Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Dr. Regina Christopher Malima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. DKT. REGINA C. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nikushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia hotuba muhimu sana katika Wizara ya Elimu na Teknolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kwanza kabisa kupongeza wasilisho ambalo limefanywa na Mheshimiwa Waziri. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri Profesa Mkenda pamoja na Msaidizi wake, Mheshimiwa Wanu na timu yote ya wataalam katika Wizara hii. Zaidi ninamshukuru sana Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna uwekezaji mkubwa ambao wananchi wanapaswa kufahamu ambao umefanyika katika sekta ya elimu, basi ni Wizara hii kuchukua jukumu kubwa la kuleta mageuzi katika sekta ya elimu nchini. Mengi yamesemwa na Wabunge wenzangu na sintotaka nirudie sana, lakini niendelee kupongeza juhudi za Wizara hii katika kupanua miundombinu kupitia Mradi wa HEET (Higher Education for Economic Transformation). Mradi huu unatekeleza ujenzi wa campus mpya 16 katika nchi yetu. Hili ni jambo la kupongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, kuna kozi maalum ya kuwainua wanawake wanaotoka kwenye mazingira au kaya maskini kupitia Mradi huu wa HEET. Mradi huu katika kuendesha programu hii wanashirikiana na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Mpaka sasa wanafunzi zaidi au vijana zaidi ya 711 wamenufaika na 137 wanatokea Zanzibar, jambo hili ni la kupongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nina hoja mbili tu na kama muda hautaruhusu nitaleta hoja binafsi kwa ajili ya haya ambayo ninataka kuyasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza kabisa ninatambua Wizara hii ipo katika kupitia Sera ya Elimu ya Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023 pamoja na mapitio ya sheria na mitaala. Kama tunavyofahamu nchi yetu iko katika changamoto ya mmomonyoko wa maadili, jambo hili linapaswa kuchukuliwa kitaifa, ajenda hii ni ya msingi sana kuitazama katika jicho la kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba tu Wizara hii kupitia wataalam wake pamoja na taasisi nyingine zilizoko chini ya Wizara kuanzishwa rasmi kwa somo la maadili kama somo linalojitegemea katika mfumo wa elimu. Kwa nini ninasema hivyo? Tafiti zinaonyesha kabisa kwamba nchi yetu iko kwenye mmomonyoko mkubwa wa maadili, tunafanya nini kunasua kizazi chetu kutokana na changamoto hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya juhudi kubwa sana katika kutengeneza miundombinu, katika kuboresha mambo muhimu katika sekta ya elimu, lakini haya yote yatakuwa bure kama maadili tuliyonayo katika Taifa hili kwa sasa yataendelea kubaki hivyo. Kwa hiyo, niseme tu kwamba kuna mwenendo wa maadili ambao siyo mzuri katika jamii na tafiti zinaonyesha, lakini pia tunaona nidhamu, vitendo vya rushwa, vitendo vya rushwa hivi haviji kwa bahati mbaya, hivi ni mwendelezo tu wa tabia ambazo yumkini mtu hakupata malezi katika utoto wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala ya uadilifu na uzalendo yote haya yamekosekana katika nchi, elimu bora bila maadili ni bure. Kwa maana hiyo, ninapendekeza katika Wizara hii rasmi tuweke somo la maadili kama somo linalojitegemea. Niombe Wabunge wenzangu waniunge mkono katika hili kwa sababu bila maadili nchi yetu itaendelea kupata shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia vitendo mbalimbali ambavyo Serikali inatengeneza miundombinu, lakini vijana wanaharibu, hili siyo jambo la kufumbia macho. Niombe Wizara ya Profesa Mkenda iliangalie jambo hili kwa umakini na somo hili liwe ni somo la lazima katika ngazi ya elimu ya msingi, awali lakini pia sekondari na hata vyuo lijitegemee, liwe na maudhui maalum ambayo yataonesha namna ambavyo jamii au vijana wetu na jamii kwa ujumla wanaopaswa kuwa na kuna faida nyingi tu katika kuweka somo la maadili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo nchi ambazo zimeendelea sana baada ya kuwa na mifumo kama hii, Profesa Muhongo aliongelea habari ya nchi kama Japan, Singapore, South Korea, kuna Finland. Nchi hizi ni nchi ambazo zimeendelea, wana somo la maadili katika mitaala yao na linajitegemea kwa namna fulani na limeleta heshima kwa hizi nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mifano Barani Afrika tunayo Nchi ya Rwanda, Nchi ya Rwanda sasa hivi wana somo linaloitwa values and ethics. Pia tuna Nchi ya Kenya wana somo linaitwa life skills education. Tuna Nchi ya South Africa wana somo linaitwa life orientation, Nchi ya Ghana hawa wana somo linaitwa religious and moral education. Yote haya yametengeneza msingi wa maadili katika nchi yao na tumeona namna ambavyo wanapiga hatua katika masuala ya maadili na namna ambavyo vijana wameendelea kuwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nipendekeze somo la maadili liwe ni somo, lazima katika mfumo wetu wa elimu na kuanzia sasa Wizara ijipange tu, nitaleta hoja binafsi kama ambavyo nimesema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la ubora wa elimu. Ubora wa elimu uko katika nyanja mbalimbali, lakini tumeona namna ambavyo Serikali imejipanga au imeboresha miundombinu na mambo kama hayo, lakini bado kuna changamoto kwa wahadhiri au wakufunzi wetu. Wabunge wenzangu walielezea hiyo kwa upana zaidi, lakini niendelee tu kusisitiza, bado tunahitaji motisha kwa wahadhiri na wakufunzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini ninasema hivyo? Hotuba ya Mheshimiwa Waziri imeonyesha namna ambavyo enrollment ya wanafunzi imeongezeka, lakini bado hatuoni namna ya ku-balance workload ya jambo hili. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri na hili nalo alifanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niunge hoja hii mkono. Ahsante sana. (Makofi)