Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Edwin Enosy Swalle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara ya Katiba na Sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme mwanzoni kabisa kwamba nimeisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwa umakini mkubwa sana, page kwa page na nimevutiwa nayo sana. Baadhi ya mambo mahsusi ambayo Mheshimiwa Waziri ameyasema kwenye hotuba hii, ninaomba niyataje matatu: Moja, anasema Sekta ya Sheria ni mlinzi wa amani, utulivu na usalama wa nchi; Pili, anasema Sekta ya Sheria ni mlinzi wa uwekezaji nchini; na Tatu, anasema sheria siyo kikwazo bali ni daraja la maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtazamo huu wa hii Wizara unaonesha jinsi ambavyo hii Wizara wamejipanga kuwa sehemu ya kutekeleza Dira 2050. Mheshimiwa Waziri, Dkt. Juma Zuberi Homera, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara hii na Naibu wenu hongereni sana kwa kazi nzuri ya Wizara ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, baada ya kuwapongeza hivyo, ninaomba pia niwasemee kwa kifupi waajiri wangu toka Jimbo la Lupembe, wananchi wa Jimbo la Lupembe wanaishukuru sana Serikali kwa kupeleka Mahakama ya Mwanzo Tarafa ya Lupembe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, wananchi wangu wa Kata ya Mtwango, Kata ya Kichiwa, Ninga, Igongolo, Ikuna, wanaomba Mahakama ya Mwanzo pale Mtwango. Ninamwomba sana Waziri na ninajua Katibu Mkuu ananisikia, wananchi wa Kata hizi tano muhimu hawana Mahakama ya Mwanzo wanafuata mahakama Njombe mjini na Makambako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mahakama ya Mwanzo pale Mtwango ili tuweze kuendeleza ujenzi wa Mji wa Mtwango ambapo tayari kuna kituo cha afya na vitu vingine, tupate huduma ya haki ya sheria pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ninataka nichangie kuhusu eneo la mfumo wa Mahakama nchini. Kwanza kabisa, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Jaji Mkuu wa Tanzania, Mheshimiwa Masaju, kwa jinsi ambavyo amekuwa positive sana kwenye reforms za kisheria nchini, kama Wabunge tumekuwa tukimfuatilia namna ambavyo ana kiu ya kuona mabadiliko na mfumo wa sheria ukiwa rafiki kwa wananchi wa Tanzania. Tunamuunga mkono aendelee kuchapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa karibuni tumemsikia akisema kwamba ni muhimu mashauri mahakamani yakaisha kwa muda mfupi. Pia, amekuwa akisisitiza umuhimu wa Mahakama kuzingatia matumizi ya tamaduni na mila zetu kama Watanzania. Kama Waafrika, tunamuunga mkono na kwa hili aendelee kuchapa kazi. Pia, Mahakama nzima, majaji na Mahakimu wafuate aina hii ya mtazamo kwenye Mahakama yetu ili kutekeleza dira ya mwaka 2050.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kwenye mfumo wa Mahakama asubuhi imesemwa hapa na ninaunga mkono sana, kwamba Mabaraza ya Ardhi Nchini ni muhimu yakarudi kwenye mfumo rasmi wa mahakama yetu na sababu zipo kadhaa. Sababu ya kwanza, haya mabaraza yameshindwa kuleta tija iliyokusudiwa. Kwa sababu takwimu zinaonyesha 32% ni migogoro ya ardhi, maana yake dhumuni la haya mabaraza halijafikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya yako mbali sana na wananchi, kwa mfano, Mkoa wa Njombe, tunalo Baraza moja la Ardhi Mkoa mzima. Wananchi wa kule Madeke, umbali wa kilomita zaidi ya 120 wanafuata Baraza la Ardhi na Nyumba Wilayani Njombe. Barabara za matope, wananchi wa Ludewa na Wanging'ombe wanafuata Baraza Njombe Mjini. Kwa hiyo, yako mbali na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu Mabaraza haya pia yamelalamikiwa mara kadhaa kwa ajili ya kesi mbalimbali za wananchi kutofanyiwa kazi vizuri. Kubwa kuliko yote, ipo kanuni ya haki ya asili au tuseme natural justice, kwamba hapa nchini Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya yako chini ya Wizara ya Ardhi, lakini Wizara ya Ardhi ndiyo wanaopima ardhi, ndiyo wanaotoa hati. Sasa, haiwezekani ndani ya hii Wizara tena wakasimamia haya mabaraza. Kwa misingi ya rule against bias, jambo hili haliwezekani! Kwa hiyo ni muhimu haya mabaraza yakarudi kwenye mfumo wa Mahakama ili tutoe haki kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninataka pia nishauri. Kwa kuwa, tunazo Mahakama za Mwanzo nyingi nchini, ambazo kule chini wako Mahakimu wenye weledi wa degree, lakini pia tumeweka sheria Mawakili wanaruhusiwa kwenda Mahakama za Mwanzo, ninashauri Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, tuanze kuruhusu Mahakama za Mwanzo kusikiliza mashauri ya ardhi.


Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hizi Mahakama za Mwanzo ndiyo zipo karibu na wananchi na Mabaraza ya Ardhi ya Kata tumeshayaondolea mamlaka ya kuamua kesi za ardhi. Kwa hiyo, ni muhimu Mahakama za Mwanzo sasa zikaingia kwenye mfumo wa kusikiliza mashauri ya ardhi nchini ili kusudi mfumo huu uweze kwenda kwenye Mahakama ya Wilaya, Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, niseme kidogo hapa kuhusu Law School of Tanzania. Law School of Tanzania kama ambavyo imesemwa na wengi, iliundwa maalum kuzalisha wasomi wa sheria nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2025 Desemba, Law School au tuseme mawakili walioingia kwenye mfumo wetu wa uwakili walikuwa 774. Katika mawakili 774, mawakili 388 hawajapitia kusoma Law School darasani. Wamepata uwakili kwa njia ya kuomba nje ya kwenda kusoma Law School. Tafsiri yake ni nini? Kama utaratibu huu ukiendelea, tunaenda kuua Law School.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hii ni alert kwamba watu baada ya kuona Law School ni ngumu, wameamua kutanua goli waweze kufunga magoli kwa urahisi zaidi. Ninaomba Serikali ilete sheria Bungeni, tubadili hii sheria ili watu wakasome Law School tupate mawakili wenye viwango, wenye ubora watakaoweza kufaulu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kabisa, ninataka niseme kidogo sana hapa kuhusu uhuru wa Mahakama. Hapa ninaongelea mahsusi, uhuru wa Mahakama juu ya kuisaidia Mahakama iwe na uwezo wa kuamua mashauri bila kuwa na sheria ambazo zinailazimisha mahakama kutoa adhabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee ninarejea Sheria ya Makosa ya Kujamiiana. Sheria ambayo imelazimisha Mahakama za Tanzania kutoa adhabu kwa washtakiwa wanaotiwa hatiani, kumfunga mtu kifungo cha minimum miaka 30 kwenda juu. Maana yake nini? Hata kama Jaji au hakimu ataona kesi ingefaa kumpunguzia mfungwa adhabu, amefungwa mikono kwenye sheria. Ninaomba Serikali ifike wakati tutunge sheria kuisaidia Mahakama iwe huru kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kwa sababu hii bajeti ni nzuri, ninaiunga mkono kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)