Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Msalala
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MABULA J. MAGANGILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii. Nami ninaomba nianze kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan; vilevile Waziri, Mheshimiwa Profesa Mkenda pamoja na Naibu Waziri Mheshimiwa Wanu Hafidh; kwanza kabisa kwa kuamua kutekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa sera hii, ni mageuzi makubwa yanayomgusa kila Mtanzania; na hii inathibitisha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania humgusa kila Mtanzania. Utekelezaji wa elimu ya lazima ya miaka 10, kwa kweli hatuwezi tu kujua ni kwa namna gani Mheshimiwa Rais amekwenda kutatua tatizo la watoto waliokuwa wakifika darasa la saba wanakwenda kuolewa; tatizo la watoto waliokuwa wanashindwa kumaliza sekondari kwa sababu ya umbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunapokwenda kutekeleza elimu ya lazima, maana yake ni kwamba Mheshimiwa Rais Samia amekwenda kukubaliana na kutekeleza sera ya sekondari kila kijiji. Awamu ya Nne ilitekeleza sekondari kila kata, leo hii kwa sera hii tunakwenda kutekeleza sekondari kila Kijiji; ambapo mtoto akiingia darasa la kwanza, anatoka akiwa form four. Jamani! haya ni mageuzi makubwa mno. Mheshimiwa Rais amechukua maamuzi makubwa mno ya kuwasogezea huduma watoto wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kule jimboni kwetu bado watoto wetu wanasafiri kilometa 10 hadi 15 kwenda kutafuta sekondari. Mtoto kutoka Matinje kwenda Butondoro; kutoka Nyangarata, Kalole, aende Lunguya. Kutoka Mwankima, Igungu aende Mwaruguru ni umbali mrefu mno. Mtoto huyu kwa mazingira ya kawaida hawezi kumaliza shule. Wanaanza 100 wanamaliza 60. Kwa mazingira haya na kwa mageuzi makubwa haya tuna uhakika wa watoto wetu wengi sasa wanakwenda kupata elimu ya sekondari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mageuzi ya kuamua kujenga VETA kila wilaya; ujenzi wa VETA kila wilaya; na Waheshimiwa Wabunge ninaomba niwaambie, kwamba VETA hizi si zile VETA ambazo zilipendwa; ni VETA ambazo zimewekewa miundombinu ya kisasa. Mimi ni mjumbe wa Kamati hii, nimetembelea hizo VETA hata mimi nilikuwa siamini, lakini ukifika VETA zetu sasa hivi zinachukua watoto wa aina zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwenda kwenye VETA unakuta mtoto ni mlemavu hana mikono yote, lakini leo ni architecture, anachora ramani za majengo. Haya yanawezekana kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa hiyo kwa kweli niipongeze sana Serikali hii ya Awamu ya Sita kwa kuamua kutekeleza sera hii ya elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa kampasi za vyuo vikuu katika mikoa yote ambayo haina vyuo vikuu; jamani, haya yanawezekana kwenye awamu ya sita pekee yake. Idadi hii ni kubwa mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwetu sisi Jimbo la Msalala tumepata angalau Training Center ya wachimbaji wadogo pale Segese ambayo inatokana na Serikali hii hii. Kwa hiyo, niseme tu kwamba tuendelee kuipongeza Serikali na kuendelea kupitisha bajeti hii kwa kishindo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wito wangu sasa, TAMISEMI wauchukue utekelezaji huu. Kwetu sisi ukizungumza, tuna shule za msingi 122, tuna sekondari 26 pekee yake. Kwa utekelezaji wa sera hii wa sekondari kila kijiji, tunahitaji madarasa mapya 166, ambayo leo hii kwenye shule za msingi tuna watoto 92,000, sekondari tuna watoto 15,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiendelea na utekelezaji wa sera hii, sekondari mwaka 2028 kuna watoto 17,000 wanaingia form one. TAMISEMI wasikie na waanze utekelezaji sasa, tusisubirie mwaka 2028, tutafeli. Idadi hii ni kubwa mno, mageuzi haya ni makubwa mno, ni lazima tuone umuhimu wake. Jambo hili haliwezekani likarudi nyuma, haya ndiyo maendeleo na hii ndiyo kazi na utu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokuwa na Taifa lililoelimika kuanzia chini Taifa linaloajirika; mageuzi haya yanakwenda kutoa ajira kwa vijana wetu waliohitimu fani ya ualimu ambao walikuwa wamekata tamaa; mageuzi haya yanahitaji walimu 40,000, ni ajira za kutosha kwa Watanzania ambao walikuwa wanajiuliza hivi tulisoma ualimu kwa ajili ya nini. Hata ikitokea walimu tukaona kama vile hawatoshi, sasa hivi sisi wenyewe Waheshimiwa Wabunge hapa ni mashahidi, tumejifunza mambo mangapi kupitia simu zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri na sera hii inataka somo la biashara liwe ni somo la lazima kwa watoto wetu wa sekondari; itakapotokea upungufu wa walimu Wizara iangalie topic ambazo zinaweza kufundishwa kwa kutumia AI. Kwani balance sheet, book keeping, trial balance haiwezi kufundishwa jamani na AI?
Mheshimiwa Mwenyekiti, twende tukaanze kufundisha wafanyabiashara tusifundishe wahasibu, tuwafundishe wanasayansi, tusifundishe walimu wa sayansi, tukafundishe wafanyabiashara kwa wingi kuliko wahasibu ili wafanyabiashara hawa wawaajiri wahasibu. Tukiendelea kufundisha wahasibu wengi kuliko wafanyabiashara watakwenda kufanya kazi wapi? Kwa hiyo mitaala yetu iende ikajikite huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)