Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Neema Peter Majule

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi hii ya kuchangia katika Wizara hii ya Katiba na Sheria. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa nafasi hii ya kufika mahali hapa na pia ninaomba niweze kuipongeza sana Wizara hii ya Katiba na Sheria kwa kazi kubwa ambayo wanafanya. Ni chombo ambacho tunakitegema Watanzania wote cha kutunza haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Waziri Dkt. Juma na pia nimpongeze Naibu Waziri mwanangu Zainab kwa kazi kubwa anazofanya. Ninampongeza Katibu Mkuu; ninawapongeza watendaji wote wa vitengo vyote vya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo kwenye Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria, tulifanikiwa kutembelea hata miradi ambayo wanaifanya, ni kazi nzuri sana ambayo imefanyika. Hivyo, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea sana, ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye kwa kweli ameongoza nchi hii kwa kufuata Katiba na sheria, ndiyo maana tuna hii amani na utulivu. Si hivyo tu, ameiwezesha Wizara hii kufanya kazi yake kwa kuruhusu hela za kutosha kwenda kwenye Wizara hii. Kongole nyingi sana kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu ya kwamba chombo hiki sasa ni chombo ambacho sisi Watanzania wote tunakitegemea kwa ajili ya haki hasa tunapoongelea habari ya Mahakama. Hivyo, tuna matarajio makubwa, Watanzania wana matarajio makubwa ndiyo maana Wabunge hapo wakisimama wanasema juu ya sheria mbalimbali ambazo zinabidi zibadilike ili ziweze kwenda sawa na wakati huu tulionao. Ninaamini kwamba Waziri Juma atakuwa anasikia jambo hili na atakwenda kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba Wizara hii ya Katiba na Sheria imefanya jambo zuri sana hasa ile Kampeni ya Mama Samia Legal Aid ambayo imesaidia Watanzania wengi. Tumeona wamewafikia karibu Watanzania milioni 7.4, lakini wanaume wakiwa milioni 3.6 na wanawake wakiwa milioni 3.8. Ina maana Watanzania wengi wamenufaika na hii kampeni. Niombe tu kwamba iendelee, imekuwa faraja kubwa. Watu walikuwa na matatizo, lakini hawana fedha za kulipia mambo ya sheria. Sasa tuna huduma ya Miswada ya Sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme tu na sisi UWT tuna Kamati ambayo pia ina wanasheria wabobezi ambao pia wanasaidia wanawake katika mambo haya ya msaada wa kisheria. Tume-copy na ku-paste, lakini inasaidia. Kwa hiyo, moja kwa moja tunaunga mkono jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo labda inabidi sasa tuweze kuona ambayo yanaweza yakakinzana kidogo na huu msaada wa kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba, mambo ya rushwa bado yapo ambayo yanaweza yakawa yanasumbua katika suala hili nayo tuyaangalie tuweze kudhibiti jinsi tunavyoweza.


Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu kuna gharama zingine ambazo mtu ambaye amepewa msaada wa kisheria, gharama kama za usafiri na accommodation. Yaani gharama nyingine ambazo zinaweza zikawa mzigo kwa mtu japokuwa amepewa msaada wa kisheria, lakini bado gharama zingine ambata zikawa kikwazo kwake. Wizara pia ipanue, inaweza kuwa hata na Mfuko tu maalum kwa ajili ya kuwasaidia hao watu ambao wanawapatia msaada wa kisheria, lakini pia wapate na misaada mingine ya kujikimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni ucheleweshwaji wa kesi. Kesi zikiwa za muda mrefu sana, mtu anahangaika hata kama ana msaada, anahangaika hizo gharama, anasubiri kesi ni ya muda mrefu, inamaliza mwaka na inaanza mwaka mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema watu wanakata tamaa njiani kabla hawajapata hiyo haki yao, hata kama wana msaada wa kisheria. Hivyo, kesi ziwe zina muda mfupi, ziweze kumaliza kwa wakati ili huyu sasa aweze kufaidi huo msaada wa kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni mambo ya ubambikizwaji wa kesi. Kuna kesi zingine zinabambikizwa, watu wanalalamikia mambo kama haya. Hivyo basi, Wizara au Mahakama pia iweze kuona vitu kama hivyo. Yaani kweli unasikiliza, unasema kweli hivi huyu mtu anaweza akafanya hivi? Unatumia na vyanzo vingine, hata vyanzo vya kisaikolojia kwamba kitu hiki ninafikiri huyu mtu…; kwa hiyo, yapo mazingira ambayo yanaweza kuonesha kuwa huyu mtu amebambikizwa kesi ili pia tuweze kuwa sasa na huduma nzuri ya msaada wa kisheria, lakini haya mambo mengine manne ni muhimu pia kuyaangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ninaomba kuchangia ni mambo ya RITA. Kwa kweli RITA ni chombo muhimu ambacho kinatupa sisi vyeti vya kuzaliwa na vifo, lakini kuna shida kwenye RITA. RITA inabidi sasa hivi nayo ijirekebishe ili iweze kuwasaidia watu. Wanafunzi, mtu amefiwa na wazazi wote anaambiwa ukalete cheti cha kifo.


Mheshimiwa Mwenyekiti, muda mrefu anapokwenda kutumia kutafuta cheti cha kifo cha wazazi wake, kwanza ana machungu yeye kuwa yatima, RITA iwe na kitu angalu kirafiki angalau cha kuweza kutoa huduma haraka kwa watu ambao wana maumivu. Pamoja na wajane, amefiwa na mume huku anaenda kutafuta mambo ya cheti, pia ni shida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu RITA inabidi pia ibadilishe mambo. Zaidi ya kutumia zile kanuni walizonazo RITA iwaangalie...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa
muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante kwa mchango wako. Muda wako umekwisha.

MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaomba kuunga hoja mkono. (Makofi)