Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Agnes Mathew Marwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Nianze moja kwa moja kwa kumpongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa jambo zuri analolifanya la kutoa scholarship kwa masomo ya vyuo vikuu nje ya nchi na ndani ya nchi kwa watoto na hasa watoto wa maskini wasiyojiweza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninampongeza sana Waziri Profesa Mkenda na Naibu wake pamoja na Wizara nzima kwa kazi nzuri wanayoifanya na hasa kwa ubunifu walioufanya wa huu mpango wa SIS (School Information System). Hiki ni kitu kizuri kilichofanyika cha kwamba mifumo inasomana, kila shule nchi nzima wanakuwa wanaona kwamba hapa kuna walimu kiasi fulani, hapa kuna jambo fulani linalohusiana na elimu, huu ubunifu kwa kweli ni mzuri sana na ni ubunifu unaostahili kuendelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kutokana na ubunifu huo, Mkoani kwangu Mara imekuwa ni sehemu ambayo tuna malalamiko ya muda mrefu ya walimu, walimu ni wachache sana na hasa kule Jimbo langu la Musoma Vijijini, kwa kweli walimu ni wachache sana wanafunzi ni wengi mno. Naamini kabisa hiki kilio yawezekana kwa vijijini ni maeneo mengi nchi nzima, kwa hiyo niombe jambo hili lifanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika masomo ya biashara pia kumekuwa na wimbi la ukosefu wa ajira. Ni ukweli usiyopingika ni kwamba hawawezi watu wote wakaajiriwa Serikalini, kutokana na hili ningeomba somo la biashara liwe ni somo muhimu sana kuanzia chini mpaka juu kwa maana ya kuwajenga Watanzania au vijana wetu wa Kitanzania kwenye soko la ajira wanapomaliza elimu za juu basi wanaweza kujiajiri wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hili ninamshukuru sana Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ajira nyingi sana kwa walimu, kwa kweli ametoa ajira nyingi sana kwa walimu, Mwenyezi Mungu ambariki sana. Ninaomba Wizara iangalie kwa undani zaidi kuna vijana ambao wamesoma masomo ya biashara na wako mtaani hawana kazi, basi waangalie mpangokazi wa kuwatengenezea ajira vijana hawa, wawashindanishe hili na wao sasa waende kufundisha somo hili la biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwa walimu, kuna changamoto kubwa sana ya kupandishwa madaraja, kupewa posho zao, lakini pia walimu wanacheleweshewa mishahara. Niombe suala hili Wizara ilifanyie kazi. Kwa kweli walimu hawa jamani ni watu ambao tunapaswa kuwajali sana. Tunapaswa kuwa-motivate kwa kila hali kwa sababu ni watu ambao wanatutunzia watoto wetu, tena kwa kipindi hiki kwa karne hii, Walimu wamekuwa sasa kama walezi, mtoto wa miaka mitatu anapelekwa shule. Kwa hiyo, niombe Wizara iwaangalie walimu kwa jicho la ziada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu hawa mazingira wanayoishi na hasa kwa jiografia ya Mkoa wangu wa Mara, kwa kweli jiografia imekaa vibaya, wanakaa mbalimbali. Mwalimu anafundisha Nyamitwe B, lakini anakaa umbali wa kilometa 10 kutoka pale anapofundishia. Kwa hiyo niombe Serikali iangalie jinsi gani ya kuwakopesha usafiri wa bei nafuu ili na wao waweze kufika kwa wakati, lakini wanapofika shuleni angalau na wao wanakuwa tofauti na wanafunzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwalimu akifika shuleni ukimwangalia miguu ana vumbi ndugu zangu, tuwaonee huruma walimu hawa kwa sababu wanafanya kazi ngumu sana. Pia tuwakumbuke kwenye hardship allowance yaani posho inayotakiwa katika kufanya kazi kwenye mazingira magumu. Walimu wao wamekuwa wakituomba na hasa mimi pale Musoma Mjini katika Jimbo langu pendwa, walimu nilikaa nao siku moja wakaniomba, wakaniambia Mheshimiwa nenda katuwakilishie hili jambo kwamba na sisi tunaomba basi japo watujali tunapofanya kazi kwenye mazingira magumu na sisi kama walimu tupate angalau allowance kwa ajili ya mazingira magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hili jambo la Sera ya Elimu ya Mwaka 2023 la kuongeza ufaulu, ni jambo zuzuri sana na limekwenda vizuri sana lakini kuna mikoa kama Mkoa wa Simiyu, Mkoa wa Mara, Mkoa wa Geita kwetu bado watoto wanarudi mchana nyumbani na jioni wanarudi tena shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili kwa kweli limekuwa likishusha sana ufaulu wa watoto wa shule; ukizingatia huko njiani, na hasa kwa wale ambao walinichagua mimi, wanawake; watoto wetu wa kike, wanapata majaribu mengi sana kutokana na hali hii kutokana uwepo wa bodaboda huko njiani. Hivyo, watoto wengine wanaweza wakashawishiwa kwa chipsi huko njiani kabla hawajafika nyumbani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe Serikali iangalie namna ya kukaa na wazazi, wazazi wachangie kiasi fulani; lakini pia na Serikali i-top-up ili kusudi watoto hawa wapate chakula, wasiwe wanarudi nyumbani mchana na kurudi jioni. Kwa hiyo niombe sana sana sana, niombe sana Serikali iwaangalie walimu hawa kwa jicho la kipekee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamalizia kwa kusema, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kweli ni mama mzazi, ni mama ambaye ametuonyesha kwamba anapenda sana kuipandisha elimu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niwaombe sana, ndugu zangu, ndugu zangu, Wizara husika, ninaamini kabisa liko pale jembe letu; Mheshimiwa Wanu, mchapakazi kabisa, anaonekana kila siku kazini; vilevile yupo kaka yetu Profesa Mkenda, kwa kweli ni wachapa kazi kwelikweli. Ninaomba waliangalie hili jambo ili wamsaidie mama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuipandisha elimu hii walimu waangaliwe wapewe kipaumbele. Walimu wakipewa kipaumbele angalau wakawa vizuri na wao, ninaamini kabisa hata watoto watakuwa wanawaangalia vizuri, hawatakuwa wanawaza mawazo ya tuition na vitu vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru sana Serikali yangu ya Chama Cha Mapinduzi, Serikali sikivu; ninaamini kabisa kupitia mpango huu wa mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan elimu itakwenda juu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja asilimia mia kwa mia. Mungu awabariki sana, ahsante sana. (Makofi)