Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Ado Shaibu Ado

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Tunduru Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango wangu kwenye bajeti ya Wizara ya Elimu. Ninaomba hoja zangu tatu za mwanzo ambazo nitazisema kwa muhtasari zielekezwe kwa mabosi wangu wananchi wa Tunduru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafanya hivi kwa sababu wananchi wa Tunduru wamenipa heshima kubwa sana na wanaendelea kunipa heshima kubwa sana kwa kuniunga mkono kisiasa na kuniamini. Kama inavyofahamika hakuna kitu azizi, hakuna kitu cha thamani kubwa ambacho mwanasiasa anapaswa kukipigania kwa nguvu zake zote isipokuwa imani ya umma. Kwa hiyo, hoja zangu tatu zitaelekezwa kwao kwa ajili ya kuilinda imani yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazitaja tu, Wanatunduru wamenituma jambo la kwanza, pale Tunduru tuna Mradi wa Ujenzi wa Chuo cha VETA; tulihoji hapa Bungeni, tunarudia tena Wanatunduru wanataka jibu, wanataka kauli ya Serikali ni lini watapata chuo kamili cha VETA cha Serikali? Ninataka kusema ninakubaliana na Kamati ya Bunge ya Elimu kwamba kama tunataka kuwakomboa vijana wetu, tuwekeze kwenye elimu ya ufundi. Hilo ni la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Wanatunduru wamenituma nikukumbushe kwamba wao walitoa ardhi yao, wakatoa na majengo yao, wakaikabidhi Wizara ya Elimu kupitia Chuo Kikuu cha SUA. Vitu hivi vina thamani inayofikia shilingi 1,000,000. Ahadi ya SUA ikawa watajenga kampasi kamili pale Tunduru ya Tawi la SUA. Hivi sasa tunahesabu miaka, tunaona wenzetu ambao hawajatoa chochote vyuo vinajengwa katika maeneo yao. Wanatunduru wamenituma nimhoji Waziri na kwa hili nitaishika shilingi yake mpaka watakapotueleza chuo kitajengwa lini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, wapiga kura wangu viziwi na hiki ni kilio cha viziwi wote Tanzania. Wamenituma nikueleze kwamba, wakati umefika kwa Lugha ya Alama kutambuliwa rasmi, kuwekewa kinga ya kisheria kama ambavyo Kenya lugha hiyo imo kwenye katiba yao na ifundishwe kwenye mitaala ya elimu katika nchi yetu. Hayo nimeyasema upesi ili kulinda imani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ninalotaka kulisema na hasa ikizingatiwa kwamba mengine yanayohusu elimu ya awali, ya msingi, ya sekondari na elimu ya vyuo vya kati yamepata mjadala mkubwa hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda nijielekeze kwenye ufanisi kwa elimu ya juu; nitarejea nyaraka ambayo Waziri na mimi tunafahamu, ninarejea azimio ama tamko la Kampala juu ya wajibu jamii pamoja na haki ama uhuru wa wanazuoni ama wana-academia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukilisoma azimio lile utakuta kwamba viko vipengele muhimu viwili vya kujipima. La kwanza ni lazima Serikali i-commit rasilimali kwa ajili ya elimu ya juu. Azimio lile linatamka hakuna ufanisi vyuo vikuu, hakuna uhuru vyuo vikuu kama Serikali haija-commit rasilimali za kutosha kwa ajili ya elimu ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Azimio la Kampala linasema lazima wanazuoni wafanye kazi kwa uhuru bila kutishwa, bila kuingiliwa, vipengele viwili na Waziri anafahamu, that was way back 1990. Tukifanya assessment leo kipengele cha rasilimali kwa maoni yangu, nikitazama hali ya wahadhiri wa vyuo vikuu, hitimisho langu kwa Waziri wa Elimu, tumewasahau, huo ndiyo ukweli wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitampa mifano michache Waziri, yeye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni nyumbani, aende nyumbani awatembelee ma-comrade wake majumbani, wako wahadhiri nyumba zao zinavuja na ushahidi upo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, atembelee madarasani akaone jinsi whiteboard zinavyobadilika kuwa blackboard. Atembelee maofisini University haina Wi-Fi, haina Wi-Fi ya uhakika. Zamani ilikuwa ukiwa mhadhiri ni jambo la fahari, leo hii hali ni ngumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pale nimefanya utafiti wahadhiri wanadai zaidi ya shilingi 6,000,000,000 za posho ya malazi kwa miaka minne mfululizo. Tutapata fahari ya wahadhiri wetu? Wanadai malimbikizo ya mishahara zaidi ya shilingi 1,000,000,000. Kuna fahari gani tena ya kuwa Profesa, ya kuwa daktari wa chuo kikuu? Hili la rasilimali bado tuna mlima mrefu wa kuukwea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipengele cha pili, uhuru. Kama tunataka kupata kilicho bora kutoka kwa Wanazuoni wetu, tuwaache wafanye kazi yao kwa uhuru na uhuru wa Mwanazuoni unaanzia katika chumba cha kufundishia, Mwanazuoni aachwe afanye kazi yake kwa uhuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viko visa kwa karibuni vya kuwatisha, vya kuwashughulikia Wanazuoni. Sina muda, Chuo Kikuu cha Dodoma yuko Mhadhiri ametoa maoni yake kwenye lecture, ameitwa Polisi na akawekewa dhamana na UDOMASA. Pale SUA iko mifano ya namna hiyo. Ushahidi upo, Iko mihadhara inashindwa kuendelea katika vyuo vikuu kwa sababu wanapata mbinyo wa Dola. Kama tunataka Wanazuoni wetu watupe matunda mazuri, tuwaache wafanye kazi kwa uhuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, ninashukuru sana na nimemaliza. (Makofi)