Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Maryam Ussi Yahya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. MARYAM USSI YAHYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninachukua nafasi hii kushukuru kwa kunipa nafasi ya kuongea, lakini pia, kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia kuwepo hapa katika siku hii ya leo. Hakika yeye kwa rehema zake ndiyo tupo hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kwa kuipongeza Wizara, kwanza kwa mafanikio yao makubwa kwenye Mama Samia Legal Aid, lakini kabla ya hapo ninampongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Makatibu na watendaji wao wote. Kwa kupitia wao Wizara hii safari hii imeweza kupatiwa bajeti kubwa zaidi kulinganisha na bajeti za miaka iliyopita kwa sababu, imeonesha umahiri katika utendaji wake wa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijachangia ninagusia pia, asilimia kubwa ya watu 7,000,000 iliyofikiwa kwenye Mama Samia Legal Aid. Hiyo ni zaidi ya 10% ya statistics ya wananchi wote katika nchi yetu. Inamaanisha kwamba, Legal Aid imeingia mikoa mbalimbali katika nchi yetu na kutuletea tija katika mustakabali mzima wa kuwapatia wananchi haki katika maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo yote katika hii Mama Samia Legal Aid ninagusia vilevile 14% ambayo ilisemwa kwenye kuhakikisha inaondoa migogoro hasa kwa watoto. Wote tunatambua ya kwamba, watoto ndiyo waathirika wakubwa katika migogoro hasa ya ardhi, ya mirathi na ya ndoa. Kwa hiyo, ninategemea na ninaishauri Wizara katika kuhakikisha inatekeleza majukumu yake, basi iipe kipaumbele sekta ya watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ingawa ipo kwenye maendeleo ya jamii, lakini tunaona jinsi familia zinavyoanguka kwenye migogoro ya ndoa na ya mirathi, ndivyo tunavyopata watoto wa mitaani. Watoto wao hawawezi kwenda kuomba sheria katika vyombo vya sheria, wanawategemea wazazi au wasamaria wema. Kwa hiyo, ninaishauri Serikali katika eneo la utatuzi wa migogoro, basi sehemu ya watoto ipewe kipaumbele mwaka wa fedha ujao, tuje tuone asilimia hii imepanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hilo la utatuzi wa migogoro, katika ripoti ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri imeeleza ya kwamba, katika kipindi cha Julai, 2025 mpaka Machi, 2026 watoa huduma wa msaada wa kisheria 47 na wasaidizi wa kisheria 243 walisajiliwa, kama ongezeko la asilimia 6.2. Tunaelewa fika kwamba, katika nchi yetu Chuo cha Wanasheria cha Law School of Tanganyika kinatoa wahitimu wengi kila mwaka. Chuo kile kina cohort mbili kila mwaka ambayo inatoa wanafunzi zaidi ya mia na katika mwaka wanatoka mara mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba sasa Wizara pamoja na kwamba, ina-train watu kufanya kazi katika huu Mradi wa Mama Samia Legal Aid, lakini pia, iangalie kwa makini wanasheria wale ambao wana-graduate wanakaa zaidi ya miaka na miaka mitaani hawana ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ifikirie sasa katika miradi inavyochukua wafanyakazi kuwa-train, kuliko kupoteza fedha ku-train watu wengine ni bora wakawachukua wanasheria ambao wamemaliza, wana elimu ya juu na pia, wamefanya Law School.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ninaomba niongelee suala zima la utatuzi wa migogoro, hasa kwenye masuala ya pre-bargain. Pamoja na kwamba, tumeisifia Wizara na ni haki yake, inafanya kazi yake vizuri, lakini bado katika maeneo ya utatuzi wa migogoro, hasa kwenye maeneo ya pre-bargain, bado tunaona eneo hili ufanisi wake unasuasua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mhalifu yeyote ambaye amekubalika na mahakama kutoa pre-bargain, kuilipa fidia Serikali ni kwamba, zile fidia ni mapato ya Serikali ambayo yanaenda kuendeleza uchumi wetu wa nchi. Kuna maeneo mbalimbali hawa walipa fidia wamekubali kulipa fidia, lakini bado inatokea ukiritimba wa wao kucheleweshwa kutoa hizi fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pia, ninaiomba Wizara katika utendaji wao, basi wafikirie kuhakikisha wanaofanyiwa pre-bargain, hasa wale wafanyabiashara wakubwa, ambao wanatakiwa walipe fedha nyingi katika Serikali, wanalipa fedha hizo kwa muda mwafaka na siyo kucheleweshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja na ninashukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)