Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyerwa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KHALID M. NSEKELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa nafasi hii ya kuchangia bajeti hii nikiwa wa kwanza kabisa. Kwanza kabisa, ninaomba nimpomngeze Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake na jitihada za makusudi za kuweza kuinua sekta hii ya mifugo na uvuvi kwa sababu tumeshuhudia tarehe 25 Aprili akizindua Meli ya Uvuvi wa Bahari Kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo hiki ni historia kwa Tanzania, lakini inaonesha kabisa kwamba ni jinsi gani Mheshimiwa Rais ana maono na maslahi mapana katika Uchumi wa Buluu. Kwa kuwa tumezoea kumiliki Bahari, lakini sasa ni dhahiri kwamba tunamiliki Bahari, na pia tunamiliki na uchumi wa bahari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza pia Mheshimiwa Waziri na timu nzima ya Wizara kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya katika jitihada za makusudi kuweza kuona tunapata mabadiliko makubwa na chanya katika uvuvi na ufugaji, lakini tunatambua kwamba, wafugaji na wavuvi ni jamii kubwa sana ambayo imepiga kura za kutosha kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Pamoja na kazi kubwa inayofanyika, bado tunaona kuna changamoto nyingi sana zinawakumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumemsikia Mheshimiwa Waziri akiwasilisha hoja nzuri, lakini sijasikia kitu cha kumtambua mfugaji kama mwekezaji. Wameonesha jitihada za kutambua mifugo, jitihada za kampeni za kufanya chanjo, lakini hoja yangu sijaisikia, ya kumtambua mfugaji kama mwekezaji. Hapa ninataka kusema nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba, ni muda muafaka sasa mfugaji atambulike kama mwekezaji katika nchi yake kwa sababu, tunajua ufugaji unagusa zaidi ya 33% ya ajira za Watanzania. Tunajua kuna wafugaji wakubwa sana ambao wana uwezo, wana vitalu, wana leseni, lakini wafugaji hao hawawezi kufika hata taasisi za kibenki kupata mikopo kwa kutumia vile vibali vyao au leseni kama collateral ya kupata mikopo. Kwa hiyo, ni muda muafaka, kama Wizara kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kusema kwamba, Wizara zina haja ya kushirikiana. Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi wakae na Wizara ya Viwanda na Biashara waone jinsi gani ya kushirikiana na taasisi za kifedha kumtambua huyu mfugaji kwamba, sasa kwa sababu ana leseni na kibali cha miaka 20 na ana kitalu kina ng'ombe wa kutosha, itumike ile kama dhamana ya yeye kukopa na kujiendeleza kwenye ufugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni changamoto ambayo wanakutana nayo wafugaji. Wafugaji kwa sasa kuna hili jambo la wachimba madini, wanaingia kwenye sehemu za ufugaji kwa sababu, wameambiwa kuna madini. Wanachimba kwa ajili ya kupata madini, wanaacha mashimo makubwa. Sisi Kyerwa tuna ng'ombe takribani 80,000 lakini kwa sasa hivi tumeingiliwa na watu wa kuchimba madini aina ya tin. Wanaacha mashimo makubwa, kitu ambacho kinaanza kusababisha ng'ombe wengi kufariki, hii ni changamoto kubwa. Kwa hiyo, ninatoa rai kwa Wizara kwamba, wakae washirikiane na Wizara hii ya Nishati kuona ni jinsi gani wataweza kuokoa hili janga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, ninaenda kwenye uvuvi kwa sababu ya muda, hatuwezi kuongea vingi sana, lakini uvuvi tumeona jitihada zimefanyika. Mheshimiwa Rais anafanya jitihada kubwa sana. Ninachoweza kusema kwa Mheshimiwa Waziri ni kwamba, ni wakati muafaka sasa kuwekeza fedha nyingi za Serikali kwenye kupanua na kuendeleza hii Sekta ya Uvuvi. Kuna haja sasa Wizara iweke nguvu nyingi sana katika kupambana na changamoto ya uvuvi haramu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni janga kubwa sana kwa uvuvi. Tunatambua bado wapo watu wanavua kwa kutumia baruti, bado wapo wavuvi wanatumia sumu, bado wapo wengine wanatumia nyavu zile ndogo kwa kuvua samaki wachanga. Hili ni janga kubwa. Wakati Serikali inaweka nguvu kubwa kuendeleza hii sekta, huku tunaingiziwa watu wanaturudisha nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Wizara kwa kuongozwa na Mheshimiwa Waziri, na ninampongeza kwa hilo, kokoro ambalo nimelikamata kwenye Ziwa Tanganyika, bado katika vyanzo vyote vya wavuvi kuna haja ya kufanya kazi kubwa kuweza kuona huu uvuvi haramu unakabiliwa na unazuiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Kamati imetoa maelekezo; wakati tumetembelea TAFICO tumekuta pale kuna magari matatu ya cold chain kwa ajili ya kusafirisha samaki. Magari hayo yamekaa muda mrefu sana. Sasa ninaomba Mheshimiwa Waziri wakati anamaliza atuelezee kama magari hayo tayari yameanza kufanya kazi, kwa sababu, zile ni fedha za Serikali zimewekwa pale. Magari yanavyozidi kukaa pale chini, maana yake yanaanza kuharibika. Kwa hiyo, tunaomba, magari hayo yamenunuliwa, na ni fedha ya Serikali, yaanze kufanya kazi, tuone tija katika hilo suala la uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa kwa kutambua umuhimu mkubwa wa wavuvi na ufugaji...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, muda wako umeisha.
MHE. KHALID M. NSEKELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru. Ninaunga mkono hoja. (Makofi)