Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Agnes Elias Hokororo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa, ni mara yangu ya kwanza katika Bunge hili la Kumi na Tatu, nianze kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali kuingia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nikishukuru chama changu, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wote tunakubaliana, ninampongeza Mheshimiwa Rais, kwanza kwa umakini wake, lakini pili kwa uimara, tatu kwa ustahimilivu na nne kwa usimamizi thabiti wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninadhani wote tunaendelea kushuhudia namna Mheshimiwa Rais anavyoendelea kutuongoza sisi Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani zangu za tatu, ninazipeleka kwa wanawake wa Mkoa wa Mtwara kwa kunipa tena nafasi ya kurudi katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sasa nijikite katika hotuba iliyopo mezani ya bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria. Kama nilivyotangulia kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais, ninarejea tena kumpongeza sana kwa sababu katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri yameonekana mafanikio kadhaa tena ni mengi. Ninawapongeza sana Wizara kwa kazi kubwa waliyoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/2026, yapo mambo yamefanyika. Nikirejea katika mzungumzaji aliyepita katika ile kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia ambayo imejulikana kwa Kimakuwa kama Mama Samia Legal Aid. Tumeona yako mafanikio makubwa sana, lakini yale ni maono ya Mheshimiwa Rais. Ile kampeni imewawezesha wananchi ambao walikuwa na uhitaji mkubwa wa kuhakikisha kwamba haki yao inapatikana na hasa wanawake na makundi maalum na watu wa pembezoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri inaonekana jumla ya watu waliofikiwa ni 4,157,065,000. Ukiangalia kwa makundi ya wanawake na wanaume unaona karibu kuna uwiano sawa. Lakini migogoro iliyoshughulikiwa ukiacha ardhi, kuna masuala ya mirathi, kuna masuala ya talaka na migongano ya ndoa, lakini kuna masuala ya ukatili wa kijinsia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii ukiangalia kwa awamu ya kwanza imekuwa na mafanikio makubwa. Ni ombi langu, ninatambua awamu ya kwanza imeishia hii 2026, (2023 - 2026). Ni ombi langu na rai yangu kwa Serikali ya chama changu kwamba, awamu ya pili ni muhimu ianze sasa 2026 - 2030 kwa sababu, kuna uhitaji mkubwa wa wananchi walio pembezoni, wanaohitaji kutatuliwa migogoro yao na kupata haki. Hii inathibitishwa na hata ziara za viongozi tunaona bado kuna wananchi wengi wanaowasilisha migogoro kama sehemu ya matatizo ya kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo ninaomba nijielekeze ni Taasisi ya RITA. RITA iko chini kwenye Ofisi za Wakuu wa Wilaya na kwa ushahidi, ofisi hii haina manpower za kutosha, lakini haina pia hata vitendea kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakubaliana na mimi ofisi za ma-DAS ndizo zinazosimamia RITA, lakini kazi inayofanywa na RITA ni kubwa sana. Hapa kuna changamoto ambazo pengine ni kutokana na fedha, lakini fedha ambazo zinatakiwa ziende RITA zinatokana na retention, ambapo mara nyingi huwa haiendi. Hata kama kunakuwa kuna kazi imefanyika, lakini zile fedha hazirudi kwenye ofisi za RITA kwenye wilaya zetu. Inakwamisha kazi ya usajili wa vizazi na vifo na tunafahamu, sisi tumekuwa tukifanya sensa kila baada ya miaka 10. Je, hii miaka ya katikati hapa hatuhitaji kufahamu idadi ya vizazi vilivyopo? (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wakati nchi inaendelea kupanga mipango ya maendeleo na Bunge tunapopitisha, ni muhimu kuzingatia pia idadi ya watu mwaka kwa mwaka na hii kazi inafanywa na RITA. Kukosekana kwa rasilimali katika RITA inakwamisha mamlaka nyingine za Serikali Ikiwemo NIDA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu sasa hivi katika shughuli zote, cheti cha kuzaliwa ni muhimu sana. Tumekuwa tukishuhudia wakati vijana wetu wanapotaka kwenda chuo kumekuwa na foleni kubwa sana katika ofisi za RITA, lakini wakati wanapotaka kujiunga, kwa mfano na JKT, hata kazi zinazotolewa na vyombo lazima wawe na cheti cha kuzaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni muhimu sana ili NIDA ifanye vizuri kwa kuwa cheti cha kuzaliwa ni kigezo kikubwa sana katika kupata namba ya NIDA ama namba ya utambulisho wa kitaifa, ni muhimu sana tukaimarisha RITA kwa vitendea kazi, rasilimali watu na fedha ili iweze kutekeleza majukumu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu na ninaamini ni la mwisho; katika yale mafanikio ya Wizara ipo kazi kubwa pia wameifanya katika bajeti, tumeiona katika taarifa hii. Suala la urekebu wa sheria, Sheria 446 zote tulizonazo, zimefanyiwa urekebu. Kwanza suala la urekebu wa sheria ni gumu, lakini pia linahitaji muda na linahitaji fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa nini? Kwa sababu kazi hii ni ngumu. Ilifanyika kwa mara ya kwanza miaka 60 iliyopita, ikafanyika kwa mara ya pili mwaka 2002 na imefanyika kwa mara ya tatu mwaka 2023. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee 2023 kwa nini? Mara ya kwanza ilitumia fedha za wahisani, mara ya pili ikatumia fedha za wahisani, World Bank lakini mara ya tatu tumetumia fedha za ndani, fedha za walipa kodi na wataalam wa ndani. Kwa hiyo, sisi lazima tutembee kifua mbele. Pamoja na yale mambo mengine yote katika sekta zote ambayo Mheshimiwa Rais amekuwa akiyasimamia na kuyatekeleza kikamilifu, lakini kwenye eneo hili la haki na usawa kwa Watanzania wote amekuwa akilifanya kwa kiwango cha juu cha kupigiwa mfano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwenye eneo la urekebu, kwa kuwa sasa juzuu zipo, ni muhimu sana tukapata soft copy ama nakala tete hasa kwa sisi Wabunge watunga sheria, lakini na kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa ili tuendelee kuzitumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja na ahsante sana kwa nafasi. (Makofi)