Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Ester Edwin Malleko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Katiba na Sheria. Ninaanza kwa kuipongeza Serikali chini ya Rais wetu makini kabisa, Mama Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Waziri na Naibu Waziri, ninampongeza pia, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, bila kumsahau Katibu Mkuu wa Wizara hii pamoja na watendaji wote kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakwenda moja kwa moja kwenye kuchangia katika Mama Samia Legal Aid Campaign. Kipekee sana ninachukua nafasi hii kumpongeza sana Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa maono makubwa ya kuanzisha na kutekeleza Mradi huu wa Msaada wa Kisheria unaojulikana kama Mama Samia Legal Aid Campaign.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msaada huu wa kisheria umeleta mapinduzi makubwa sana katika upatikanaji wa haki nchini. Msaada huu umeweza kuleta haki karibu na wananchi, umeweza kupunguza migogoro iliyokuwa inatokana na masuala mbalimbali, ambayo yalikuwa hayawezi kupatiwa ufumbuzi, lakini pia, imeweza kuimarisha utawala wa sheria hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Kampeni ya Mama Samia Legal Aid, wameweza kuwafikia wananchi 7,462,387. Kipekee ninaipongeza sana Wizara, hawa ni watu wengi, wameweza kufikiwa kwa muda mchache kwa sababu, kazi hii imeanza Julai, 2025 mpaka leo Machi, 2026 wamewafikia watu hao, zaidi ya milioni saba. Tunaipongeza sana Wizara kwa kazi kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Mama Samia Legal Aid Campaign wameweza kupokea zaidi ya migogoro 5,209 ambapo migogoro 2,545 tayari imehitimishwa, kwamba, tayari imetatuliwa, imebaki migogoro 2,664 ambayo iko katika hatua mbalimbali kwenye vyombo vya maamuzi. Ninaipongeza sana Wizara kwa kazi hii kubwa iliyofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia katika migogoro ambayo imetatuliwa na kampeni hii ya Mama Samia, 32% ni migogoro ya ardhi. Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, asilimia kubwa ya migogoro ya ardhi inawatesa wananchi wetu kwa kiasi kikubwa sana, lakini ukiangalia migogoro hii inachangiwa kwa kiasi kikubwa na mfumo wa utatuzi wa migogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Wizara hii, ione ni namna gani inaweza kuhamisha Baraza la Ardhi lirudi Mahakamani, ili liweze kufanya kazi hii kwa umakini zaidi kwa sababu, tunaona mpaka sasa kazi haiwezi kufanyika kwa sababu ya ukwamishaji unaotokana na mabaraza haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kuipongeza sana Wizara hii, kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aid wameweza kufikia madai ya matunzo ya watoto kwa 14% katika migogoro waliyoipokea. Sisi wote ni mashahidi, kupitia migogoro ya ndoa watoto walikuwa wanakosa haki zao, lakini kupitia kampeni hii watoto sasa wanapata haki zao za msingi, wazazi wanajua wajibu wao na sisi tunaenda kujenga Taifa imara linalojali watu wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa pongezi kubwa sana kwa kazi hii iliyofanyika. Wamefikia 13% ya migogoro ya ndoa, ambayo ni changamoto kubwa sana kwa masuala ya ndoa ambayo yanaenda kupeleka matatizo mengi yanayoaenda kuleta migogoro ya kifamilia. Wamefikia pia, kwenye mirathi kwa asilimia nane, ukatili wa kijinsia asilimia nne, masuala ya jinai asilimia tatu, ajira asilimia tatu na masuala mengine asilimia nane. Tunawapongeza sana kwa kazi kubwa waliyoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipopongeza maono mazuri waliyokuja nayo Wizara hii. Kupitia ile kampeni ya 'Sema na Waziri' inaweza kuwafikia wananchi wengi, wanaweza kupiga simu na kueleza matatizo yao na baadhi ya matatizo yanatatuliwa wakati huo huo. Hii inaendelea kuongeza ufanisi katika Wizara yetu, ninapongeza sana ubunifu huo na tuendelee kuona namna gani tunaweza kufanya kazi hii kwa muda mwingi zaidi, ili migogoro mingi zaidi iweze kutatuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna faida kubwa sana kupitia Mama Samia Legal Aid Campaign, wananchi wengi wanapata ushauri wa kisheria bure. Tukumbuke kwamba, kuna wale wananchi ambao hawakuwa na uwezo wa kwenda kuweka mawakili, walikuwa wanapoteza haki zao, lakini wengine walikuwa wanashindwa kulipa gharama hizo na mwisho wa siku wanapoteza haki zao. Kupitia kampeni hii wameweza kupatiwa msaada wa kisheria, zaidi migogoro imetatuliwa, maridhiano yamepatikana, watu wanaelewana na haki inatendeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke pia, Mama Samia Legal Aid Campaign imepunguza kwa kiasi kikubwa sana idadi ya kesi Mahakamani.

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa kwa mchango wako. Muda wako umekwisha.

MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)