Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
Ex-Officio
Constituent
None
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia neema ya uhai na leo tuko mbele ya Bunge lako Tukufu kwa ajili ya hoja hii ya Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee ninamshukuru Mheshimiwa Waziri kwa namna ambavyo anaiongoza Wizara ya Katiba na Sheria. Pia, ninamshukuru Naibu Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara na Watendaji Wakuu wote wa taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa kazi nzuri ambayo tunaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninazungumza tu kwa ujumla kwa kuwa Wajumbe wengi ambao wamechangia, walikuwa wanazungumzia kwa uzito wake umuhimu wa kurekebisha sheria ili ziweze kuendana na hali ya sasa, lakini ili ziweze kuendana na Dira ya 2050.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sisi sote tunakubali kwamba ili tuweze kutekeleza au kuyafikia malengo ya Dira yetu ya 2050, ni lazima tuhakikishe kwamba sheria zetu nazo tunazihuisha ili ziweze kuwa daraja la kutuwezesha kutufikisha katika malengo hayo tuliyojiwekea katika dira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii tumeianza kwa umakini mkubwa na kama wote tunavyofahamu, huu ndiyo mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa dira. Kwa hiyo, hakuna hata sheria moja ambayo haitapitiwa. Ninarudia tena, hakuna hata sheria moja ambayo itaacha kupitiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kwamba sheria hiyo inakuwa na ubora ule ambao unatarajiwa ili tuweze kutimiza malengo ya dira. Kwa hiyo, sheria zote zitaguswa na kwa mwaka huu wa kwanza tumeshazibainisha chache ambazo tumeanza kuzifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu tuliouweka na utaratibu uliopo sasa, ni kwamba sheria yoyote ile ambayo itakuwa inarekebishwa, ni lazima iwe zao la utafiti. Kwa sababu kwa kufanya hivyo ndiyo tutakuwa tunajijua kwamba tuko ndani ya mstari kuelekea Dira ya 2050 au tunakwenda nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana sasa hivi utaratibu ni kwamba sheria zozote ambazo zitakuwa zinapendekezwa kurekebishwa, ni lazima kwanza zikapitie kwenye Tume ya Kurekebisha Sheria ili waweze kuzichakata vizuri kupitia tafiti watakazokuwa wanazifanya na kwa kushirikisha wadau, ili tutakapotoka na sheria hiyo kuja kuileta Bungeni, basi ikaakisi yale malengo ya dira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaenda kuachana na ule utaratibu wa zamani ambapo tafiti zilikuwa hazifanyiki za kutosha na matokeo yake tukawa na sheria ambazo zinatuletea changamoto. Kwa hiyo, hilo ni jambo ambalo tunakwenda kulizingatia kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo, zikiwemo na sheria zile za uwekezaji na zote ambazo zimesemwa, hata na zile za ndoa. Nimemsikia mchangiaji aliyezungumzia Sheria ya Ndoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa hii Sheria ya Ndoa, sasa hivi tunaendelea na zoezi la kukamilisha maoni ya wananchi, ni lazima tuhakikishe kwamba tumepata maoni yote ya wananchi nchi nzima na tunakwenda vizuri ili tutakapokuja kufika mwisho tuhakikishe kwamba sheria hiyo imeakisi maoni ya wananchi vizuri na baadaye itakuja kuletwa katika Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tusubiri kazi hiyo inaendelea na inaendelea vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo mengine ambayo yametolewa tumeyapokea, kwa mchangiaji aliyezungumza suala la Law School, kwa maana ya kwamba umuhimu wa kuwa na matawi sehemu mbalimbali za nchi yetu ili kurahisisha ufikiwaji wa wanafunzi katika shule yetu hii ya sheria uwe rahisi. Hayo ni maoni mazuri na tumeyapokea na yatafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mapendekezo pia ya lile suala la exemption. Ninamtoa tu wasiwasi Mbunge kwamba, suala hili hukumu ya Mahakama ilishatoka na Serikali inaendelea na mchakato wa kufanya marekebisho ya sheria. Kwa hiyo, kwa kifupi tu ni kwamba hayo ndiyo mambo ambayo yalikuwa yanamhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na suala la Mheshimiwa Agnes Hokororo ambaye yeye alizungumzia suala la Sheria Ndogo kwamba zimekuwa nyingi, kwa hiyo suala zima la kutafsiri katika lugha ya Kiswahili liongezeke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokea ushauri huu, lakini hata hivyo utaratibu wa kufanya ufasiri wa sheria unatanguliwa na kufanyika kwa lile zoezi la urekebu. Kwa hiyo, kwa sasa Serikali inaendelea na zoezi la urekebu ambapo mpango ni kufanya urekebu wa Sheria Ndogo 1,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninarudia tena, mpango ni kufanya urekebu wa sheria 1,000 kwa mwaka, tukiamini kwamba kwa kasi hii tutaweza kuzifanyia urekebu sheria nyingi. Hata hivyo, ili kuongeza kasi ya kutafsiri sheria, Serikali sasa hivi tunajenga mfumo wa kielektroniki utakaorahisisha ufasiri wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge vile vile alizungumzia kwamba baada ya zoezi la ufasili wa sheria kuu kukamilika sheria hizo zitangazwe rasmi. Nimfahamishe tu kwamba baada ya zoezi hilo kukamilika sheria hizo zilitangazwa rasmi kwa mujibu wa taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao. Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imejipanga vizuri katika kuhakikisha kwamba tunarekebisha sheria zote kwa kadri tafiti zitakavyotupa taarifa na kuhakikisha kwamba sheria hizo zinaendana na malengo yaliyowekwa katika Dira yetu ya 2050.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kwa heshima na taadhima ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)