Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi kuweza kuchangia Bajeti yetu ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Ninamshukuru sana Mungu kwa kunipa nafasi hii kuweza kushiriki tena hapa. Kabla sijasema lolote, ninaomba kumshukuru sana Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumwamini kaka yetu Mheshimiwa Profesa Mkenda na sisi watu wa Kilimanjaro. Niwaambie tu kaka yetu sisi tunamwamini na tunaendelea kumwombea amtumie kwenye mambo magumu kama haya kipindi ambacho tunafanya mabadiliko makubwa ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza pia wasaidizi wake Mheshimiwa Naibu Waziri, jirani yangu, dada yangu lakini pamoja na Katibu Mkuu Profesa Nombo na Naibu Makatibu Wakuu Hussein pamoja na ndugu yangu Mushi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kila sababu ya kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mambo makubwa aliyoyafanya kwa kipindi chake kwenye mabadiliko ya elimu. Itakumbukwa kipindi hiki cha Mheshimiwa Profesa Mkenda na Mheshimiwa Dkt. Samia na wasaidizi wake, yametokea mabadiliko mengi sana kwenye mfumo wetu wa elimu. Leo hapa tunavyozungumza, wanafunzi wa Kitanzania wamepata Samia Scholarship na tumewashuhudia pale. Haya ni mapinduzi makubwa sana, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi hii kubwa aliyoifanya kwa wanafunzi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yametokea mabadiliko ya kimfumo, kubadilisha mfumo wetu wa Elimu ya Awali. Leo tunazungumza Elimu ya Amali na Mafunzo na vyuo vinajengwa na wanafunzi wanapata taaluma, hayo ni mapinduzi makubwa sana. Hili kubwa ambalo Mheshimiwa Profesa Muhongo ameongea kwa undani sana sitarudia na mabadiliko kutoka kwenye mfumo wetu wa elimu kwa maana ya saba, nne mbili halafu three plus. Leo tuna Mfumo wa Elimu wa six kwa maana ya four, two na three plus, haya ni mapinduzi makubwa sana. Mheshimiwa Profesa Muhongo ameeleza nchi zilizofanikiwa kwenye mfumo huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, sasa ni wakati sahihi wa kwenda kubadilisha mawazo ya kwamba, ukimchukua mtu wa darasa la nane wakati wa Mkoloni na ukimchukua mwanafunzi wa Masters sasa hivi, yule wa Mkoloni anaonekana ni bora kuliko sisi. Kupitia mfumo huu ninaamini tunaenda kubadilisha mtazamo huo. Watoto wetu, wanafunzi wetu wawe na elimu ambayo akija mtaani, inapimika na inakuwa na ubora na ubora zaidi. Kwa mfumo huu, tunakwenda mahali, Profesa Mungu akubariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuzungumza kwa uchache tu kuhusiana na ujenzi wa Vyuo vya VETA. Ndugu yangu na kaka yangu Mheshimiwa Profesa Mkenda, Mama Samia amefanya kazi kubwa sana kwenye Jimbo la Hai na Wanahai wamenituma leo kumshukuru sana. Kule kwetu amejenga barabara, amejenga masoko. Sasa hivi ninamtaarifu Mheshimiwa Profesa Mkenda akiwa anaenda nyumbani, amwambie dereva wake akifika pale Hai tuna taa za kuongoza magari. Muda si mrefu ninaamini tutapata na flyovers. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili la VETA atakapoanza, Mheshimiwa Naibu Waziri ametuahidi hapa kufikia mwezi Desemba zitakuwa zimekamilika, ninakuomba sana uanze na Chuo cha Wilaya ya Hai kwa jirani zako. Pale tumekutengea eka 52, ukitaka kujenga Chuo cha VETA cha Kanda, njoo pale Hai tuna eneo la kutosha. Ninakukumbusha, Mheshimiwa Naibu Waziri alifanya ziara kutembelea Chuo cha Kikuletwa pale, ile barabara ya mkoa Mheshimiwa Naibu Waziri ninakumbuka alisema neno, akasema ninalichukua, ninapeleka kwa kaka yao Mheshimiwa Profesa Mkenda na mama yao Mheshimiwa Samia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile barabara ya kuelekea kwenye chuo siyo rafiki. Tumepata kilometa tatu lakini ninajua, wale waliotuwezesha kwenye kile chuo wanaweza kutusaidia Barabara ya Bomang’ombe – Chekimaji – TPC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kuzungumza jambo moja kuhusiana na watumishi wanaotoa elimu kwetu. Ninawashukuru sana walimu wa Tanzania. Profesa umeweza haya yote magumu, hebu ninaomba hili, Mheshimiwa Mama Sitta amekuwa akizungumza mara nyingi sana, sisi tuna Taasisi TSD inayohusika na walimu, kwa nini walimu wa nchi hii wanakuwa na mabosi kila mahali? Ninamwomba, kama ameweza la mitaala, hili aliweze, walimu wawe na msimamizi mmoja ili waweze kupata stahiki zao kwa wakati kama ilivyo Nchi ya Ghana na maeneo mengine. Yuko expert Mheshimiwa Mama Sitta