Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru. Kwa sababu, muda ni mfupi ninachukua fursa hii kuipongeza Wizara na watendaji wote kwa kazi kubwa wanayoifanya. Sekta au Wizara ya Uvuvi, Mifugo na Kilimo ni kati ya sekta ambazo tunapoongea uchumi jumuishi ndiyo zinajumuisha vijana wengi, akinamama wengi na Watanzania wengi kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza Serikali yangu kwa juhudi ambazo imezifanya, hasa ununuzi wa meli kubwa ya uvuvi. Ninadhani hapa tunakwenda kwenye uchumi ambao tumeukosa kwa muda mrefu. Nilikuwa ninaangalia takwimu hapa, ambazo zimetoka kwenye Wizara ya Mifugo na Uvuvi, wanasema Tanzania tunazalisha almost tani 500,000 za samaki kutoka baharini. Kwenye maziwa, tuna almost tani 400,000; bahari kuu na kwenye mabwawa. Nimeangalia mahitaji ya samaki Tanzania, tunahitaji zaidi ya tani milioni moja. Kwa hiyo, tuna upungufu wa kitoweo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Waziri Dkt. Bashiru, ameanza vizuri kazi. Alipoanza alitutembelea Kagera, alikuja pale tukakaa na wavuvi tukasikiliza matatizo yao; amekaa na wafugaji akasikiliza matatizo yao. Ninadhani kilio cha wavuvi alikisikia Mheshimiwa Waziri, hasa tunapoongelea Wilaya ya Muleba. Wilaya ya Muleba ina ukubwa wa square metre 10,000, lakini 7,000 ni maji. Kwa hiyo, tunaishi kwenye maji sisi. Wilaya ya Muleba mapato yetu makubwa yanatokana na mazao ya uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Mheshimiwa Waziri wakati anasoma hotuba yake ameongelea uanzishwaji wa mamlaka ya uvuvi. Ninadhani Mheshimiwa Waziri akilitekeleza hili, kwanza mazao na mapato uvuvi yatapanda na tutapunguza tatizo tulilonalo la vijana kupata ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema, kama nilivyoanza, kwamba hizi ni sekta zinazoakisi uchumi jumuishi ambao unahusisha watu wengi na vijana wengi. Kwa hili ninaomba tumuunge mkono Mheshimiwa Waziri, tuanzishe hii mamlaka ya uvuvi ikadhibiti tatizo kubwa la uvuvi haramu linaloendelea katika Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuishi karibu na ziwa, samaki ni tatizo. Ni tatizo, siyo kwamba watu hawavui, siyo kwamba watu hawana mitaji, mitaji wanayo na wanaingia ziwani, lakini hakuna samaki. Ninaomba tukadhibiti hili, ili tuokoe maziwa yetu kwa vizazi vingine. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri, vijana wa Muleba wamenituma, wameniambia jana, na leo wanashukuru. Wamewapatiwa vizimba na wanaendelea kuzalisha na kufuga samaki pale, lakini tatizo kubwa walilonalo Wilaya ya Muleba, vijana hawana chakula cha samaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanapaswa kufuata chakula kutoka Mwanza. Vile vifaranga walivyowapatia tunashukuru, lakini vingine vinaanza kupotea na kufa kwa sababu, ya kukosa chakula. Ninaomba hili sasa tuliangalie na kwenye mipango yetu tujenge kiwanda cha chakula cha samaki Mkoa wa Kagera. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kwamba, Mheshimiwa Waziri, alipokuja Muleba, watu walitoa kilio chao na akawapatia mwezi mmoja kutoa suluhu ya kilio chao. Ninatumaini atakuwa amelifanyia kazi. Ameongea kwamba Ziwa Ikimba wataanza kuvua Samaki. Tatizo tulilonalo Ziwa Burigi, tulipoongelea sera, dira, Mkumbi II, 2025 – 2050, tuliongelea Sekta Binafsi. Mialo ya Ziwa Burigi, ninasisitiza kwa umakini mkubwa zaidi, mialo iliyokuwa pale ilifungwa na Serikali. Tunaomba kama ziwa kazi yake ni kuvua samaki, sasa tunafunga mialo tunategemea kufanya nini na hilo ziwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba wananchi ambao wanazunguka Ziwa Burigi wapatiwe fursa ya kuendelea kuvua samaki na kuchochea maendeleo ya familia zao, kukuza uchumi wao na uchumi wa Taifa. Ninaomba Mheshimiwa Waziri, atakapokuja kumalizia hotuba yake atuambie nini hatima ya mialo ya Ziwa Burigi iliyofungwa, na tunakwenda kuifungua lini, ili ziwa liwe na maana? Ni maji pamoja na uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ufugaji, Kagera tuna vitalu zaidi. Ranch za Taifa ni zaidi ya nusu, lakini Mheshimiwa Waziri alikutana na wafugaji. Ninaiomba Serikali iwekeze zaidi, ndugu yangu, Mheshimiwa Nsekela amesema…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga hoja mkono. Nitaomba maelezo jinsi ya ufunguaji wa mialo ya Ziwa Burigi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana. Naunga hoja mkono. (Makofi)