Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Kassimu Amari Mbaraka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. KASSIMU A. MBARAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, shukran sana kwa kupata fursa hii nami kuchangia kwenye bajeti hii ya Wizara ya Elimu. Awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kutujalia kuwepo hapa Bungeni na kuendelea kulitumikia Taifa letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nukta ya pili ninapenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ndani ya Taifa letu la Tanzania kwenye kuisimamia na kuleta mageuzi makubwa chanya hususan mageuzi ya kielimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona miaka mingi sana tumepita na kauli mbalimbali za elimu, lakini leo ile azma ya kauli kubwa ya Taifa hili ya elimu ya kujitegemea inaenda kutimia kwa kuona mabadiliko makubwa yaliyofanyika kwenye mitaala ya elimu ambayo inawawezesha vijana kuhitimu kidato cha nne akiwa pia amehitimu masomo yanayosimamiwa na NACTVET na kuweza kupata cheti na kuingia kwenye soko la ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, atakuwa na ujuzi ndani ya umri mdogo au hata kuendelea katika vyuo vya kati na kuweza kupata elimu. Hili ni jambo kubwa sana kwa sababu soko la dunia ya leo linahitaji watu wenye ujuzi na si nadharia tena. Kwa hiyo, wataweza kushindana katika soko la ajira hapo baadaye. Hilo ni jambo kubwa sana. Tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa hiyo aliyoifanya kuisimamia mageuzi ya mitaala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Profesa Adolf Mkenda pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Naibu Waziri, Wanu Hafidh Ameir kwa kazi kubwa wanayoifanya kwenye Wizara hii ya Elimu pamoja na watendaji wao Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara ya Elimu. Kwa kweli wanafanya kazi kubwa sana kuisimamia maono mapana ya Taifa hili pamoja na maono mapana ambayo yamo katika Dira yetu ya 2050 kuhusiana na masuala elimu ndani ya Taifa letu la Tanzania. Ni jambo jema kabisa hilo na mambo yote yanakwenda vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuongea hayo kwa muhtasari sasa nijikite kwenye jambo la msingi. Ukichunguza zaidi utakuja kugundua kwamba Wizara ya Elimu 100% maisha yake inagusa maisha ya vijana wa Taifa la Tanzania na katika Taifa la Tanzania vijana katika population ni takriban 68% hadi 70%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii tafsiri yake ni nini? Tafsiri yake ni kwamba idadi ya ongezeko la watu inakua Tanzania, lakini ukiacha hivyo idadi ya vyuo vikuu vinaongezeka Tanzania. Maana yake ni nini? Ni lazima tujifunge mkanda vizuri kuhakikisha tunaihudumia vizuri elimu ya juu kupitia Higher Education Students’ Loan Board kwa kuhakikisha mikopo ya vyuo vikuu (elimu ya juu) na ya kati inayotolewa na Higher Education Students’ Loan Board inatoka kikamilifu na bajeti ile inatoka kama vile ilivyopitishwa na kuidhinishwa na Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatolea mfano, ukiangalia bajeti ya Mwaka wa Fedha 2023/2024, 2024/2025 na 2025/2026 kuna kitu utakigundua. Bajeti iliyoidhinishwa na Bunge katika jumla ya vipindi hivyo vitatu ni shilingi 2,442,851,755,519.98. Hii ndiyo bajeti iliyoidhinishwa kipindi cha Mwaka wa Fedha 2023/2024, 2024/2025 na 2025/2026. Iliidhinishwa hii iende kwenye Higher Education Students’ Loan Board, ifike pale watoto wale wakopeshwe, vijana wetu waweze kusoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiasi kilichopokelewa Loan Board ni shilingi 1,788,017,499,927.58. Hiyo ndiyo fedha ambayo imepokelewa takriban shilingi bilioni 654 na ushee bado haijapokelewa. Tafsiri yake ni nini? Ni kwamba kampasi zinaongezeka, kampasi zinakuwa nyingi zinazidi kutanuliwa, idadi ya enrolment inakua vyuo vikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba tunaishauri Serikali fedha tunazozipanga hapa Bungeni kuhusiana na Higher Education Student Loan Board na tunazoziidhinisha katika bajeti hii ikishapitishwa na Bunge Tukufu fedha hizo ziende kama zinavyohitajika. Watoto wetu wapate mikopo kwa sababu ukiangalia takwimu hii Bodi ya Mikopo inafanya kazi vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, takribani 70% ya pesa wanayotoa wanaikusanya takribani 70%. Afrika Mashariki, Afrika kwa ujumla na duniani ni moja katika organ muhimu na inafanya kazi vizuri sana. Kwa nini fedha hizi tusiziidhinishe zote zikafika zikapokelewa zikaingia kwenye matumizi vijana wetu wakapata elimu tukawa tunawasaidia kikubwa zaidi? Hilo ni jambo la msingi kwenye Higher Education Students’ Loan Board. Fedha tunazoidhinisha hapa Bungeni ziende Bodi ya Mikopo kama tulivyoidhinisha, vijana wa Tanzania