Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tanga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KASSIMU A. MBARAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani sana. Kwanza kabisa ninamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia sote kuwemo humu tena na kuendelea kulitumikia Taifa katika hili Bunge Tukufu, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nikushukuru wewe kwa kunipa fursa hii na nafasi hii ya kuweza kuchangia katika suala zima la msingi linalohusiana na masuala ya Wizara ya Katiba na Sheria katika siku hii ya leo. Pia, nitumie fursa hii kumpongeza kwa kiwango cha hali ya juu Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria, Naibu wake, wasaidizi wao wote pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kazi kubwa wanayoifanya ndani ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote ni mashahidi na sote tunafahamu na tunaona namna wanavyoratibu mambo na namna yanavyokwenda hususani kuhusiana na kliniki mbalimbali za misaada ya kisheria hususani ile Samia Legal Aid ambayo inafanya kazi vizuri sana kwa kiwango cha hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijikite katika mchango wa msingi kabisa na umuhimu kwenye masuala ya kisheria. Jambo la msingi kubwa zaidi ni kwamba kuna madai mengi sana ambayo yanakuwepo Mahakamani na yanachelewa sana kupatiwa ufumbuzi kwa muda mrefu sana kiasi ambacho yanaathiri miradi mingi sana ya maendeleo katika jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, imefika mahali wakati mwingine kama imekuwa sehemu ya Mahakama ya watu kufanya kitu kitaalam, tunakiita technical delaying, yaani kuchelewesha mambo kwa ajili ya faida binafsi au kwa ajili ya maslahi yao binafsi. Nitatoa mfano katika jambo ambalo limetokea katika Jimbo letu la Tanga Mjini. Hapa nitafanya reference kidogo ya land case namba tatu ya mwaka 2021 ndani ya Jimbo la Tanga Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale pana hospitali ambayo ni binafsi, ilianza kuwa dispensary ikaja mpaka ikafikia hatua ya kuwa hospitali. Inafanya kazi kubwa sana na kusaidia watu wa Tanga, lakini ukatokea mgogoro baina ya wamiliki pamoja na watu ambao ni wawekezaji katika lile eneo. Kesi ile imekwenda mpaka leo ni mwaka 2026 bado haijatoka Mahakamani na shauri lile halijakwisha, imekuwa ikiisha ikikatiwa rufaa, imebakia katika hali hiyo. Nini kilichotokea sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea...
MWENYEKITI: Mheshimiwa kwa mujibu wa Kanuni zetu kama kuna kesi iko Mahakamani inaendelea, haturuhusiwi kuijadili humu ndani.
MHE. KASSIMU A. MBARAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunifahamisha na kunielimisha kwa hilo. Kutokana na hilo naendelea, nukta nyingine ya msingi ya pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza Wizara ya Sheria na Katiba kwa kuonesha na kudadavua vizuri sana katika randama yao, hususan, kuonesha suala zima la elimu ya kisheria. Nimeona pale kwamba, kuna mchakato mzima wa kuingiza masuala ya elimu ya kisheria VETA, hali kadhalika mchakato mzima wa kuingiza kwenye mtaala elimu ya kisheria, hususan kwenye Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni mambo ambayo Wizara inayachopeka kule ni ya msingi sana kwa sababu, migogoro yote tunayoiona kwenye jamii inatokana na Watanzania walio wengi sana katika masuala mbalimbali kutokufahamu vizuri sheria za nchi hii, ambalo ni tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili ninawapongeza sana, wamefanya jambo kubwa sana la kimageuzi na kimabadiliko na liende katika vyuo vyote nchini Tanzania. Kila kijana anayehitimu walau ngazi ya diploma aelewe sheria za msingi za nchi hii, aelewe Katiba ya Nchi yetu, aelewe sheria za mambo ya ardhi na umiliki wa ardhi. Itasaidia sana kutatua migogoro mingi hapo baadaye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha hilo kuna suala la Katiba Mpya. Ninaipongeza sana Wizara ya Katiba na Sheria, jambo hili limekuwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambapo tumelinadi sana Wabunge wote Mwaka 2025 mpaka 2030 katika kipindi hiki. Nimeona tayari mchakato na utaratibu umeanza kupitia Wizara yetu ya Katiba na Sheria kwamba, jambo hili tayari limeshawekwa Mezani na mchakato umeanza kwa kuanza kushirikisha wadau na kuandaliwa taratibu zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ninapongeza na ni jambo kubwa sana kwa sababu, mabadiliko ya Katiba ni jambo la kitaifa na linatuhusu sisi sote. Wakati umekwenda sana, muda umesogea, mazingira yamebadilika, jamii tuliyonayo ni changamani sana, tunahitaji zaidi kuliangalia hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza walioliweka kwenye ilani, hali kadhalika ninaipongeza Wizara ya Sheria na Katiba, kwa mara nyingine tena, kuliona hili na kuanza kuchukua hatua mapema na kufanyia kazi utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ninachangia kwa kusema, Samia Legal Aid, msaada ule wa kisheria ni jambo kubwa na adhimu sana, linawasaidia watu wengi sana ndani ya Taifa hili. Tumeona kliniki ile ikifanyika, sasa ninashauri msaada ule, wale mawakili 171 wa kujitegemea ambao Wizara ya Katiba na Sheria inawatumia kati ya mawakili wengi wa Serikali walionao, sasa uende magerezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kuna watuhumiwa wengi, wako mahabusu, wasikilizwe na wayasimamie mashauri yao mahakamani, wenye hatia wapate hatia, ambao hawana hatia watoke waungane na ndugu zao. Hii itasaidia sana iwapo Samia Legal Aid itafika magerezani na kusikiliza wafungwa mbalimbali ambao hawana msaada wa kisheria kuweza kuwasaidia katika hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya ninasema ninashukuru sana kwa siku ya leo nami kuweka mchango wangu kwenye randama hii ya Wizara, hoja hii ya Wizara ya Katiba na Sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ninaunga mkono hoja. (Makofi)