Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Bahati Keneth Ndingo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mbarali

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Nami niungane na wenzangu kuipongeza Wizara chini ya Mheshimiwa Waziri Dkt. Juma Zuberi Homera, lakini na msaidizi wake Mheshimiwa Zainab Katimba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nimpongeze Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kaka yetu Mheshimiwa Hamza Johari kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Nianze kwa kuipongeza Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na kilikuwa kilio kikubwa cha Waheshimiwa Wabunge kwa Bunge la Kumi na Mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaambiwa sasa Wizara hivi karibuni watakwenda kuzindua mpango wa kuanza kutumia sheria zetu kwa lugha ya Kiswahili. Hiki kilikuwa ni kilio cha Wabunge wengi kuona tafsiri ya sheria hizi kwa lugha ambayo wananchi wengi wataelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tuna furahi kuona hatua kubwa ambayo imepigwa na itawasaidia wananchi wetu wengi kutafsiri vizuri sheria na itawasaidia katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, tunaishukuru na kuipongeza sana Serikali kwa hatua hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu vilevile kuishukuru Serikali kwa program mbalimbali zilizopo chini ya Wizara hii ikiwepo hiyo ya Samia Legal Aids ambayo imewafikia wananchi wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri hii kampeni iendelee na iwafikie na wananchi huko ndani vijijini kabisa ili waweze kupata msaada wa kisheria. Hata ile kampeni yako ya ‘Ongea na Waziri’ kwa kweli watu wanaifurahia sana. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri ikiwezekana aongeze muda kabisa ili wananchi wengi waweze kufikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri wa mambo machache kabisa kwenye Wizara hii. Tunatambua kama Taifa sasa hivi tunakwenda kwenye utekelezaji wa Dira ya 2050 na kiukweli katika Dira ile ili kuweza kutekelezeka tunaambiwa 70% ya mafanikio ya Dira yetu ile yatategemea sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, tumekuwa na sheria nyingi ambazo zinalalamikiwa na sekta binafsi. Nichukue nafasi hii kumwomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lakini vilevile na Tume yetu ya Kurekebisha Sheria, tunatarajia Bunge hili tuone sheria nyingi zikija Bungeni kwa ajili ya marekebisho. Sheria za uwekezaji bado zinapigiwa kelele, milolongo ni mirefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo vilevile sheria za fidia. Leo hii mwananchi akipigiwa fidia, Serikali inapotaka kutwaa (kuchukua) maeneo kwa wananchi, mwananchi akishalipwa fidia hata robo ya mali alizorudisha Serikalini hawezi kwenda kununua. Hebu tupate sheria ambazo zinaendana na wakati wa bei halisi zilizopo, lakini tuendane na wakati kama ilivyo dira yetu, tunasema tunakwenda kwenye uchumi jumuishi, hatuwezi kuwa na sheria ambazo bado zinawakandamiza wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali, acha alama kaka yangu Hamza kwa kutuleta sheria nyingi ambazo zitabadilika kuendana na wakati. Tunahitaji kuona Bunge hili likileta sheria za kuwalinda wafugaji. Wapo wengine ambao kweli wanafanya makusudi kuingia huko hifadhini, wapo wale ambao ng’ombe wanaingia kwa bahati mbaya, leo wanaenda kutaifishwa ng’ombe wao. Kila ng’ombe mmoja shilingi 100,000, hii ni gharama kubwa sana. Tuwaombe wawasaidie wananchi hawa tusiendelee kuwakandamiza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaungana pia kabisa na hoja ya Kamati ya Bajeti kwamba Mabaraza ya Ardhi yasiwe yanasikiliza kesi za ardhi. Kumekuwa kuna urasimu mkubwa, tunaomba mashauri yote ya ardhi yarudi kwenye Mahakama na haya mabaraza yasiendelee kwa sababu kuna malalamiko mengi ambayo yanawarudisha nyuma wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, niombe sana. ninasisitiza kwa Mwanasheria Mkuu wetu wa Serikali na Tume ya Kurekebisha sheria, niwaombe sana tunatarajia tupate mabadiliko mengi ya sheria ili kuendana na utekelezaji wa Dira ya 2050. Tunafahamu kwamba msingi ukiwekwa vizuri wa hii Dira na Dira hii wameibeba kwa sababu mambo mengi, vikwazo vingi vya kisheria vinatakiwa virekebishwe ili twende vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunatarajia tupate sheria nyingi na kama kuna mambo ambayo ni ya kisera hayajakaa vizuri, basi nayo yarekebishwe ili tuweze kupata sheria bora ambazo zitatupelekea msingi imara wa kutekeleza Dira ya Maendeleo 2050. Tusipofanya hivyo tutabaki kuwa na mipango mizuri aliyoiandaa Profesa Kitila Mkumbo na wenzake itabakia kwenye karatasi, lakini utekelezaji wake hautowezekana. Niombe sheria nyingi zinazolalamikiwa ziletwe Bungeni tuzirekebishe tuweke msingi mzuri wa kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)