Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Selina Henry Kingalame

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. SELINA H. KINGALAME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia katika hii Wizara ya Elimu. Kwanza kabisa ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa uzima, afya na kibali. Pili, ninapenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mapinduzi makubwa ya sekta ya elimu, hasa elimu ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mradi Mkubwa wa HEET. Mradi huu ni wa miaka mitano, ulianza Mwaka 2021 mpaka Mwaka 2026. Mradi huu wa Dola za Kimarekani 425, unafanya mapinduzi makubwa sana katika marekebisho na ujenzi wa vyuo vikuu mbalimbali nchini Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipomshukuru tena Mheshimiwa Rais. Siku anahutubia Bunge hili la Kumi na Tatu alikuja na akasema azma ya Serikali ni kujenga matawi ya vyuo vikuu katika mikoa yote ya Tanzania. Sisi ni mashahidi, tunaona kabisa wameanza kwa ujenzi wa vyuo 16 kwenye mikoa mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichukue nafasi hii pia, kumpongeza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Profesa Mkenda. Hongera sana kwake, kazi yake tunaiona na ameonesha yeye siyo Waziri wa ofisini ni Waziri wa field. Hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii pia kumpongeza Naibu Waziri wa Elimu, hongera sana Mheshimiwa Wanu, kwani kazi yake tunaiona, ziara zake tunaziona. Nimekuwa mmoja wa watu ambaye ninapeleka kero nyingi sana na amekuwa akizitatua kwa wakati. Hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nijikite sasa kwenye mchango wangu, nitazungumzia vitu viwili. Kwanza ni udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu ni wazi kwamba, umeongezeka. Tukiangalia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 ambapo ni wanafunzi 137,000 na Mwaka wa Fedha 2025/2026 wanafunzi 170,000. Hii ni wazi kwamba, ongezeko hili la udahili kuna mazingira rafiki na mazuri katika vyuo vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ni moja, tunadahili wanafunzi hawa, lakini vyuo vingi havina uwezo wa kuwapa hosteli. Hii inasababisha wanakwenda kutafuta hosteli nje ya kampasi, ambapo sasa usalama wao na mali zao inakuwa ni changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu na ushauri kwa Serikali ni waangalie namna ambayo wanaweza kujenga hosteli maeneo ya vyuo. Kama maeneo ya vyuo siyo rafiki sana, labda ni madogo, waangalie ni namna gani ambavyo wanaweza wakatafuta maeneo mengine yakasimamiwa vizuri, ili vijana wetu wa vyuo na vyuo vikuu wawe salama. Pia, muda mwingine gharama za usafiri kutoka hosteli mpaka eneo la chuo imekuwa ni changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili ni Mikopo ya Elimu ya Juu. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ongezeko la bajeti ya mikopo mpaka kufikia shilingi bilioni 917. Ni ukweli usiyopingika, siyo wanafunzi wote ambao wanapata mkopo wanapata na ada pia, changamoto hii imekuwa ni kubwa sana kwa wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanafunzi inabidi atumie boom lake kulipia ada, ili asiweze kukosa masomo au mitihani yake. Ombi langu kwa Serikali, najua Serikali yangu ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni sikivu sana, lakini pia, nina imani kubwa sana na Waziri, baba yangu Mheshimiwa Profesa Mkenda, ukishirikiana na Naibu wako hakikisheni vijana hawa wanapata boom, basi wazingatiwe na ada pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo lazima wakapata asilimia yote mia, lakini angalau asilimia ambazo zitakuwa na unafuu kidogo, ili waondokane na hii adha ya kulipa ada. Nawahakikishia siyo kwamba, wataleta tu tabasamu kwa vijana hawa wa vyuo na vyuo vikuu, bali mtaleta utulivu wa nafsi na akili katika masomo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)