Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili nitoe mchango wangu katika Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaifanya, hasa ya kuziongezea thamani sekta hizi za mifugo na uvuvi. Sisi wananchi wa Mkoa wa Lindi tumetengenezewa historia kubwa sana, tumebadilishiwa historia kubwa sana kwa kuletewa bandari ya uvuvi, bandari ya kwanza ya uvuvi katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari hii ina thamani ya shilingi 280,000,000,000. Tunatarajia kwamba, kama Mheshimiwa Waziri alivyosema, itakuwa na ajira rasmi 300 pamoja na ajira zisizokuwa rasmi, kwa maana ule mnyororo wa thamani, ziko 3,000. Pia ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuja na mkakati mwingine wa kujenga Bandari ya Uvuvi katika Wilaya ya Bagamoyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa shuhuda wa hizi bandari zote mbili kwa sababu nilikuwa Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo wakati tunapanga mipango ya kuijenga bandari ile na pia nikaenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilwa ambapo nimeshiriki moja kwa moja kwenye zile hatua za awali za kupatikana kwa bandari hii ya uvuvi ya Kilwa. Kwa hiyo ninaweza kusema kwamba kwa kweli nimeshuhudia Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan akiahidi anatekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni shuhuda mkubwa wa bandari hii ya uvuvi ninawiwa kusema kwamba, ikimpendeza Mheshimiwa Waziri amfikishie salaam Mheshimiwa Rais. Tunatamani sana Bandari ya Uvuvi ya Kilwa ipewe jina la Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ukanda huu wa Pwani ambako kuna ukubwa wa maelfu ya kilomita na kuna fukwe nzuri za bahari ilikuwa ni sahihi sana kwa Mheshimiwa Rais kutujengea hizi bandari mbili za uvuvi; kwa maana ya Kilwa na upande wa Bagamoyo. Hii inakwenda kuchochea kukuza uchumi wa blue. Bandari hii ni component, haiishii tu kuwa bandari peke yake, ni lazima kuwe na umeme wa uhakika kwenye bandari ili tuweze sasa kufanya kazi vizuri na kwa ufanisi, pia ni lazima kuwe na barabara nzuri. Hili la barabara nitakwenda kulichangia wakati utakapofika kuchangia Wizara ya Ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta hii ya bandari ya uvuvi katika Wilaya ya Kilwa itachochea pia utalii wa kufanya deep sea fishing kwenye bahari. Pia itasaidia kuondokana na uvuvi haramu, pamoja na kupata samaki ambao watakuwa wamenona. Tunatarajia kuondokana na kuvua kwenye maeneo yenye maji machache kwenda sasa kwenye kina kirefu. Ninaiomba Wizara itusaidie kuwasaidia jamii za wafugaji waliopo katika Wilaya hii ya Kilwa waweze kupewa mafunzo ya kuvua kwenye kina kirefu, lakini wapatiwe zana za kuvua kwenye hicho kina kirefu, zana za kisasa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Kilwa hakuna chuo cha uvuvi. Ninaomba ikiwapendeza; ninajua kuwa kule Mbegani Bagamoyo kuna chuo cha uvuvi, ikiwapendeza watusogezee pia kama ni branch ama ni Tawi la Mbegani lije pale Kilwa ili kurahisisha angalau kupunguza gharama za kutoka pale Kilwa kwenda kule kwenye wilaya nyingine ama kwenye mkoa mwingine kwa ajili ya kupata mafunzo haya ya uvuvi na mafunzo mengine ya kufanya uvuvi wenye tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie kwenye sekta ya mifugo. Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na mifugo mingi Barani Afrika. Ninaona namna ambavyo mifugo yetu imezagaa, ninaweza kusema imezagaa kwa kutokuwa na utekelezaji wa mipango sahihi ambayo imewekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano; tuna eneo letu pale linaitwa ninafikiri ni NARCO, ipo Ruvu; lilitengwa kwa ajili ya wafugaji kwenda kufuga mifugo yao pale wakiwa wanakodishwa; lakini mpaka sasa wafugaji wengi wanahama wanatoka kwenye maeneo hayo wanakuja kwenye maeneo ya kusini ambapo sisi wananchi wa Lindi na Mtwara na kwingineko hatujajiandaa kupokea mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kumekuwa na lindi la mifugo, sijui ni lindi au ni limbi…(Kicheko)
…sisemi wingi, lindi la mifugo katika wilaya zetu hizi za Mkoa wa Lindi wakati huo huo hatuna malisho ya uhakika kwa mifugo hiyo; na kwa bahati mbaya sana mifugo hiyo sasa inakimbilia kwenye maeneo ya wakulima. Tukumbuke hii mikoa yetu huku sisi…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Muda wako umekwisha Mheshimiwa, malizia.
MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi niombe, kwamba tuje na mipango mahususi ya kuwaweka wafugaji kwenye maeneo sahihi na salama ili tuepuke migogoro ya wakulima na wafugaji. Kwa kuwa shughuli zetu nyingi ni za kulima zaidi kuliko kufuga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja hii. Ahsante sana. (Makofi)