Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kwanza nimpongeze sana Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa namna ambavyo Wizara hii ameibeba kama agenda binafsi katika kuleta mabadiliko makubwa. Kwa ufanisi huo ambao tunauona na namna ambavyo ameweka jitihada kubwa, inaleta matumaini kwamba Wizara hii inaenda kupata mabadiliko makubwa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nollo, ninaomba ujaribu kipaza sauti kingine cha pembeni yako.

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kuchangia masuala matatu. Moja ni suala la kuchanja mifugo; pili, ni suala la kuweka hereni kwenye mifugo yetu; na tatu, ni suala zima la malisho kwa ajili ya mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la kuweka herein, jambo hili ni muhimu sana, kwanza linatupa utambuzi wa kujua tunayo mifugo kiasi gani? Pili, lina faida muhimu sana kwamba tutaweza kuwa na takwimu ya kila mfugo. Nchi ya Botswana wamefanikiwa katika suala la utambuzi wa mifugo yao. Kwa hiyo, mfugo anapozaliwa anapewa ile electronic tag, taarifa zake zinakuwa kwenye ile tag, lakini katika masoko ndani ya nchi yao local market huwezi ukauza kama ule mfugo hauna ile ear tag. Vilevile, inawapa wafugaji utajiri, kwamba wanakuwa wanajua miliki waliyonayo ya mifugo kama inventory.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jambo hili anaweza akakopesheka benki, na anaweza akaweka insurance ya mifugo yake. Vilevile nchi ya Botswana wamefika mbali kwa sababu ya utambuzi wa mifugo na pamoja na kuchanja mifugo yao, sasa wana uwezo wa kuuza. Kwa mfano, wanauza sana nchi ya Ujerumani kwa sababu traceability ya mifugo yao inaonekana katika hali nzima ya kiafya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza sana Serikali kwa namna ambavyo wameweka jitihada kubwa katika suala zima la chanjo ya mifugo. Sasa nguvu ifanyike kulipa zile shilingi bilioni 8.6 kwa wale wakandarasi wanaodai. Jambo hili ni zuri na Serikali ifanye na ripoti ya Waziri inaonesha kwamba kiwango cha uuzaji wa nyama nje ya nchi umeongezeka kwa sababu ya utambuzi wa mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nyingine huwezi ukawauzia nyama ya mifugo ambayo haina address. Kwa hiyo, lazima muwe mna-address, lazima huo mfugo ujulikane matunzo yake na mambo mengine ikiwepo katika hali nzima ya kuchanja mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, ni suala la malisho. Bado mifugo yetu na wafugaji wetu tunafuga kwa kubahatisha. Nchi nyingi kwa mfano Zimbabwe, ulimaji wa malisho ya mifugo imekuwa ni utamaduni, na siyo jambo la Serikali kuwekeza kulima malisho ya mifugo. Hili tulibadilishe, iwe ni culture kwa ajili ya wafugaji wetu. Uwe ni utamaduni wa nchi hii, tulime malisho kwa ajili ya mifugo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile kuchunga, kwamba unatoka Shinyanga unapeleka ng’ombe mpaka Lindi, wanachunga njiani mpaka unashangaa umefika Lindi, hii ni enzi nyingine kabisa. Kwa hiyo, nilikuwa ninaomba sana suala la malisho Serikali ifanye kampeni ya kutosha ili tuweze kulima nyasi kwa ajili ya mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la majosho kwa maana ya miundombinu, tunahitaji miundombinu ya majosho, na miundombinu ya mabwawa kwa ajili ya kunywesha mifugo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala zima la abattoir (machinjio) kwa ajili ya mifugo. Kwa mfano, machijio ya hapa Dodoma, hatuwezi kusafirisha katika nchi karibu zote za Uarabuni, kwa sababu ya hali ya machinjio yale ilivyo. Ninaishukuru sana Serikali, Wizara kupitia Mheshimiwa Waziri, ametoa maelekezo kwamba machinjio yale ya Kizota yaanze kufanyiwa ukarabati ili tuweze kupeleka nyama nje ya nchi. Kwa hiyo, tukifanya hivyo tunaweza kuleta mapinduzi makubwa kwa wafugaji na sekta ya mifugo katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi, tujikite zaidi kuangalia uwekezaji. Mfugaji awe ni mwekezaji badala ya kuwa ni mtu ambaye umaskini wake na kiasi alichonacho cha ng’ombe haviendani kwa maisha anayoishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninakushukuru sana, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)