohifadhiwa na mara nyingi sana mifugo inapokosea ikaingia maeneo yaliyohifadhiwa, mifugo ile hutaifishwa. Wito ni kukomesha utaifishwaji wa mifugo ambayo ina wenyewe. Tuache kabisa kutaifisha mifugo ya wananchi kwa sababu siyo sahihi na siyo haki kuchukua mifugo ambayo ndiyo uchumi na ndiyo chakula cha familia hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni wito wangu kuhakikisha kwamba kunajengwa aina fulani ya mahusiano kati ya maeneo yaliyohifadhiwa na wananchi na ikiwezekana kabisa hiyo sheria tuipige marufuku kwa sababu kufilisi ni vibaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimekwishaeleza, bahati mbaya sana sisi tuko mpakani na upatikanaji wa masoko ni mgumu sana kwa sababu hatuna aina nyingine yoyote ya masoko tunayoitegemea isipokuwa Kenya. Hii siyo sahihi kwa sababu mifugo mingi inauzwa Kenya, halafu inaenda kuchakatwa nyama ya mifugo huko na maziwa, tunauziwa kupitia Namanga, Arusha na wakati sisi wenyewe tungeweza kunufaika na rasilimali hizo za mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wito wangu kwa Wizara na Serikali kuhakikisha kwamba wanaweka mazingira mazuri kwa wafugaji, ili waweze kupata masoko kwa urahisi na kwa uhakika wakati wakitaka kuuza mifugo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na ninaunga mkono hoja hii. Ahsante sana. (Makofi)