Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ZAINAB ABDALLAH ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii kuchangia Bajeti ya Wizara ya Elimu. Ninaanza na hadithi ya Mtume wetu Muhammad (SAW) ambayo alisema: “Twalabul 'ilmi fariidhatun 'alaa kulli Muslimin wa Muslimat” kwa maana kuitafuta elimu ni faradhi kwa kila Muislamu mwanamke na mwanaume. Pia, ukisoma Mithali 4:13 inasema: “Mkamate elimu usimwache aende zake, mshike kwa maana huo ndiyo uzima wako.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha huo ninachukua fursa hii kumpongeza sana Waziri wetu wa elimu Mheshimiwa Profesa Adolf Mkenda, mtu bingwa kabisa aliyefanya mageuzi makubwa sana kwenye sekta ya elimu nchini Tanzania na msaidizi wake Naibu Waziri Mheshimiwa Wanu Hafidh Ameir, mwanamke mchapakazi, mnyenyekevu, mtulivu, hodari, anayepambana kuhakikisha Sekta ya Elimu inapiga hatua kimaendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kuwaambia nchi hii katika Makatibu Wakuu waliowahi kutokea katika Wizara hii, ni Profesa Nombo. Huyu mama mpigie simu mpaka saa nane usiku, atapokea simu kuhakikisha anahudumia wananchi kwa masilahi mapana ya elimu ya Taifa hili. Profesa Nombo popote alipo apokee maua yake, Mwenyezi Mungu ambariki sana. Ninawapongeza Naibu Katibu Mkuu, Menejimenti ya Wizara na hapa wapo vijana wanaofanya kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda pale VETA, Mkurugenzi wa VETA CPA Anthony Kasore, kaka yangu apokee maua yake, VETA wanafanya kazi kubwa na kazi nzuri sana. Pia, tunampongeza Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania, Profesa Aneth Komba, hongera sana kwa mama yangu anafanya kazi kubwa sana. Ninaomba pia kumpongeza Katibu Mtendaji Mkuu wa Baraza la Mitihani la Taifa, Profesa Said Mohamed, hongera sana, anafanya kazi kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upekee Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), hongera sana kwao, tunatambua na kuthamini kazi yao. Tunataka kuwaambia, elimu ni ibada. Kama sisi hatutawapa malipo basi malipo watayakuta kwa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwa upekee kabisa kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye suluhu ya matatizo kwa Watanzania. Tumeona mageuzi makubwa sana aliyoyafanya kwenye sekta ya elimu. Kwenye historia ya nchi hii tumeenda kufanya maboresho ya Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 ambayo kwa sasa hivi elimu ya lazima itakuwa miaka 10 kwa maana kutoka darasa la kwanza mpaka kidato cha nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, KPI ya development index, moja ya maeneo ni literacy rate. Leo hii tunaenda kupata uhakika kwamba watoto wetu wote nchini Tanzania watafika kidato cha nne. Haya ni mageuzi makubwa na ya kuungwa mkono. Hongera sana kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amezindua Mpango Mkakati wa Kisayansi wa KKK, kwa maana sasa watoto wetu mpaka watakapofika darasa la tatu watakuwa wana uwezo wa kusoma, kuandika na kuhesabu. Haya ni mageuzi makubwa. Ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuja na mpango wa pamoja kati ya waajiri, vyuo vyetu vya ufundi stadi pamoja na vyuo vikuu ili kuhakikisha kwamba vijana wetu wanaokwenda kwenye elimu ya vitendo, wanapata ujuzi, wanapata uzoefu waende kupambana kwenye soko la ajira, hongera sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa kuliko yote, Mheshimiwa Dkt. Samia amefanya mageuzi makubwa kwenye miundombinu ya elimu. Kwa mfano, kwenye shule zetu za sekondari mwaka 2021 tulikuwa na shule 18,000, sasa hivi tuna shule 20,889, sawa na ongezeko la 11.2%. Kwenye elimu ya sekondari tulikuwa na shule 5,000 tu, sasa hivi tuna shule 6,488, sawa na ongezeko la 18.5%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa vyuo vikuu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mageuzi makubwa sana. Mwaka 2021 bajeti ya mikopo ya vyuo vikuu ilikuwa ni shilingi 700,000,000,000, leo ninavyozungumza hapa bajeti ya Vyuo Vikuu ni shilingi 839,000,000,000. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye historia ya nchi hii, Mheshimiwa Rais Samia anaweka rekodi kuwa Rais wa kwanza kutoa mikopo kwa vyuo vya kati, haijawahi kutokea kwenye historia ya nchi hii. Mwaka 2021 waliokuwa wanapata mikopo ya vyuo vya vya kati ni 10,200, sasa hivi wanaopata mikopo ni 18,473 kutoka shilingi 10,000,000,000 mpaka shilingi bilioni 18.7, nani kama Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa kuliko yote, kupitia uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia, sasa hivi tuna Samia scholarship ambazo zinawainua vijana wetu kwenye masomo ya sayansi kutoka wanafunzi 1,407 mpaka wanafunzi 2,630, sawa na ongezeko la 46.5%. Ametoa mikopo kutoka shilingi 7,000,000,000 mpaka shilingi bilioni 13.7% sawa na ongezeko la 40%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kumtia moyo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Madam President, thank you for promoting Educational Policies, thank you for strengthening Diplomacy, thank you for fighting up for this country, thank you for your untouched victory.
