Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mvomero
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SARA M. ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu waliotangulia kwanza kutoa pongezi nyingi kupitia Wizara yetu hasa kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Menejimenti yote. Ninampongeza sana na kumshukuru Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, walifanya ziara ndani ya Jimbo la Mvomero mara tu walivyoapishwa wakatembelea shughuli za ufugaji, tukaenda kwenye mashamba, tunashukuru sana wananchi wa Jimbo la Mvomero hasa wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nimpongeze sana Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka nguvu nyingi sana kwenye sekta hii hasa ya mifugo. Tunajua kwamba wananchi wa Jimbo la Mvomero, wakulima na wafugaji tulikuwa hatuwezi tukaelewana kabisa, migogoro hii ilikuwa mikubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia historia kabla Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani, tulikuwa tumejenga mpaka na mitaro mikubwa kwamba wakulima wakae huku, wafugaji wakae huku, tusichangamane lakini tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliona ipo haja ya kutumia falsafa yake ya 4R tuweze kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulianzisha programu ya “Tutunzane” ambayo mlezi wetu mkubwa ni Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kwa kweli wananchi wa Mvomero tumejifunza mengi kutokea kwa Mheshimiwa Rais, kwamba siyo kila migogoro inatatuliwa kitaalamu tu. Mheshimiwa Dkt. Samia ametuonesha jinsi ya kukaa na viongozi wa dini, wazee wa kimila, machifu na mpaka sasa Programu ya Tutunzane imeleta matokeo makubwa hasa Jimbo la Mvomero. Wakulima na wafugaji kila mtu anafanya shughuli zake vizuri na kwa kuelewana. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli ni Chifu Hangaya. Ule usemi wa Chifu Hangaya tumeuona Mvomero. Ninaomba sana, Wizara tunajua imewekeza sana kwenye mifugo na tunaona kama nchi tunaongoza kwa Afrika, sisi tunayo mifugo mingi, ni namba mbili, lakini kipekee niipongeze Wizara kwamba sasa tupo kwenye top ten kwa wauzaji wa nyama kwa nchi zinazouza nyama hasa nje ya nchi. Sisi Tanzania ni top ten hasa kwa nchi za Saudi Arabia, Kuwait na nchi nyingine za Falme za Kiarabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeanza kuona matokeo mazuri, na uwekezaji huu kimsingi tumeanza kupata matokeo kuanzia mwaka 2023 mpaka sasa. Kwa hiyo, hayo ni matokeo makubwa ya Mheshimiwa Rais na juhudi za Wizara katika kuinua sekta ya mifugo hasa kwenye ubora na masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninaomba nipongeze kwenye suala la chanjo ya Taifa ya mifugo na utambuzi wa mifugo. Kwa kweli hili limetusaidia sana hasa wafugaji. Wafugaji wamekuwa wakitumia madawa mengi yenye chemical nyingi kutibu mifugo, matokeo yake nyama inakosa ladha, gharama za matibabu ni kubwa na zinapunguza thamani ya mifugo, lakini kupitia chanjo hii ya mifugo na utambuzi wa mifugo, sasa hivi imepelekea sasa nyama inauzwa nje ya nchi na gharama zile za kutunza mifugo imepungua kwa sababu chanjo ile ina kinga magonjwa mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwapongeze sana Wizara na nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa chanjo hii, na kwa Jimbo la Mvomero tumefanya vizuri. Haya ni matokeo mazuri sana katika kuongeza ubora wa nyama na uhakika wa masoko na wafugaji wamepunguza gharama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nililokuwa ninaomba ni upatikanaji wa mbegu za madume ya mifugo. Bado tunayo changamoto hiyo, na Wizara itusaidie. Sasa hivi ukitaka mbegu bora ya madume ni lazima ukanunue South Africa au uende Kenya. Tunaomba Wizara itengeneze utaratibu, ili hiyo mbegu bora ya mifugo ipatikane hapa nchini, ipunguze gharama. Unajua dume moja linafikia mpaka shilingi milioni 15, milioni 20.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile tunayo mifumo hii ya uwekezaji wa pamoja au ya PPP na tunayo maeneo makubwa ya NARCO, basi tuwatafute hao wanaoweza kutengeneza hizo mbegu bora wapewe nafasi waje wawekeze hapa ili mfugaji; na kuna vikundi mpaka vya wakina mama wanafuga, lakini hawana madume; kwa hiyo, kukiwa na sehemu ambapo upatikanaji wa madume haya yanapatikana kirahisi, basi tutaweza kuongeza tija katika ufugaji kwa wananchi wetu na kuongeza pato la nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, itasaidia kuondoa ng’ombe wa kienyeji. Sasa hawa ng’ombe wa kienyeji hakuna aina ya ng’ombe wa kienyeji. Aina bora za ng’ombe majina yake yanafahamika na yanakuwa na historia yake, lakini sasa wafugaji wanachofanya, anaenda kwenye zizi la mwenzake akiona dume kubwa la ng’ombe yeye anafikiria hii ndiyo mbegu bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tukifanya hivyo, ninaamini kabisa hii sekta ya mifugo itachangia pato la nchi na tutaweza kukomboa wananchi wetu kutoka kwenye umaskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Mnada pale wa Mikongeni, uko pale Dakawa, ni mnada wa mifugo. Nimeona presentation nzuri sana, tuna bandari ya samaki, tunasema Kilwa Fishing Harbour; basi niwaombe lile Soko au Mnada wa Mikongeni uwe wa kimataifa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa kwa mchango wako…
MHE. SARA M. ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)