Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilosa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, URATIBU NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaungana na wale wote walionitangulia kumpongeza sana Waziri wa Katiba na Sheria kwa kuwasilisha hotuba nzuri sana ya bajeti. Hotuba ambayo imeeleza mafanikio ambayo yamepatikana, lakini inayoeleza pia mipango katika mwaka ujao wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaungana na wengine wote ambao wamemshukuru sana Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mambo makubwa ambayo ameyafanya katika sekta hii ya Katiba na Sheria katika muhula wa kwanza wa uongozi wake na sasa katika huu muhula wa pili wa uongozi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kilosa, ninapenda nimshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini pia na Mahakama ya Tanzania kwa kutujengea Mahakama mpya ya Wilaya na Mahakama ya Mwanzo kule Kilosa katika eneo la Kondoa, Kilosa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukija Kilosa pia kuna eneo la Kondoa. Mahakama ni nzuri sana na tunashukuru kwa kuzingatia maombi yetu ya kwamba mahakama ile ziwe mahakama mbili ndani ya mahakama moja yaani Mahakama ya Wilaya na Mahakama ya Mwanzo. Ninaamini kabisa tutapata pia msukumo wa kukamilisha Mahakama ya Mwanzo kule Magubike kwa ajili ya zile Kata Nane za juu za upande wa Tarafa ya Mabole.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama ili nimshukuru sana Mheshimiwa Nyamizi Mhoja, ambaye ametoa hoja nzuri sana kuhusu masuala yote yanayohusu watu wenye ulemavu ambayo yanaangukia katika Wizara yangu. Mchango wake ni mzuri, maoni yake ni mazuri na tutayazingatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sahihi kabisa kama alivyosema, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilisaini Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu Wenye Ulemavu wa Mwaka 2006, tarehe 30 Machi, 2007 na tukauridhia mkataba huo tarehe 10 Novemba, 2009.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda tu kumwarifu kwamba toka tulipojiunga katika mkataba huo, tumehudhuria mikutano yote ya mwaka inayohusu utekelezaji wa mkataba huu na mwaka huu Mkutano huo wa 19 utafanyika New York Marekani, Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, tarehe 9-11 Juni. Tanzania itawakilishwa na katika mkutano huo tutatoa pia taarifa ya utekelezaji wa mkataba huu hapa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo mengi ya kueleza ambayo yamefanyika chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo yameimarisha haki ya watu wenye ulemavu kwamba ni raia wa Tanzania wenye haki sawa na Watanzania wengine wote kwa mujibu wa Katiba, lakini pia kwa mujibu wa sheria ya watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninamhakikishia kabisa kwamba sasa tunakamilisha uandaaji wa taarifa ya utekelezaji wa mkataba huo na tutashukuru sana baada ya shughuli hizi za Bunge kuweza kuonana ili na yeye atupe mchango wake ili uwe sehemu ya taarifa ambayo tutaiwasilisha Umoja wa Mataifa mwezi Juni mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja ya Wizara ya Katiba na Sheria. (Makofi)