pale, atamweleza kwa sababu ya muda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, ameeleza kwenye hotuba yake, vyuo vikuu vya nchi hii vinafanya utafiti ngazi ya Masters, ngazi ya PhD na ngazi nyingine. Wanaandika wanayajaza kwenye makabrasha ya vyuo vyetu vikuu. Ninaomba ifike mahali Profesa sasa, waanze kutumia tafiti zinazofanywa na wanafunzi wa vyuo vikuu, kuvileta viweze kuwasaidia Watanzania wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ninaomba kusema, nilisema wakati ninauliza swali hapa, liko jambo ambalo limeanza hivi karibuni kwamba Mhadhiri anayefundisha Chuo Kikuu kwenye kozi fulani, anatakiwa sifa za ajira yake ziwe specific kwenye eneo lile na nilitoa mfano kwenye kozi ya Political Science. Mhadhiri aliyesoma Political Science, anasoma International Relations, anasoma Public Relations, lakini inapofika kwenye kufundisha anakataliwa. Matokeo yake Chuo cha UDOM wamefunga baadhi ya kozi kwa sababu ya hilo tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Profesa hebu aingilie kwa haraka jambo hili, vinginevyo tutakosa kozi nyingi ambazo ni mahitaji. Ni sambamba na lile ambalo wanafunzi wanasoma kozi ambayo ukija mtaani, yes mwajiri namba moja tunaamini ni Serikali, ninaamini pia sekta binafsi, lakini huyu mwajiri namba moja kwa nini mtoto asome kozi ambayo akija mtaani, akiingia kwenye Sekretarieti, haipo. Nimefanya utafiti mdogo nikagundua, vyuo hivi vinafanya mawasiliano na Sekretarieti ya Ajira, lakini na Utumishi, kunakuwa na delay hapa katikati. Ninaomba Waziri atusaidie kuondoa hilo haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema kabla kengele ya kwanza haijalia, ninaomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, chondechonde hii Bajeti ya Elimu ni ya kimkakati, tunaomba fedha zote tunazozipitisha hapa ziletwe kwa 100% ili hii mipango iweze kutekelezeka. Tumeambiwa hapa 2028 watoto wetu wanaenda kuhitimu darasa la sita, lazima tuanze kuweka bajeti zinazotekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko jambo ambalo tunapanga mipango, tunashusha kwenye level ya halmashauri, tunasema halmashauri wakajenge madarasa. Halmashauri hizi ninaomba waziweke kwenye cluster. Halmashauri zina uwezo tofauti, huwezi kulinganisha Halmashauri ya Kinondoni na Halmashauri ya Wilaya ya Hai. Ukiwaambia hawa waende wajenge vyoo ndani ya miezi sita, hawa wakajenge madarasa, hili jambo hatutafanikiwa. Lazima tufanye tathmini ya mahitaji ya walimu wanaotakiwa, madarasa yanayotakiwa na vifaa vya kufundishia ili inapofika 2028, tuwe tumejiandaa lisiwe ni jambo ambalo limetokea kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla muda haujakwenda, sikupata nafasi ya kuchangia Wizara nyingi kidogo kwa sababu ya matatizo niliyokuwa nayo. Wanahai wameniambia Ndugu Chongolo ni rafiki yako, kule Hai alituahidi kutujengea Bwawa la Kilanya, ninaomba sana anisaidie kumkumbusha. Hata hivyo, alituambia atatueletea fedha kwa ajili ya Bwawa la Mbatakero kwa maana ya Skimu ya Umwagiliaji. Anisaidie kumkumbusha na zile za Metrom na Bolutu, haya ni mahitaji makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ni shida, tatizo la mbolea. Wakinisikia watu wa Hai nimesimama hapa sijazungumza mbolea, mbolea imekuwa ni changamoto kwenye wilaya yetu. Anisaidie kuongea na senior mwenziwe, amwambie tuna hiyo changamoto ya mbolea, watu hawapati mbolea, matokeo yake sasa hivi wamelima, mashamba mengi mbolea haijapatikana, achukue hatua za kidharura ili tuweze kupata mbolea kwa wakati na iuzwe kwa bei rafiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, anisaidie kumwambia Profesa hapo ambaye ni jirani yake kwamba, kule kwetu tuna shule chakavu, ninajua na Rombo zipo, tumeandika andiko maalum la Mkoa wa Kilimanjaro, tumeshawasilisha TAMISEMI, tunaomba watusaidie kuleta fedha hizi za shule chakavu ili na sisi tuondokane na shule ambazo hazifanani na sisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ninamshukuru sana, sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa heshima anayotupa katika Jimbo letu la Hai. Leo Jimbo la Hai ninapowaambia taa zinawaka barabarani, barabara zinapitika. Na yale machache yaliyokuwepo ambayo tunajua atayafanya, kwa kweli sisi tunaendelea kumwombea Mheshimiwa Rais, tunampenda sana na tunasema Mama Samia ni mama wa Hai, karibu sana Jimbo la Hai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)