Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja iliyopo mezani; hoja ya hotuba ya bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake mahiri, thabiti na wenye maono ya mbali ambao umeendelea kuleta mafanikio makubwa kwenye sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha ninaomba kutumia nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa uongozi wao imara na maelekezo yao thabiti ambayo yanatuongoza katika utekelezaji wa majukumu yetu Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa ninapenda kutumia nafasi hii kumshukuru Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Dkt. Juma Homera kwa uongozi wake bora, malezi, miongozo na maelekezo mbalimbali ambayo ananipatia ambayo imekuwa ikiniwezesha kufanya majukumu yangu kwa amani, utulivu na ufanisi. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia kutumia nafasi hii kumshukuru sana Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mheshimiwa George Masaju na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mheshimiwa Hamza Johari. Kwa hakika wamekuwa ni walimu wangu kwa siku zote na wamekuwa na mchango wa kipekee katika kunijenga kitaaluma pamoja na katika utekelezaji wa majukumu yangu; ninawashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatumia nafasi hii vilevile kutambua mchango wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Ndugu Eliakim Maswi, pamoja na timu nzima ya Management ya Wizara ya Katiba na Sheria, bila kuwasahau wasaidizi wangu wa karibu, ambapo nina Katibu wangu Wakili Amani, Karani Shani Suleiman pamoja na dereva wangu Sabri. Kwa hakika ndugu Katibu Mkuu na timu yake yote hii ya Wizara ya Katiba na Sheria wamekuwa ni msaada mkubwa sana katika utekelezaji wa majukumu yangu; ninawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa ninatumia pia fursa ya kulishukuru Bunge hili Tukufu chini ya uongozi wa Mheshimiwa Azzan Zungu, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitambue mchango wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria wakiongozwa na Mwenyekiti wao Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro, pamoja na Waheshimiwa wote ambao wamechangia hoja hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, michango ya Waheshimiwa Wabunge tumeisikiliza kwa makini, maoni yao tumeyapokea na maelekezo yao tutayazingatia katika utekelezaji wa majukumu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Msingi Mkuu wa Dira 2050 ni Utawala, Amani, Usalama na Utulivu. Huu ni msingi unaobeba mustakabali wa Tanzania ya kesho; ni msingi unaotofautisha Taifa linalokuwa kwa bahati na Taifa linalojengwa kwa makusudi. Ni muhimu kutambua kwamba katika historia ni kwa mara ya kwanza sekta ya sheria imewekwa katikati ya mjadala wa uchumi wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni hatua ya kihistoria sana kwa kuwa tumetoka katika mtazamo wa kuitazama sekta ya sheria kama sekta mtumiaji wa rasilimali na sasa tunaijenga sekta ya sheria kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi, mlinzi wa uwekezaji na nguzo ya kuaminika ya utulivu wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna uchumi wa kisasa unaoweza kustawi bila uhakika wa sheria. Vilevile, hakuna mwekezaji anayeweza kuwekeza bila ulinzi wa haki; na hakuna maendeleo endelevu bila mifumo ya haki inayofanya kazi kwa ufanisi, usawa na uwazi. ukiitazama Dira yetu hii 2050 ina nguzo tatu. Nguzo ya kwanza ni uchumi imara, jumuishi na shindani; nguzo ya pili ni uwezo wa watu na maendeleo ya jamii; na nguzo ya tatu uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nguzo hizi za Dira 2050 haziwezi kuota, haziwezi kujengwa kama hatuna msingi imara ambao tumeutaja hapa, wa utawala, amani, usalama na utulivu; ambao kimsingi msingi mkuu huu pamoja na mambo mengine unahusisha mageuzi ya kina ya kimfumo, ili kujenga Taifa ambalo sheria siyo kikwazo bali ni daraja la maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamechangia hapa, wamegusia maeneo kadha wa kadha. Hata hivyo, ninaomba kuzungumzia baadhi ya maeneo kwa sababu Mheshimiwa Waziri atakuja kuhitimisha atazungumza na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa wabunge wengi wamezungumzia kuhusiana na kazi kubwa inayofanyika katika sekta hii ya sheria ambayo ni kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid campaign). Waheshimiwa Wabunge wafahamu kuwa mkakati huu na kampeni hii ilianzishwa kwa maono ya mwenyewe Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa ana nia na lengo la kuhakikisha kuwa anaimarisha upatikanaji wa haki kwa Watanzania wote na hususan wale wenye mahitaji maalum ambao hawawezi kumudu gharama za kuwa na mawakili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Waheshimiwa Wabunge walivyotambua hapa, awamu ya kwanza ya kampeni hii ambayo ilianza mwezi Machi, 2023 na kwisha mwezi Februari, 2026. Ni awamu ambayo ilihusisha wataalam wa sheria, Mawakili kuzunguka katika mikoa yote 26 kwenda kuwatafuta wale wenye uhitaji na kutatua migogoro yao ya kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya Watanzania 7,462,000 walifikiwa katika huduma hii muhimu ya upatikanaji wa haki. Kampeni hii kwa kweli imezaa matunda makubwa sana kwa kuwa imepunguza migogoro na imeongeza upatikanaji wa haki kwa uharaka na kwa njia rafiki zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaomba niwatangazie Waheshimiwa Wabunge kwamba, mpango sasa wa pili wa kampeni hii ya Mama Samia Legal Aid campaign tunatarajia kuizindua siku ya tarehe 30 Aprili, 2026 katika Mkoa wa Dodoma. Tunatarajia awamu hii lengo ni kwenda kufika katika maeneo yenye uhitaji mkubwa ya vijijini tofauti na kubakia kwenye miji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu hii tutakuwa tunaweka kambi kwa siku 15, tofauti na awali ilikuwa ni siku 10. Hii yote ni dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kwamba wananchi wote wanapata haki bila ubaguzi na ili wanapopata haki hiyo inaweza kuchangia katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Waheshimiwa Wabunge walizungumza kuhusiana na masuala ya mrundikano wa mashauri katika Mahakama na kuhusiana na kesi; kwamba, kuwe kuna uharaka wa kesi kusikilizwa. Kwenye eneo hili ninaomba kusema hivi; kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imefanya uwekezaji mkubwa sana katika mhimili huu wa Mahakama ili kuhakikisha na kuboresha upatikanaji wa haki kwa Watanzania wote. Ukisoma Ibara ya 107A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazungumza hapa, kwamba mamlaka ya mwisho ya kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa ni Mahakama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama inatambua kwamba utoaji haki hauishii tu kwenye kusikiliza mashauri; kwamba, upatikanaji wa haki na utoaji wa haki unahusisha pia katika masuala mengine muhimu ikiwemo pia kuendeleza miundombinu ya majengo ya Mahakama ambayo Watanzania wanaweza wakafika kwa ajili ya kupata huduma za haki. Ndiyo maana Mahakama inatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi na ukarabati wa miundobinu ya Mahakama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye huu mradi umeenda uwekezaji wa shilingi bilioni 524.9 tisa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Tanzania nzima majengo ya Mahakama yanakarabatiwa na kwenye maeneo ambayo hamna majengo, majengo ya kisasa yanajengwa kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa Watanzania. Hii ndiyo Serikali ya Awamu ya Sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyozungumza wakati huu katika mikoa 25 kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara tayari kuna Mahakama Kuu, zipo na zinatoa huduma kwa wananchi. Katika kipindi hiki cha miaka mitano, Mahakama Kuu 15 zimejengwa katika muundo wa vituo jumuishi vya upatikanaji haki au