Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kutoa mchango wangu. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na naibu wake kwa kazi nzuri ambayo kwa kweli wanaendelea kuifanya. Wamefanya vizuri na wanaendelea kufanya vizuri. Pia niwapongeze Katibu Mkuu na watendaji wa taasisi zote zilizoko chini ya Wizara yake; kwa kweli wanafanya vizuri, hongera sana kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati ninachangia kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu nilitamka nikasema kwamba maadui wakubwa wa Tanzania wako wanne, na nikawataja. Juzi Mheshimiwa Rais wa Kenya ametutajia maadui hao. Leo ninasema maadui wale wameongezeka, sasa wako sita na nitawataja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, adui wa kwanza wa nchi yetu ni umaskini mkubwa, adui wa pili ni ujinga, adui wa tatu ni maradhi, adui wa nne ni ukosefu wa ajira, adui wa tano ni uchumi mdogo wa nchi yetu, adui wa sita ni rushwa kwenye nchi yetu na maeneo mbalimbali na wa saba ni ukosefu wa uwajibikaji na uadilifu katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maadui hawa tutaweza kupambana nao vizuri ikiwa Wizara yetu ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itatusaidia sana kwenye hili. Hatuwezi kuondokana na maadui hao bila kuwa na maarifa ya kutosha, bila kuwa na ujuzi wa kutosha, bila kutumia elimu kubadilisha tabia zetu na mienendo yetu. Mienendo yetu inaweza ikabadilika kama tutakuwa na maarifa ya kutosha. Kwa hiyo kazi hii ni ya Wizara hii. Tutapambana na rushwa kwa kuwaelimisha watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kazi ya Wizara hii wanaweza kutupa ujuzi kuhusu namna ya kupambana na rushwa, namna ya kupambana na umaskini, namna ya kupambana na maradhi, namna ya kutengeneza ajira na namna ya kutumia teknolojia mbalimbali. Ndiyo maana Wizara hii inaitwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunajua, kwamba hakuna nchi inayoweza ikaendelea bila hivyo vitu kutiliwa mkazo. Kwa hiyo ninasema kwamba wanafanya vizuri sana. Kutokana na hilo ninampongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa kuongeza bajeti ya Wizara ya Elimu. Sasa hivi bajeti ni zaidi ya 2,000,000,000,000 inayokwenda Wizara ya Elimu ili kutekeleza sera mbalimbali. Huu ni ujasiri mkubwa, haya ni maono makubwa. Tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa maamuzi haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema vyuo vitapambana na hao maadui; ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri. Wamekuwa wakijibu maswali na wamekuwa wakitueleza; sisi Mkoa wa Songwe tumekuwa tukiomba vyuo; na ni mkoa wa mwisho kuanzishwa, ni mchanga. Bahati mbaya hatuna chuo lakini wanasema tuna chuo kimoja kiko kule chini mpakani, kilometa 130 kutoka pale Vwawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri, ametuambia tunajenga Chuo cha VETA cha Mkoa, tunashukuru sana. Tunaomba basi kile Chuo sasa kikamilike. Kisipokamilika kile chuo, vijana wetu wataendelea kukosa ujuzi, vijana wetu hawataweza kujitegemea, umaskini utaendelea kuwepo na maarifa yataendelea kukosekana. Tunaomba kije haraka. Mheshimiwa Waziri ajitahidi akamilishe kile chuo ili angalau kitoe mchango mkubwa na sisi Wanasongwe na Wanavwawa tuondokane na hao maadui ambao nimewasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapotaka vyuo kwamba tunahitaji vyuo, wengi wanasema ni huduma, lakini kwa tafsiri yangu ninasema vyuo siyo huduma. Ninasema vyuo vinatupatia maarifa, ujuzi na umahiri wa kuweza kufanya mambo mbalimbali hapa duniani. Vyuo ni uchumi, vyuo ni biashara, vyuo ni ajira na vyuo ni viwanda kwa sababu utawatayarisha watu na utawachakata. Kile chuo ni kiwanda cha kuwachakata na kutengeneza ile malighafi ili wawe na maarifa ya kutosha na ndiyo maana, kasi ya maendeleo ya nchi yetu itakuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji hao ili wale Wanambozi wanaozalisha mahindi kwa wingi, wanaozalisha kahawa kwa wingi na wanaozalisha maparachichi kwa wingi waondokane na kuuza kama malighafi bali watengeneze viwanda vya kuongeza thamani ili tupate uchumi mkubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji na tumetenga maeneo. Kata ya Ipunga tuna ekari 308 tumetenga kwa ajili ya chuo, bado hatujapata. Kata ya Nyimbili tumeweka eneo zuri pale Sasanda kuna ekari 700 tumetenga ekari 200 kwa ajili ya vyuo. Pale Kata ya Hasamba tumetenga maeneo zaidi ya ekari 125 zipo, maeneo yapo. Tunahitaji na tunaamini tukijenga vyuo kwenye maeneo yale, tutaweza kupata fedha za kigeni nyingi. Wazambia, Wamalawi, Wakongo na wengine watakuja kusoma kama sisi tunavyokwenda kusoma Ulaya na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tufike mahali vyuo vilivyopo katika nchi yetu hii, watu watoke katika maeneo mbalimbali waje kusoma hapa kwetu. Mazingira ni mazuri, tuboreshe maeneo. (Makofi)

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ubora wa maeneo...

MWENYEKITI: Mheshimiwa Japhet Hasunga, kuna taarifa.

TAARIFA

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninaomba kumpa taarifa mzungumzaji ndugu yangu Mheshimiwa Hasunga asiwe na wasiwasi na Mheshimiwa Rais kukamilisha hizo VETA kwa sababu amekuta shule za amali ziko tisa nchi nzima. Leo zimekamilika shule 103. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Japhet Hasunga unaipokea taarifa hiyo?

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea kwa mikono miwili. Ninataka kuzungumzia mabadiliko makubwa ambayo Wizara wameanzisha. Hii ya mitaala ambayo wameibadilisha (mitaala ya elimu ya shule ya msingi na sekondari). Wamefanya jambo nzuri sana, lakini mitaala hii tunataka hata kwenye vyuo, vyuo wavisimamie navyo vibadilishe viwe na mitaala inayokidhi mahitaji ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo pale bado pana changamoto. Wakati tunakwenda tunahitaji kwenye vyuo tuboreshe mitaala. Nilikuwa ninaangalia vyuo bora Tanzania, ambavyo kwenye dunia ni vya ngapi ambacho ni chuo bora Tanzania ni cha ngapi duniani. Sitaki kusema na sitaki kutaja vyuo hapa maana yake nikitaja itakuwa aibu na itakuwa kama ninatangaza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niseme ukiingia kwenye website ukatafuta vyuo bora Tanzania ni vya ngapi duniani tuko mbali sana, tuko mbali sana. Ni kwa nini? Kwa sababu hatujaweka mkazo namna ya kuviendesha vyuo vyetu ili tuhakikishe kwamba professors na wahadhiri wafanye machapisho ya kutosha, wafanye utafiti wa kutosha, watunge vitabu na mambo mengine yote ili yasaidie katika kuleta maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda ninataka niseme wanafanya kazi nzuri na sisi tutawaunga mkono na tutaendelea kuiunga mkono kuhakikisha maendeleo makubwa yanapatikana kupitia Wizara yetu ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninakushukuru sana.