Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Zena Maulidi Katambo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ZENA M. KATAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika mapendekezo ya Bajeti ya Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Lindi, hususan wakina mama, ninapenda kuipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa ambao umefanywa katika ujenzi wa bandari ya uvuvi, bandari ya Kilwa. Serikali ya Awamu ya Sita sasa hivi katika Mkoa wetu wa Lindi katika Wilaya ya Kilwa imejenga mradi wa bandari ambayo inahusiana na uvuvi yenye thamani ya shilingi bilioni 280. Mradi huu hadi sasa umefikia 98% ya utekelezaji wake, na muda wowote Mheshimiwa Rais anatarajiwa kwenda kuuzindua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkoa wa Lindi tunashukuru sana na tunaiomba Serikali kupitia mradi huu, kuna miradi mingine midogo midogo ambayo inaenda kutekelezwa inayoambatana na mradi huu wa bandari ya uvuvi. Miradi hiyo ni pamoja na kiwanda cha kuchakata samaki, soko la kisasa la samaki, karakana za matengenezo kwa ajili ya miundombinu hii ambayo itatumika kwenye uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, mradi huu pia unahusiana na ujenzi wa ghala kwa ajili ya zao la mwani. Tunafahamu kwamba zao la mwani nchi hii lilikuwa lipo nyuma kidogo na wakulima ambao wanahusiana na zao la mwani mara nyingi wamekuwa wakikumbana na changamoto ya soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao hili linajumuisha wanawake wengi katika maandalizi yake, lakini pia wanawake wengi ndio wanajihusisha katika sekta ya uzalishaji wa zao la mwani. Kwa hiyo, tunaipongeza Serikali kwa kitendo cha kuleta hili ghala ambalo tunaenda kupeleka zao la mwani katika mfumo wa soko la Stakabadhi Ghalani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo cha kulipeleka hili zao katika mfumo wa Stakabadhi Ghalani unaenda kuwahakikishia wakulima moja kwa moja uhakika wa soko na kuuza mazao yao hali ambayo inaenda kuinua kipato chao cha uchumi. Bandari hii pia tunatarajia kutoa ajira za moja kwa moja za vijana, wananchi 3,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkoa wa Lindi, tunatarajia kunufaika na huu utekelezaji wa huu mradi moja kwa moja ambapo wananchi ambao wanahusika na zoezi la uvuvi wanatarajiwa kwenda kuwezesha kwenda kuvua katika bandari kuu ambapo hapo awali kabla ya utekelezaji wa mradi huu haujatekelezwa wananchi walikuwa wanashindwa kufika kwenye yale maji makubwa, hivyo kushindwa kupata samaki wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia mradi huu wa bandari ya uvuvi tunakwenda kuboresha kipato cha Mtanzania moja kwa moja, kwa Mtanzania mmoja mmoja, pia kuinua zile familia ambazo zinahusika na shughuli za uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkoa wa Lindi wanaendelea na maandalizi ya kuhakikisha kwamba wananufaika na uwepo wa bandari hii na hawaishii tu kuwa watazamaji. Katika kuhakikisha kwamba wananchi wa Mkoa wa Lindi wananufaika, tarehe 12 mwezi wa Tano, Wilaya ya Kilwa imefanya kongamano kubwa la kuhamasisha wananchi kuwa tayari kutumia fursa ya uwekezaji katika bandari hii pale itakapoanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali, kwa sababu mradi huu unavipengele vingi, tuiombe Serikali kwamba muda utakapofika miradi hii itekelezwe kwa wakati, pia ikamilike ili kusudi zile gharama kubwa, hii shilingi bilioni 280 ambayo imeshatolewa na Serikali iende kuleta tija ya haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la mifugo. Kwa asili wananchi wa Mkoa wa Lindi sisi siyo wafugaji, lakini Serikali kati ya mwaka 2015/2020 ilikuja na mpango wa kuwahamasisha wafugaji kutoka sehemu mbalimbali za nchi kuhamia Mkoa wa Lindi kwa sababu Mkoa wa Lindi ulikuwa na eneo kubwa ambalo lipo wazi kwa ajili ya malisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wafugaji wale waliitikia wito na wamekuja kwa wingi. Hata hivyo, licha ya kwamba wafugaji wale wamekuja na kutuletea baraka ya uwepo wa chakula kama nyama na maziwa, tumekutana na changamoto ambayo sasa imeanza kuibuka, ya uwepo wa migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa baadhi ya maeneo, almost Wilaya zote...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa kwa mchango wako.

MHE. ZENA M. KATAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, almost wilaya zote wananchi wanapambana. Hivyo ninamwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja, atueleze mpango wa Serikali kuhakikisha wanapambana na changamoto hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninaunga mkono hoja. (Makofi)