vituo jumuishi vya Mahakama Kuu. Vituo hivi ni vya kipekee kabisa ambavyo vinakuwa na ngazi zote za Mahakama kwenye jengo moja; kwa maana ya jengo la Mahakama Kuu. Yaani kunakuwa na jengo la Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama ya Wilaya pamoja na Mahakama za Mwanzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni nini? Hii inaleta wepesi kwa Watanzania, kwa wananchi kupata haki yao. Kwa maana ule muda waliokuwa wanatumia, zile gharama walizokuwa wanatumia kutoka katika ngazi moja ya Mahakama kwenda kwenye ngazi nyingine ya Mahakama, wanakuwa wameepuka na maisha yao yanakuwa ni rahisi kwa kuwa changamoto zao na haki yao inaweza ikapatikana kwa gharama nafuu na kwa urahisi. Hii yote ni kazi kubwa na uwekezaji mkubwa ambao umefanyika katika Mhimili huu wa Mahakama katika kipindi cha Awamu ya Sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upekee wa hivi vituo pia upo katika kuwa na wadau mbalimbali wa haki ambao nao wapo katika jengo moja. Wadau mbalimbali ninaowazungumzia hapa ni Jeshi la Polisi nao wanakuwa na chumba katika jengo hilo; watu wa ustawi wa jamii nao wanakuwa na chumba katika jengo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kunakuwa na watu wa huduma ya msaada wa kisheria, kunakuwa na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali, kuna hadi chumba cha kunyonyesha watoto ambacho akina mama wanaweza wakaenda wakanyonyesha watoto wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo unaona kwamba huu ni uwekezaji mkubwa sana unaofanya mapinduzi makubwa ya kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata haki na katika mazingira ambayo ni mazuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha muhimu siyo tu upatikanaji wa haki. Hata ukisoma Ibara hii ya 107A(2)(b) inasema kwamba pamoja na mambo mengine inaipa mamlaka Mahakama kwamba kutokuchelewesha haki bila sababu ya msingi. Wanasema hivi; “Justice delayed is justice denied”. Ukichelewesha haki ni sawasawa na umeinyima hiyo haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ukiangalia muktadha wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inataka Watanzania wapate haki kwa wakati. Kwa hiyo hoja siyo tu upatikanaji wa haki, lakini hiyo haki iwe imepatikana kwa wakati. Kwa hiyo kuwa na mifumo na majengo bora ya namna hii unawezesha upatikanaji wa haki kwa wakati, kama ibara ya 107A(2)(b) inavyotaka iwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama kuna matokeo ambayo tunayaona; na ndiyo maana mlundikano wa mashauri umepungua. Kwa sasa tuna mlundikano wa mashauri katika Mahakama zetu kwa asilimia nne tu. Hii asilimia nne Mahakama tayari inaifanyia kazi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kunakuwa hamna mrundikano kabisa wa mashauri katika Mahakama, wananchi wapate haki yao kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa Mahakama za Wilaya, Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi kwa maana walipokuwa wanachangia wamegusia. Kwenye Mahakama za Wilaya, wilaya zimejengewa hizi Mahakama, wilaya 42. Kwa hiyo kwa wakati huu katika wilaya 139 tulizokuwa nazo, wilaya 136 tayari zina majengo ya Mahakama. Mahakama ambazo zimebaki na ambazo zipo katika mpango unaofuata wa ujenzi ni pamoja na Wilaya ya Mkalama, Chamwino na Ikungi. Hizi ndizo wilaya tatu ambazo zimebakia hazina majengo ya Mahakama za Wilaya na zitakuja kujengewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Mahakama za Mwanzo kwenye mpango huu zimejengwa Mahakama za mwanzo 72. Ninatambua kuwa Waheshimiwa Wabunge wana uhitaji bado wa Mahakama za Mwanzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyofahamu tuna kata 3,956 na Mahakama za Mwanzo tulizokuwa nazo kwa wakati huu ni 960, hivyo bado kuna uhitaji wa Mahakama za Mwanzo katika kata 2,996. Ninaomba kuwataarifu Waheshimiwa Wabunge kwamba mkakati wa Mahakama ni kuhakikisha katika mpango wa tatu wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya Mahakama, Mahakama hizi zitajengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama hizi zitajengwa kwa ushirikiano kati ya Mahakama na Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI. Kwa hiyo siku ya tarehe 5 Aprili, 2026 tukiwa kwenye uzinduzi wa Jengo la Makao Makuu ya Mahakama (Judiciary Square), Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo kwetu. Alisema kwamba Wizara ya TAMISEMI, Mahakama pamoja na Wizara ya Katiba na Sheria tushirikiane kwa pamoja ili kuongeza kasi katika ujenzi wa Mahakama hizi za Mwanzo tukishirikiana na Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba dhamira ile ya Serikali ya kuendelea kufanya uwekezaji katika Mahakama na katika eneo hili la miundobinu ya Mahakama ipo; na tayari kuna hadi Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na ninaomba niwatambue kwa majina yao. Ninaomba kumtambua Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mheshimiwa Zainab Telak; Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mheshimiwa Mwanamvua Mrindoko; Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Charles Makongoro. Hawa wote tayari wameanza utekelezaji kwa kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama za Mwanzo. Kwa hiyo Mahakama hizi zitajengwa ili kuendelea kuboresha upatikanaji wa haki kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji huo wa shilingi bilioni 524.9 haujaishia kwenye upande wa miundombinu, kwa maana ya majengo pekee; yamefanyika mapinduzi makubwa ya kidijitali, kwa maana ya kutengeneza mifumo ya kidijitali kwa ajili ya upatikanaji wa haki; pamoja na kutumia teknolojia ya TEHAMA kurahisisha na kusogeza huduma za upatikanaji wa haki kwa wananchi. Sasa hivi katika Mahakama tuna mfumo ECMS ambapo mwananchi anaweza akaingia kwenye mfumo na akafungua shauri, akafuatilia shauri lake na akapata hadi hukumu kupitia mfumo huo. Haya ni mapinduzi makubwa kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna huduma ya Mahakama Mtandao ambapo Mtanzania anaweza akaingia kupitia mtandao huu, akahudhuria shauri lake. Haya ni mapinduzi makubwa sana. Tunaona kwenye upande huo huo wa mapinduzi kwenye mifumo ya kidijitali, Mahakama ina call center, kituo cha huduma kwa wateja, ambacho namba zake ni 0800750247.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtanzania anayehitaji mwongozo wa namna gani ya kupata haki zake katika mfumo wa Mahakama, anaweza akapiga namba hii na akapewa mwongozo sahihi wa taratibu za kufuata ili aweze kupata haki yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mfumo pia wa namba ya WhatsApp ambayo kwa kutumia teknolojia ya chatbot, roboti hili lina-chat na Watanzania, linawaelekeza mambo tofauti tofauti na namna gani ya kupata haki zao na taratibu za kufuata Mahakamani ili kupata haki zao. Hii ni kazi kubwa sana ambayo imefanyika katika Serikali ya Awamu ya Sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuhitimisha ninawaomba Waheshimiwa Wabunge watupitishie hii Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 ili twende tukaimarishe Sekta ya Sheria ili kuwezesha utekelezaji wa Dira ya 2050.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba Waheshimiwa Wabunge watupitishie bajeti hii ili twende tukaimarishe upatikanaji wa haki kwa wote kupitia mifumo jumuishi yenye ufanisi na inayofikika. Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge watupitishie bajeti hii ili tukajenge mazingira bora ya uwekezaji kwa maana katika kipindi hiki cha ushindani wa kimataifa wa uwekezaji tunatakiwa kulinda maslahi ya Taifa kupitia sheria madhubuti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba Waheshimiwa Wabunge watupitishie bajeti hii ili twende tukaimarishe utawala bora na uwajibikaji na kuhakikisha Taifa linaendelea kuwa na amani, usalama na utulivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)