Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Ninaanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, nimesikiliza hotuba yake kwa makini nimeona kwamba, ana mwelekeo mzuri sana ambao ataufanya na utaleta matumaini makubwa sana kwa wafugaji wetu. Tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri, ameanza vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dunia ijayo maeneo ambayo yatakuwa na biashara kubwa, namba moja ni eneo la IT, namba mbili ni eneo la chakula, na namba tatu ni eneo la tiba. Wizara hii inaenda kuangukia kwenye eneo la chakula. Kama inakwenda kuangukia kwenye eneo la chakula, ni eneo ambalo linatakiwa pia Serikali ijiwekeze vizuri na iwe makini sana inapokuwa inatunza yale maeneo yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema tu mifano michache. Nimemtazama juzi Waziri wetu, kaka yetu, Mheshimiwa Dkt. Bashiru wakati Mheshimiwa Mchengerwa anawasilisha bajeti yake na akisisitiza kuhusu ujenzi wa Muhimbili, wakati anasisitiza kuhusu ujenzi wa Muhimbili, anasema sisi ni wajamaa. Niliposikia lile neno wajamaa, nikamwona Waziri Mheshimiwa Dkt. Bashiru akipiga makofi na kufurahi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninataka kumwambia Mheshimiwa Waziri, Muhimbili yake ni mashamba makubwa ya mifugo kwenye nchi hii. Muhimbili yake ni NARCO, Muhimbili yake ni Mashamba ya TALIRI, Muhimbili yake ni kila eneo ambalo kuna ardhi kubwa, ambayo ina uwezo wa kuzalisha mifugo na mambo mengine. Ni maeneo ambayo anatakiwa aende kuwekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI. Watu wa Siha wamenituma, wameniambia “ukitusemea, sema Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI amekuwa ni mtu mzuri sana kwa wafugaji wa Wilaya ya Siha na Wilaya ya Longido. Ni mtu ambaye amekuwa anamaliza migogoro vizuri na kuwatengenezea wafugaji wetu mazingira mazuri.” Ninaomba mumpigie makofi ya kutosha mkurugenzi huyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu kuna Shamba la NARCO. Ninaishukuru Wizara ya Mifugo, huko nyuma iliona lile eneo ambalo halitumiki na NARCO na TALIRI wawekezewe wafugaji wetu wadogo. Tulifanya hivyo, ikaondoa moja kwa moja migogoro ya wafugaji na wakulima, lakini imekuja hapa karibuni anatakiwa kuwekezewa mfugaji mmoja kule NARCO, anayeitwa Akram. Ushauri Wangu kwa Mheshimiwa Waziri, hatumpingi, mfugaji yule anayetaka kuwekeza, ni wa kwetu, lakini wafugaji hao wadogo ni wa kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoshauri, asipewe NARCO yote kwa sababu, kwa Kilimanjaro ambayo ardhi ni ndogo sana na hakuna maeneo ya wazi, ukimpa tu NARCO yote ukaondoa lile eneo ambalo Serikali ilikuwa imewapa wafugaji wetu, ina maana ume-deny wafugaji zaidi ya 3,000 wasifuge, wauze ng'ombe wakae nyumbani na hawatakuwa tena na mifugo kwa sababu, wewe kazi yako ni kuwaangalia wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu, naomba na Mheshimiwa Waziri amesema anakuja, aje Siha, aende Longido, awasikilize wafugaji, tukae tuangalie tuone busara ya pamoja bila kumuumiza mwekezaji anayetakiwa kuwekeza pale, lakini bila kuwaumiza na hawa wafugaji wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu mwingine, hili ni eneo la hela. Nirudi tu pale kwenye afya. Ukiangalia madaktari wetu wanafurahi sana kufanya zile kazi. Ukienda Muhimbili na investment kwenye hospitali zetu za mikoa, asilimia kubwa uwekezaji unaofanyika ndani ya hospitali wanazalisha wenyewe madaktari wetu na wanajipa incentive.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri kwenye haya mashamba makubwa na kwenye hizi ardhi zetu kubwa tuwekeze ndani yake kwa njia namba moja. Kwa mfano, TALIRI ambao kazi yao ni utafiti, ni kwa nini tusifanye kazi kubwa ya kuongea na vyuo vikuu vikubwa na taasisi kubwa za vyuo vikuu, ndani ya zile taasisi pakawekwa research kubwa ya kufanya mifugo na wakashirikiana kufanya utafiti?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo, moja, itatusaidia kujua mambo mengi. Itaboresha mifungo yetu, na pia itaongeza incentive kwa wataalam wetu ambao wapo sasa. Nikiwaangalia ninaona, ukiondoa mshahara, hakuna namna nyingine wanayopata kama incentive. Kwa hiyo, tukitengeneze namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, pale kwetu Siha kuna shamba la TALIRI na shamba la NARCO. Tukisema pale TALIRI wanafanya utafiti halafu NARCO wanazalisha ng’ombe bora, halafu ndani ya NARCO wanatengeneza kiwanda, na kile kiwanda kinakuwa kinauza nje; na ukienda pale kwenye shamba la TALIRI mpaka kuna stripe ya kushuka ndege ndogo, maana yake ukiweka kiwanda pale, na vitu vingine wanaweza wakazalisha na faida inayopatikana, itaendelea kuboresha vituo vyetu vya mifugo, na kuongeza incentive kwa wataalam wetu Maprofesa ambao wapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inauma sana ukimwona Profesa na mazingira yake anapofanyia kazi, haiendani na ukubwa wa elimu aliyonayo. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri, moja ya kazi ambayo anataka afanye, na ninataka tu kukambia kwamba Serikali imefanya kazi kubwa sana, lakini mfano mzuri ni upande huu wa afya ambayo imefanyika. Serikali haijaongeza hela yoyote ya incentive. Imetengeneza mazingira ya wataalam kuzalisha wenyewe humo humo, fedha hizo zikasaidia Serikali na fedha hizo zikasaidia wataalam kufanya vizuri.

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, muda wako umeisha.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamkaribisha Mheshimiwa Waziri Siha, na ninaomba tukafanye vizuri kwa maana ya uzalendo na ujamaa tukauone kwa wakulima wetu. Twende tuwasimamie wawekezaji, lakini pamoja na wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ninaunga mkono hoja mkuu. (Kicheko)