wakanufaike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ninalotaka kuchangia ni kuhusiana na Wadhibiti Ubora. Ukiangalia wale Wadhibiti Ubora ni kama CAG katika elimu. Yaani ni wakaguzi ambao wao wanakagua masuala yote yanayohusiana na elimu ndani ya nchi ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hebu ifike mahali tuwaondoe kwenye Fungu 56 - TAMISEMI tuwapeleke kwenye Fungu 46 la Bajeti ya Wizara ya Elimu. Kwa nini ninasema hivyo? Mkurugenzi wa Halmashauri ndiye anasimamia karibu shule zote katika eneo lake. Mkurugenzi anaposimamia mwisho wa siku ndiye anayelipa ile capitation grant fee kwa ajili ya wale Wadhibiti Ubora kufanya kazi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa siku zote anayemlipa mpiga zumari ndiye anayechagua wimbo. Hii maana yake ni nini? Tuwafanye Wadhibiti Ubora wawe huru wafanye kazi zao vizuri. Wakipita kule wakiona hakuna madawati, hakuna miundombinu mizuri ya matundu ya choo au shule zina hali mbaya waweze kuandika ripoti na kushauri vizuri ili tuweze kupata matokeo bora kwenye shule zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachoshauri hawa moja kwa moja wasimamiwe na Wizara ya Elimu, TAMISEMI wasihusike nao. Malipo yao yote yatoke Wizara ya Elimu waje kwenye Fungu - 46 la bajeti. Hili ni jambo muhimu sana kwa sababu hili ndilo jicho letu katika majimbo ili wafanye kazi zao kiweledi na vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la msingi zaidi ni kuhusiana na suala zima la VETA. VETA ndiyo inajenga taswira kubwa ya kutengeneza ujuzi wa nchi hii, ndiyo masterplan ya ujuzi kwa vijana wetu ndani ya Taifa la Tanzania. Fedha zinazotengwa kwa ajili ya VETA zitoke, VETA zikatengenezwe zisimame ili vijana wetu waweze kuingia katika enrolment hiyo na kuweza kupata tija kubwa ya kupata ujuzi hapo baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka unaokuja mbeleni, darasa la sita wanamaliza, hali kadhalika wanamaliza na darasa la saba, kutakuwa na double cohort. Maana yake huko mbeleni kutakuwa na enrolment kubwa ya wanafunzi kuingia vyuo vya kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kinachohitajika? Kinachohitajika vyuo vya VETA vijengwe kwa haraka viwepo nchi nzima ili vijana hao waingie hapo waweze kupata ujuzi. Wakitoka pale wana ujuzi kamili wataweza kujiendeleza hapo baadaye katika shughuli zao mbalimbali za ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, VETA isiishie kujengwa, tuvilinde kwa thamani kubwa. Kwa nini tuvilinde kwa thamani kubwa? Nitatolea kesi moja ya Tanga. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Elimu. Tanga tuna Chuo cha VETA kizuri sana. Pale panatolewa mafunzo ya udereva (Passenger Service Vehicle) na HDV (Heavy Duty Vehicle). Palitokea kidogo purukushani lakini baada ya muda kuna mtu alitokea akalala, akaamka, akasema hii kozi nimeifuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Waziri wa Elimu, mtu bingwa kabisa, Profesa Mkenda. Nilikaa naye nikazungumza naye akamtoa Director wa VETA, akamtoa na Naibu Katibu Mkuu wa Elimu, waende Tanga. Leo hii Alhamdulillah Chuo cha VETA Tanga kinatarajia kurudisha kozi ya PSV na kozi ya HDV waweze kusoma pale VETA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, isiishie kuvijenga hivi vyuo tuvisimamie kwa ari kubwa na kuvitolea jicho. Ndivyo vilivyoshikilia mhimili wa vijana wa Tanzania. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ameweka mtazamo mkubwa sana kwenye suala la VETA kwa sababu ndipo ujuzi wa vijana wetu utapatikana hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo sasa nitoe pongezi zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Mradi wa HEET (Higher Education for Economic Transformation) na sisi Tanga tumenufaika kupitia Mzumbe University Mkinga Campus; mradi wa dola milioni saba. Haya ni mabadiliko makubwa na ni mageuzi makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niliambie Bunge hili Tukufu, Tanga ndio chemichemi ya elimu ya Taifa hili. Shule ya kwanza ya Msingi ilikuwa Magila na Shule ya kwanza ya sekondari ni Tanga. Sisi ndiyo watu wa mwanzo kusoma na kuwa na mwanga wa elimu. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ndani ya awamu yake kuileta Mzumbe University, Mkinga Campus ameiongezea ladha na utamu fahari ya elimu ndani ya Mkoa wa Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze sana Wizara kwa kuisimamia Miradi hii ya HEET. Tumeitembelea miradi hii value for money unaiona na wakandarasi wazawa wamepewa nafasi. Mfano Mradi ule wa Mloganzila pale mkandarasi mzawa kama Mohamed Builders ameufanya mradi vizuri na unamalizika kwa wakati. Miradi ile iko takriban 70%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo, ninaunga mkono hoja, bajeti hii tuipitishe kwa kishindo. Shukrani sana. (Makofi)