Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Asha Ramadhani Baraka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ASHA R. BARAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa ninamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, pia ninawashukuru wote, Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Utamaduni na Michezo, ninamshukuru Waziri wa Elimu Profesa Mkenda na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Wanu Ameir. Mawaziri wetu kwenye Wizara hii wametupa mchango mkubwa sana, tumeongozana nao sisi Wajumbe wa Kamati na tumeona ufanyaji kazi wao ni wa hali ya juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia Chuo cha Usafirishaji - NIT halafu baadaye nitakwenda na VETA na nitakwenda na shule za primary. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara ya kwanza Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweza kusomesha marubani kwa mara ya kwanza pale chuo cha usafirishaji. Hawa marubani ambao tunategemea watakuwa wanarusha ndege zetu pamoja na Shirika la Ndege la Tanzania, lakini hapo nyuma marubani walikuwa wakisoma Nchi kama South Africa, Marekani, Uingereza na nchi nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu ni sikivu na imeangalia upande wa usafiri wa anga ikaamua kwamba waweze kusomesha marubani. Unajua kusomesha marubani nje ni gharama kubwa sana, lakini Serikali yetu ikafanya mchakato kwamba marubani wawe wanasoma hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitembelea kwenye kile chuo utakuta kuna ndege ziko pale, lakini ni ndege kwa ajili ya mafunzo. Kwa hiyo, marubani wanapata elimu na marubani hao tayari wameanza kurusha ndege. Tunaishukuru sana Wizara yetu ya Elimu kwa jambo hili ambalo ni kubwa sana kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakwenda kwa upande wa VETA, nimetembelea baadhi ya vyuo vya VETA. Ukiangalia vyuo vya VETA Serikali inategemea kujenga vyuo vya VETA Wilaya zote nchi nzima, lakini hivi ambavyo vimejengwa sasa hivi vinapokea watoto wetu vijana tofauti tofauti. Kuna vyuo vya VETA vinapokea watoto mpaka vijana wenye ulemavu, utakuta kijana mwenye ulemavu labda hana mikono kabisa, lakini anatafutiwa mafunzo ya kuendesha maisha yake na kuweza kujikimu yeye binafsi pamoja na familia yake. Kwa hiyo, ninatoa pongezi sana kwa Mawaziri wetu na ninatoa pongezi sana kwa Serikali yetu kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, ninataka kuongelea kuhusu watoto. Utakuta watoto wetu wanaosoma shule hizi za primary au shule za awali, wanaamka alfajiri saa 11.00. Mimi huwa ninapishana nao wakati ninaenda kufanya mazoezi. Utamkuta mtoto amebeba begi kubwa lina madaftari mengi halafu yuko peke yake, wakati mwingine unamkuta mtoto wa kike anatembea barabarani umbali mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda tu kuishauri Wizara ifanye mchakato, hawa watoto kama wanaingia darasani wawe wanabebeshwa madaftari ambayo wanatumia kwa siku hiyo hiyo kuogopa kwamba yule mtoto amebeba mzigo mkubwa mgongoni na unakuta labda anakaa Kinondoni, shule yake ya primary anaenda kusoma Temeke, mfano kwa Dar es Salaam, au kwa hapa Dodoma labda yuko Dodoma Mjini shule yake anayosoma ni Chamwino.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, unamkuta yule mtoto anatembea kwenda kungoja basi, akienda kungoja basi halafu anakuwa amechoka begi limemlemea kabisa huku mgongoni. Ninaomba tu Wizara ifanye mchakato kwamba wale watoto wawe wanasoma shule jirani na sehemu wanayokaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru sana Wizara ya Elimu kwa mambo makubwa ambayo wameyafanya katika nchi yetu kuhakikisha kwamba tunakuwa na elimu nzuri na bora zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja kwa siku ya leo, kwa jioni ya leo, ninawatakia Wabunge wenzangu wote jioni njema kwa sababu mimi ndiyo mchangiaji wa mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunisikiliza. (Makofi)