Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Dr. Advocate Damas Daniel Ndumbaro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Songea Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kupata fursa ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria. Ningependa nianze na Mhimili wa Mahakama. Takwimu zilizotolewa hapa zinaonesha bayana kutoka mwaka 2021 wakati Dkt. Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani hadi mwaka 2025 takwimu za bajeti ya Mahakama zimekuwa zikiongezeka. Mwaka 2021 bajeti ya Mahakama ilikuwa ni bilioni 166, mwaka 2025 bajeti ya Mahakama ni shilingi bilioni 321, sawa na ongezeko la 95%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi si namba tu, ni namba ambazo zinaonyesha dhamira ya Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha kwamba Mhimili wa Mahakama unatenda haki kwa wananchi wake; na ili utende haki ni lazima wapewe vitendea kazi na moja kati ya vitendea kazi ni ongezeko la bajeti hiyo. Mheshimiwa Rais kwenye hili tunamshukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwenye ajira, katika kipindi cha miaka mitano Mahakama imeajiri wafanyakazi wapya 2081, ambapo Majaji wa Mahakama Kuu wameongezeka kutoka Majaji 84 hadi Majaji 104. Majaji wa Makahakama ya Rufani wameongezeka kutoka Majaji 25 hadi 37 na wengi wao wakiwa wanawake. Hapa lengo ni kupunguza msongamano uliokuwepo Mahakamani kwa muda mrefu; na matokeo yake sasa ukienda Magereza unaona kabisa msongamano umepungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeambiwa hapa kwenye hizi taarifa za leo, msongamano wa mashauri katika Mahakama zetu ni asilimia nne tu na kuifanya Mahakama ya Tanzania iongoze katika ufanisi kwenye hiki kigezo. Haya ni matokeo ya Mheshimiwa Rais kwa kufanya uteuzi wa Majaji na kuongeza ajira za Waheshimiwa Mahakimu ili tuweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa miundombinu ya Mahakama jumla ya majengo 120 yamejengwa na kukarabatiwa katika miaka mitano iliyopita. Kati ya majengo hayo majengo nane ni ya Mahakama Kuu, majengo 35 ni ya Mahakama za Wilaya, majengo 72 ni Mahakama ya Mwanzo. Hii inaonyesha kwa namna gani Serikali na Mheshimiwa Rais siyo tu wamejali ajira na kuongeza bajeti, pia amekwenda kuhakikisha majengo ambayo ndiyo vituo vya utoaji haki kuanzia Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya na Mahakama Kuu zinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taarifa ya Kamati ya Bajeti tumesikia hapa; Tanzania ni nchi ya pili duniani kuwa na vituo vya pamoja vya utoaji haki na nchi ya kwanza Barani Afrika katika eneo hilo. Mimi kule Songea Mjini katika jimbo langu nimejengewa kituo cha pamoja cha utoaji haki ambacho tunatarajia baada ya kukamilika kitaleta ufanisi mkubwa sana. Hivyo, kwenye hili tunawapongeza Mahakama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hoja ya kuhakikisha kwamba mabaraza ya ardhi na nyumba yanahamia Mhimili wa Mahakama. Mimi ninasema tumechelewa sana, hili lilipaswa lifanyike jana. Niliombe Bunge hili Tukufu tuichukue hii kama ajenda; na kwa kupitia hii bajeti ambayo inakwenda kupitishwa leo Mabaraza ya Ardhi na Nyumba yarudi katika Mhimili wa Mahakama. Kwa sababu kwa mujibu wa Katiba, Mahakama ndicho chombo kilichokasimiwa mamlaka ya utatuzi wa migogoro. Tuwaache ambao wana mamlaka ya Kikatiba waweze kufanya shughuli hiyo kwa mujibu wa Katiba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu niongelee Mama Samia Legal Aid Campaign. Ni kampeni ambayo imefanyika kwa mafanikio makubwa, imezunguka mikoa yote 31 ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Katika Kampeni hii imejionyesha kwamba tatizo linaloongoza ni migogoro ya ardhi. Katika migogoro yote 7,600,000 ambayo imepatikana ndani ya mzunguko wa kwanza, migogoro 2,400,000, sawa na 32% inatokana na eneo la ardhi. Namba hizi zinatuonyesha kuna shida kwenye ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, ile suluhu ambayo imependekezwa hapa, kwamba utatuzi wa migogoro ya ardhi urudi Mahakamani, ndiyo suluhu hasa ya kuipunguza hii 32%. Bila hivyo migogoro ya ardhi itaendelea, wananchi wataendelea kupigana, wafugaji na wakulima wataendelea kuuana na sisi tupo tumekaa hapa tunaliangalia tu; hilo haliwezekani. Hili lazima tulisimamie vizuri kabisa

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalize kwa kuongelea Dira 2050. Dira ya 2050 imesema kwamba, utawala bora, haki pamoja na mifumo imara ya kisheria ndiyo msingi wa kiuchumi. Tunapokwenda kuitafuta dola trilioni moja, ni lazima kwanza tuwekeze katika suala la utawala bora, ni lazima kwanza tuwekeze katika suala la haki, ni lazima kwanza tuwekeze katika mifumo imara ya kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ambayo Mheshimiwa Dkt. Juma Homera ameiwasilisha leo, inakwenda kutekeleza Dira ya 2050. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, kwa kuwasilisha bajeti nzuri, nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kumuunga mkono Mheshimiwa Waziri katika bajeti hii. Nimpongeze sana Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuleta bajeti hii ili Dira ya 2050 iweze kufanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana, niliombe Bunge lako Tukufu lipitishe bajeti hii ambayo ninaiunga mkono ili tukatekeleze Dira ya 2050. Ahsante sana. (Makofi)