Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuchangia bajeti ya Wizara ya Elimu. Kwanza, kabisa ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu muumba mbingu na dunia kwa kutujalia afya na leo hii tunachangia Wizara ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Profesa Mkenda, Waziri wa Elimu na Naibu wake Mheshimiwa Wanu kwa kazi nzuri ambazo wanazifanya kwenye Wizara hii ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda pia kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo amelichukulia kwa uzito suala la elimu nchini kwetu Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameweza kujenga madarasa ya kutosha kwenye Nchi yetu ya Tanzania. Pia, ameweza kujenga shule kwa watoto wa kike wasichana shule kwa ajili ya kusoma masomo ya sayansi. Hii ni hatua kubwa kwa watoto wa kike nchini kwetu Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sasa nijikite kwenye mchango wa Wizara ya Elimu. Niliwahi kusimama hapa tarehe 7 Mei, 2023 na tarehe 8 Aprili, 2026 na leo tarehe 7 Mei, 2026, nikisema kwamba kwenye Mkoa wangu wa Katavi tumeachwa nyuma kwa sababu mkoa una matatizo ya uhaba wa madarasa, madawati na matundu ya vyoo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nirudie takwimu ambazo nilizitaja humu Bungeni nilipochangia Wizara ya TAMISEMI. Mkoa wangu wa Katavi una upungufu wa madarasa 3,205, uhitaji wa madarasa 6,071, yaliyopo ni madarasa 2,866 tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wangu wa Katavi una upungufu wa madawati 27,348, ina uhitaji wa madawati 87,681 yaliyopo ni madawati 61,332. Mkoa wangu wa Katavi una upungufu wa matundu ya vyoo 5,360, unahitaji matundu ya choo 9,122 yaliyopo ni matundu ya vyoo 3,662.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nimetoa takwimu hizi? Nimeitoa takwimu hizi kwa kuwa tunakwenda sasa kwenye Elimu ya Msingi ya lazima ya madarasa kumi. Kwa maana kwamba darasa la kwanza mpaka la sita, tunakwenda sekondari madarasa manne. Sasa watoto watakuwa wanasoma madarasa 10. Kwa upungufu huu wa madarasa, madawati na matundu ya vyoo, Mkoa wangu wa Katavi utafikaje huko kwenye shule za msingi lazima miaka 10?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hivi kwa sababu Wizara ya Elimu ndiyo msimamizi wa sera, lakini mtekelezaji wa sera ni TAMISEMI. Hakuna connection, kutoka Wizara ya Elimu kwenda TAMISEMI kule kwenye halmashauri, kusimamia kuona vyoo vipo, madarasa yapo na matundu ya choo yapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali ijaribu kuliangalia hili kwa kuwa inapelekea sera TAMISEMI azitekeleze lakini haiwa-control hawa TAMISEMI kuhakikisha kwamba wanajenga hayo madarasa, wanatengeneza madawati na wanachimba hayo matundu ya vyoo. Nini maana yake? Maana yake ndiyo ukosefu wa matundu ya choo, madarasa na madawati kwenye Mkoa wangu wa Katavi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali ijaribu kuangalia, je, itaweka kanuni kwenye Wizara ya Elimu ambazo zitakuwa zina-foresee huku kwenye TAMISEMI? Kwa sababu Mkurugenzi anaripoti kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, haripoti kwa Waziri wa Elimu. Asipochimba choo, asipoongeza darasa, asipotengeneza dawati, Mheshimiwa Mkenda hawezi kumwajibisha yule Mkurugenzi. Maana yake nini? Maana yake sera zile ambazo Mheshimiwa Mkenda anazisimamia zinashindwa kutekelezwa huku chini na wale wanaozitekeleza hawako answerable kwa Mheshimiwa Mkenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizingatia mwaka 2028 tukijaliwa uhai tutakuwa na wanafunzi 21,177 ambao watakuwa wanakwenda kwenye shule za sekondari. Nini maana yake? Tutakuwa na wanafunzi ambao watakuwa wamefika darasa la sita wanahitaji kwenda sekondari, lakini tutakuwa na wanafunzi ambao wako darasa la saba ambao watakuwa wanakwenda pia sekondari. Jumla nchini kwetu Tanzania tutakuwa na wanafunzi 3,021,177 na tutahitaji madarasa 23,266, tutahitaji walimu 40,192, tutahitaji maabara 9,366 na tutahitaji matundu ya vyoo 46,632. Hizi ni takwimu zilizosomwa hapa na Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Wizara ya Elimu iweze kuangalia ni jinsi gani tutaweza kutekeleza hayo mambo. Kwa sababu ninavyoona kwenye Mkoa wangu wa Katavi, tunashukuru kweli Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais kweli imejenga madarasa, imetengeneza miundombinu lakini utekelezaji kwenye mkoa bado. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, sisi wananchi wa Mkoa wa Katavi watoto wetu watapataje hii Samia Scholarship? Leo hii umewaonyesha wanafunzi hapo kuna hii Samia Scholarship extended ambayo wanafunzi wanakwenda kusoma nje. Je, wale wanafunzi watoto wetu, lakini wajukuu zangu kule Katavi watapataje hii Samia Scholarship wakasome nje kama wanakaa chini? Darasa moja kwenye Mkoa wa Katavi wanakaa wanafunzi 200. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, nikitoa mfano, hata Mheshimiwa Waziri akituma mtu akaangalie, kuna shule pale Mpanda Mjini, Shule ya Msemulwa, watoto wanakaa darasani 200. Hawa watoto kutoka darasa la kwanza mpaka la tano wanakaa chini. Je, hii scholarship ya Mheshimiwa Rais, Mama Samia, ambaye ametupenda akatoa hiyo scholarship watoto wakasome nje, wale wajukuu zangu Mpanda wataipataje? Kama wanakaa chini kutoka darasa la kwanza mpaka la tano, wataipataje hii scholarship? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia pia watoto ambao wanakwenda kusoma gender equality walivyokuwa wanatambulishwa hapo, nimejaribu kuangalia gender nimekuta kuna wasichana wanne. Ninaomba hizi scholarship ambazo Mheshimiwa Rais ametoa zizingatie pia gender balance. Kama scholarship ziko 30, basi 15 wawe wasichana, 15 wawe wavulana ili tuweze kwenda sambamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumza leo ni lugha ya kufundishia. Mheshimiwa Profesa. Mkenda anafahamu kwamba, sera ya nchi yetu watoto wanafundishwa kwa Kiswahili kutoka darasa la kwanza mpaka la saba. Wanapokwenda sekondari ndiyo wanakwenda kupambana na Kiingereza. Yeye amesoma vizuri kwa kufundishwa na walimu wa zamani na ndiyo maana ame-excel mpaka akawa profesa wa kusoma darasani. Je, una utaratibu gani au tunawaangaliaje hawa watoto kuweka lugha ya kufundisha ya Kiingereza kutoka darasa la kwanza? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Muda wako umekwisha Mheshimiwa.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika moja. Kwa nini ninasema hivi? Ninasema hivi kwa sababu English is official language, but Swahili also is official language. Why don't we use two languages? Kwa sababu watoto wetu wanapokwenda kwenye interview nje ya Nchi ya Tanzania wana-feel inferiority mbele za watu kujitetea japo kile kitu wanakifahamu. Sisi sote humu ndani watoto wetu wamesoma English Medium.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba hili suala niliache hapo na nimwachie kama kitendawili Mheshimiwa Profesa Mkenda. Iko haja ya kuweka Kiingereza kufundishwa kutoka darasa la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)