Sayyidat Raisat Samia anjariyatun wa hawiyatun wa mutawadhiatun, wa nastamirru bijiddatin. Nahnu nad’u jami’a al-mustathmirin, wa nad’u jami’a aswihab al-maslahat. Tanzania hiya mawtinuhum. Son excellence la Présidente Samia on lit les trés fort le trophe determinér visiyonner aujourd’hui nous a pris notre avertissements nous appelons touts les parties prénomes la Tanzanie votre maison moi je suis. Mheshimiwa Rais tuko pamoja na wewe, tunakuunga mkono na Mwenyezi Mungu atakulinda na kukubariki Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kumwambia Mheshimiwa Profesa Adolf Mkenda, Hayati Sheikh Abed Karume aliwahi kusema: “Huwezi kuwa mwana wa nchi kama huna uchungu na nchi yako.” Leo hii tuna kizazi cha Generation Z, asilimia kubwa ya watoto hawa hawana Uzalendo, hawana Utaifa. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Elimu, ipo haja ya ku-integrate elimu yetu na kuhakikisha vijana wetu…
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Zainab Issa kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Saashisha Mafuwe.
TAARIFA
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kumpa Taarifa dada yangu mpendwa na shemeji yangu kwamba Bunge letu tuna lugha mbili rasmi, Kiingereza na Kiswahili. Akitusaidia kurudia yale maneno aliyosema na sisi tuweze kuyaelewa tuweze kufurahia alichokuwa anakisema. Ahsante sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Zainab unaipokea Taarifa hiyo?
MHE. ZAINAB ABDALLAH ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeipokea lakini niliweka msisitizo ili ujumbe hii dunia ijue na Tanzania ijue kwamba tunaye daktari wa matatizo ya Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizia kwa kumwambia…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Zainab, kwa mujibu wa kanuni tuna hizo lugha mbili, sasa hicho ulichokisema ni kizuri sana. Ili tuweze kuwa na uelewa wa pamoja, utusaidie kututafsiria.
MHE. ZAINAB ABDALLAH ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuzungumza, nimewaambia Watanzania kwamba Mheshimiwa Rais wetu, kipenzi chetu sisi tunampenda sana, furaha yetu yeye mwenzetu hakika anapambana. Uchumi wetu, Diplomasia yetu imeimarika sana, Utalii wetu, vivutio vyetu dunia imeviona. Tunawakaribisha wawekezaji, wadau wote, karibuni tuijenge Tanzania yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuhitimisha, ninamwomba sana Mheshimiwa Profesa Adolf Mkenda, tunaenda kwenye kizazi cha Generation Z, pamoja na kwamba tunawekeza kwenye elimu na amali, kama hatujawekeza kwenye maadili, uzalendo na utaifa, bado tutakuwa hatujafikia malengo. Ninamwomba ashirikiane na wenzetu wa Jeshi la Kujenga Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya 60 na 70 wazee wetu wanajua, kwenda Jeshini ilikuwa siyo suala hiari, ilikuwa suala la lazima. Ipo haja ya watoto wetu kwenda kupata mafunzo ya ukakamavu na uzalendo ili wanapotoka kurudi uraiani, waweze kuwa na uzalendo wa kulipambania Taifa lao. Ninakuomba sana hili jambo lifungamanishwe na masuala ya uzalendo kwa kushirikiana na Jeshi la Kujenga Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. (Makofi)