Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Juma Ramadhani Mustafa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. JUMA M. KAWAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi hii ili nichangie bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2026/2027. Kwanza, kabisa ninaanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amejalia mchana huu tumekutana hapa Bungeni kwa ajili ya kuwakilisha wananchi ambao wametutuma hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninapenda nimpongeze Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambazo anaendelea kuzifanya kwa kusimamia sekta hii ya mifugo kwa kuhakikisha inakuwa bora hapa nchini. Tatu, ninapenda nimshukuru Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake pamoja na watumishi wote wa Wizara kwa kuendelea kusimamia sekta hii ya mifugo na uvuvi hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Mei, 2025 idadi ya ng'ombe nchini kwetu ilikuwa ni 35,300,000; mbuzi ilikuwa 25,600,000; kondoo walikuwa 8,800,000; kuku walikuwa milioni 92,800,000; nguruwe walikuwa 3,800,000. Hii inaonyesha nini? Inaonesha kuwa Tanzania ina utajiri mkubwa wa mifugo Barani Afrika. Sekta hii ya mifugo na uvuvi inachangia pato la nchi yetu kwa asilimia 8.8. Asilimia saba inachangiwa na mifugo na asilimia 1.7 inachangiwa na uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya kuchangia huku sekta hii imekuwa ikiongeza mapato na kuajiri mamilioni ya Watanzania mijini na vijijini. Ninatokea Wilaya ya Uyui, ambayo humo humo kunapatikana jimbo langu la Igalula, ambamo mimi pamoja na wananchi wangu wa jimbo la Igalula tunaishi. Tuna idadi ya mifugo na tuna ng'ombe 400,000, tuna mbuzi 150,000. Japokuwa tuna mifugo hii bado tunakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jimbo la Igalula bado tunakabiliwa na changamoto ya malisho ya mifugo. Wananchi wetu wamekuwa wakitembea umbali mrefu kufuata malisho ya mifugo yao. Vilevile imekuwa ikisababisha migogoro kati ya wakulima na wafugaji. Ninaiomba Wizara kwa kushirikiana na Wizara nyingine iendelee kutenga na kuongeza malisho kwa ajili ya mifugo yetu ndani ya Jimbo la Igalula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakabiliwa pia na changamoto ya majosho, malambo, mabwawa na visima vya kunyweshea mifugo yetu. Wafugaji wetu wamekuwa wakitembea umbali mrefu kufuata vyanzo vya maji. Hivyo, tunaiomba Wizara iwekeze kwenye mabwawa na visima virefu kwa ajili ya kuwasaidia wafugaji wetu ili waweze kunywesha mifugo yao kwenye maeneo ya karibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Jimbo la Igalula kuna kata 11 na vijiji 58, lakini majosho hayazidi saba tu. Ninaiomba Serikali kupitia Wizara hii ya Mifugo itusaidie kutujengea majosho walau 20 ili kuweza kuwasaidia wafugaji wetu waweze kuchanja mifugo yao dhidi ya magonjwa ya kupe na magonjwa mbalimbali, ambayo yanapelekea wafugaji wetu kupata hasara kutokana na magonjwa haya, mifugo mingi inapoteza maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto kubwa sana ya watumishi. Halmashauri ya Wilaya ya Uyui ina kata 30 lakini watumishi waliopo pale ni watumishi 10 tu. Tunafahamu kwamba sekta hii ili iweze kwenda inatakiwa elimu kwa wafugaji wetu na inatakiwa zifanyike tafiti mbalimbali kwa ajili ya hawa wafugaji wetu. Sisi tuna watumishi 10 tu ndani ya kata 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali kupitia Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi ituongezee watumishi ndani ya Halmashauri yetu ya Wilaya ya Uyui, kusudi sasa hawa watumishi watakapokuja kwenye halmashauri zetu waweze kutoa elimu ya namna ya ufugaji bora kwa wafugaji wetu na namna bora ya kutumia ardhi kwa ajili ya kulisha mifugo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto kubwa sana ya mikopo kati ya wafugaji na wavuvi. Masharti yaliyowekwa kwenye mikopo wafugaji wengi na wavuvi wengi wanashindwa kunufaika na masharti haya. Mfugaji anaambiwa ili aweze kukopesheka anaambiwa awe na nyumba ya block, mvuvi naye anaambiwa awe na nyumba ya block. Sisi sote tunawafahamu wafugaji wetu, kwamba wengi wanaishi kwenye nyumba za tope na wanaishi kwenye nyumba za nyasi. Kwa hiyo wanashindwa kuifikia fursa hii ambayo Mheshimiwa Rais ameiweka kusudi wafugaji wengi waendelee kunufaika na fursa hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaiomba Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi waweze kupunguza masharti ili wafugaji wetu na wavuvi wetu waweze kunufaika na mikopo hii. Tunawaona wavuvi wangu wa Kata ya Loya na Kata ya Miswaki, wamekuwa wakishindwa kukopesheka kwa sababu ya kukosa vigezo vya kupata mikopo hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe ushauri kwa Wizara…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Muda umekwisha.

MHE. JUMA M. KAWAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie dakika moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti nyingi zimefanyika. Kwa nchi ambazo zilizoendelea zimewekeza kwenye matumizi bora ya ardhi, kwenye teknolojia na kwenye kutumia ranchi za kisasa. Kwa mfano, tunaona nchi kama Brazil wameendelea kwa kutumia vitu hivi vitatu. Kwa hiyo, ninaiomba Wizara ya Kilimo na Mifugo nasi twende tukawekeze kwenye angle hii kwa ajili ya kuwakomboa wafugaji wetu na wavuvi wetu hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, pamoja na changamoto hizi wananchi wa Jimbo la Igalula bado wanampenda…

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.

MHE. JUMA M KAWAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamalizia…

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, Mheshimiwa Zainab Rashid Kawawa.

MHE. JUMA M. KAWAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)