Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Paschal Inyasi Chinyele

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. PASCHAL I. CHINYELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa fursa hii. Ninaomba nichukue nafasi hii kwanza kuwapongeza Profesa. Mkenda pamoja na msaidizi wake, Wanu Ameir kwa bajeti hii nzuri waliyotuletea siku hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niongelee mambo mawili tu; la kwanza, nitaongelea kuhusiana na Bodi ya Mikopo. Tumeelezwa katika bajeti hii kwamba mwaka 2028 tutakuwa na vijana wa Form One ambao wanakaribia 3,000,000 wanaingia kwenye shule zetu. Hii maana yake nini? Kuanzia mwaka 2038 tutakuwa na waombaji wa mikopo wanaokaribia 1,000,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa, waombaji wa mikopo tunao kati ya 190,000 hadi 200,000 ambao ni wa mwaka wa kwanza. Kwa hiyo, hapa tunachokisoma ni kwamba Serikali yetu kupitia Wizara ya Elimu, ijipange sawasawa kufikia miaka ya 2038 na kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa bajeti iliyosomwa, pesa iliyopangwa kama nimesikia vizuri kwa mwaka huu ni shilingi bilioni 292, hivi imepangwa kwa ajili ya Bodi ya Mikopo. Sasa, ushauri wangu tu kwamba Serikali ijipange ifikapo miaka hiyo, ihakikishe kwamba Bodi ya Mikopo inakuwa na fedha ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikibidi, Bodi ya Mikopo ibadilishwe iwe kama Mfuko kama zilivyo NSSF au PSSSF, ziwe na fedha na zijendeshe ili kupata fedha nyingi. Ikiwezekana Serikali inaweza hata ikafanya tozo kwenye miamala ya simu kupata fedha za kutosha kwa ajili ya kugharamia elimu ya vijana wetu. Kwa sababu kwa suala la elimu na hasa hasa maamuzi haya mazito yaliyochukuliwa ya kuboresha mfumo wa elimu tutakuwa na wanafunzi wengi wanaotaka mikopo, almost a million au laki nane hivi. Sasa hivi tunahangaika na watoto 200,000 au 300,000. Je, itakuwaje mwaka 2038 na kuendelea?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri Serikali ianze kufikiria kutafuta fedha za kutosha kwa ajili ya kugharamia elimu ya vijana hawa, tunahangaika. Tumesikia kijana yule aliyekuwa analia mtaani amesaidiwa, hata hivyo, ninataka kuwahakikishia yule yule aliyesaidiwa hayuko peke yake. Wako wengine ambao vyombo vya habari havijawafikia, wanalia hawajapewa mikopo na wako mtaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ninaloomba kuchangia siku ya leo, katika ukurasa wa 97 wa kitabu cha bajeti, kimetajwa Chuo cha Ufundi cha Dodoma kinaitwa Dodoma Technical College. Chuo hiki kimejengwa katika eneo la Kata ya Mbalawala. Kama unakwenda Singida ukifika Nala upande wa kulia utaona kipo kinaonekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichukue nafasi hii kuwasilisha shukrani za wakazi wa Kata ya Mbalawala kwa ujenzi wa Chuo kile cha Ufundi, Polytechnic College, ambacho kimejengwa. Chuo kile kwa taratibu zilizowekwa na Mheshimiwa Waziri ni kwamba mwaka huu kitachukua watoto 1,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wale ni wengi kwa lile eneo na niseme tu kwamba eneo lile na hatua hii ya kujenga kile chuo inataka kufanana na mwaka 1970 pale Chuo cha Dar es Salaam kilipojengwa pale Ubungo. Wakati ule palikuwa ni pori hivi, kile chuo kikachechemua uchumi wa maeneo ya Msewe, Ubungo yenyewe, Sinza na maeneo ya Mlalakuwa yakawa ni maeneo ya miji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi pia panaenda sasa kuchangamka, maeneo ya jirani na Mbalawala, maeneo ya Chigongwe, maeneo ya Ilindi katika Wilaya ya Bahi na maeneo jirani yanakwenda sasa kupata uchumi. Ninachukua nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa maamuzi haya aliyoyafanya ya kuanza sasa kukifanya chuo hiki kianze kuchukua watoto na kuanza kutoa elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nisisitize tu kwamba chuo kile ni cha Watanzania na bado kuna miundombinu ambayo haijakamilika. Zinahitajika shilingi 3,000,000,000 ili chuo kile kianze kuchukua wanafunzi kuanzia mwaka huu wa masomo. Ni ombi langu kwa Serikali, Mheshimiwa Profesa Mkenda, ninaomba sana pesa inayotakiwa karibu shilingi 3,000,000,000 iweze kutolewa, kwa sababu mpaka sasa hivi miundombinu ya maji safi na majitaka bado haijakaa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana miundombinu hiyo ikae sawa ili mwezi wa kumi watoto waanze kuingia na kusoma pamoja na kupata ujuzi wa kusaidia nchi yetu, lakini pia chuo hiki kinaweza kuchechemua uchumi wa eneo lote la Jiji la Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)